Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano Nigeria: Namna Anthony Unuode alivyojitoa
Mwenye urefu wa futi sita na mwili uliojengeka nyama, Anthony Unuode,28, alikuwa na ndoto ya kulitumikia jeshi la Nigeria, lakini aliuawa na genge la watu waliokuwa kwenye maandamano dhidi ya ukatili wa polisi mjini Abuja, anaandika mwandishi wa BBC, Nduka Orjinmo baada ya kuhudhuria ibada ya kumbukumbu.
Wakati mamia ya mishumaa ikiwaka usiku, marafiki, familia na wageni walimzungumzia Anthony na tabia yake ya kutokuwa mbinafsi, huku wenginr wakionesha kuwa na uchungu kutokana na kifo chake.
Maandamano yalianza chini ya kampeni ya #EndSars, waandamanaji wakitaka kuvunjwa kwa kikosi maalumu cha polisi cha kupambana na uhalifu, ambacho maafisa wake wamekuwa mara kwa mara wamekuwa wakishutumiwa kutekeleza uhalifu kuanzia ukamataji kiholela na hata mauaji.
''Alikufa akipigania kitu hichohicho tulichokuwa tukikipigania,'' alisema mzungumzaji mmoja ambaye alikuwa mfuasi wake katika mtandao wa Twitter.
Waandamanaji wamesema kuwa Athony alikuwa mwerevu, magenge hayo ya watu wanaoshukiwa kukodishwa na wanasiasa kwa ajili ya kuvuruga maandamano walipowashambulia tarehe 11 mwezi Oktoba mjini Abuja, alijitokeza mbele na kuwakingia kifua alioweza kuwalinda akafanikiwa kukimbia akiwa na jeraha dogo mkononi.
Siku tatu baadae , majangili hao walifanya shambulio jingine kwa kutumia mapanga na fimbo kuvuruga maandamano katika barabara za Kubwa mjini Abuja.
Haijulikani kama Anthony alikuwa sehemu ya waandamanaji au alikuwa anatembea tu katika eneo hilo, lakini marafiki zake wanasema alikuwa na majeraha makubwa sana ya panga kwenye kichwa chake.
'Kulikuwa na masuala aliyokuwa akiyapinga'
Kwa jinsi damu ilivyokuwa ikimwagika kutoka kichwani, alivua shati lake na kufunga kwenye jeraha lake kichwani kisha alikimbia umbali wa maili kadhaa akitafuta msaada, hatimaye alinguka nje ya nyumba ya rafiki yake Muazu Suleiman.
''Nilimuweka ndani ya gari kisha niliendesha gari haraka sana mpaka kwenye hospitali yataifa, lakini tulipofika hakukuwa na gloves, pamba, hakukuwa na dawa. Nililazimika kwenda kununua vitu hivi nje,'' alisema Muazu.
''Walipotaka kufanya upasuaji walikuwa wakitumia mwanga kutoka kwenye simu za mkononi , baadhi ya vitendea kazi vilivyohitajika vilikuwa vimefungiwa,'' aliongeza.
Msemaji wa hospitali Tayo Hastrup alikana madai hayo, akisema kuwa ni ''uongo''.
Lakini kaka wa Anthony , Austin Unuode, pua alilalamika kuhusu hospitali hiyo, akisema kuwa matabibu ''hawakuweza kufanya baadhi ya vipimo kwa sababu hakukuwa na umeme''.
''Kulikuwa na vitu alipambana navyo, aliamini kuwa mambo yanapaswa kubadilika Nigeria,'' aliongeza.
Mama akosa mazishi
Eze Divine, ambaye alihudhuria shughuli ya kuwasha mishumaa iliyofanyika nyumbani kwa Anthony, ametoa wito haki ipatikane.
''Inasikitisha kuwa wale waliomuua hawatakamatwa kwasababu wanadhaminiwa na serikali.
''Kama tunataka kumalizika kwa vitendo vya ukatili wa polisi na wao wanatuma magenge ya watu, inatoa picha kuhusu serikali.
Ingeweza kuwa mimi, ingeweza kuwa mtu mwingine yeyote,'' alisema
Polisi wameiambia BBC kuwa walikuwa wakichunguza kifo cha Anthony, na hakuna aliyekamatwa mpaka sasa.
Anthony alimaliza elimu yake katika chuo kikuu cha Nasarawa state karibu na mji wa Abuja., alikuwa kielelezo cha vijana wadogo kwa kila namna.
Katika nchi ambayo mamilioni ya mamilioni ya waliohitimu hawana ajira na hupata msaada mdogo sana kutoka kwa jimbo, vijana wengi hutafuta njia binafsi ili kupata kipato.
Wakati wa kifo chake Anthony alikuwa akiendesha maduka mawili ya bahati nasibu mtandaoni.
''Tumempoteza, tangu baba yangu alipofariki, amekuwa akiitunza familia.
Mama yangu hakuwepo kuona mwili wake kwa kuwa yuko nje ya nchi,'' alisema kaka yake.
Makundi ya watu wenye silaha tu walisambazwa kwa ajili ya kuvuruga maandamano, lakini pia wanajeshi ambao siku mbili baada ya kifo cha Anthony-waliwafyatulia risasi waandamanaji huko Lekki.
Ingawa jeshi limekana kuwa watu wake walifyatua risasi, Amnesty International na mashuhuda wengine wanashuhudia kuwa jeshi liliwaua waandamanaji takribani 10.
Kabla ya kifo chake Anthony, alituma maombi ya kujiunga na jeshi, akiamini ni jukumu lake kusaidia mapambano dhidi ya Boko Haram.
''Mara nyingi alizungumzia kuhusu kujiunga na jeshi ili kupambana na Boko Haram.
Kinachofuata baada ya maandamano ya #EndSars
Siku moja baada ya mazishi ya Anthony, viongozi wa maandamano na maelfu ya watu wengine walifanya kipindi maalum mtandaoni kwa zaidi ya saa nne kujadili kinachofuata baada ya kumalizika kwa maandamano yaliyoshuhudia vijana wengi wakiingia barabarani.
''Ni nini kinachofuata? tunakwenda wapi baada ya hapa? Aliuliza mratibu Ebuka Obi-Uchendu alipofungua mazungumzo ya mtandao wa Zoom baada ya dakika moja ya kukaa kimya kwa heshima ya waliopoteza maisha.
Katika kujibu swali hilo mwanamuziki na mwanasheria Folarin Falana maarufu Falz, alisema: '' nina uhakika mambo hayatakuwa kama ilivyokuwa tena nchini Nigeria.
'' Kazi sasa imebaki kutoa elimu kwa raia, ili watu wafahamu haki zao na sheria.''
Wazungumzaji wengine wametaka vijana kujihusisha na siasa, na kutumia wingi wao kuwachagua wawakilishi wenye nguvu.
''Tulichokiona ni kuwa tunaweza kukusanyika na kupanga,'' alisema Feyikemi Abudu kutoka muungano wa watetezi wa wanawake, moja ya makundi makuu yaliyoshiriki maandamano hayo.
''Masuala ambayo tulikuwa tukifikiri kuwa hayawezi kufanyika kwa miezi au miaka yalifanikiwa kwa majuma kadhaa na hii ndio nguvu ambayo tunapaswa kuwa nayo,'' alisema.
Marafiki wa Anthony wanakiri kuwa Anthony aliandika ujumbe wa kama wa kinabii katika ukurasa wake wa twitter kabla ya kifo chake .
''Kwa kizazi changu cha Wanaijeria. Ninawapenda na nimewapatia heshima kubwa na ya kweli.
''Nguvu iliyo dhidi yetu inafanya kila iwezalo kuzima kampeni hii. Hali itakuwa mbaya lakini tusirudi nyuma. Anthony aliandika