Kinachofahamika kuhusu akaunti za Trump nchini China zilizozua mjadala

Donald Trump akiwa na Rais wa China Xi Jinping

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Ingawa kwa miaka vyombo vya habari Marekani vimehoji kuhusu madai dhidi ya Donald Trump kutolipa kodi, Jumatano hii New York Times lilibainisha kuwa kati ya mwaka 2013 na mwaka 2015 rais wa sasa alilipa kiasi cha dola za Marekani 188,561 nchini China.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, malipo hayo yanahusishwa na akaunti ya benki ambayo inamilikiwa na Trump nchini China, ambapo kwa miaka minne angejaribu kutafuta fursa za kibiashara.

Akaunti hiyo inasimamiwa na uongozi wa Trump International Hotels na michango yake kwa hazina ya China vina uhusiano na malipo ya kodi nchini humo.

Msemaji wa Trump aliliambia gazeti hilo kuwa akaunti hiyo ilianzishwa kwa ajili ya '' fursa muhimu katika sekta ya hoteli barani Asia.''

Tangu kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2016, msimamo wa Trump kwa China kumesababisha hali ya mabishano, ikiwemo kukosolewa kwa makampuni ya Marekani kufanya biashara nchini humo.

Mwezi Agosti, rais alisema alitaka kutoa motisha ya ushuru kwa kampuni za Marekani kuhamisha viwanda vyao kutoka China. Pia alitishia kuondoa mikataba ya serikali kutoka kwa kampuni hizo ambazo zinaendelea kuchukua kazi za China.

Rais alifika Ikulu akiituhumu China kuchukua faida ya kibiashara ya Marekani na amekuwa na "vita vya biashara", kuwekewa vizuizi kwa kampuni za China kama Huawei kufanya kazi Marekani kama ilivyo tuhuma dhidi ya Beijing kwa kutodhibiti virusi vya corona kwa wakati.

Wakati wa kampeni ya urais ya uchaguzi wa mwezi Novemba, Trump amekuwa akimkosoa sana mgombea wa Chama cha Democrat, Joe Biden, ambaye anasema atakuwa mpole kwa China.

Wakati huo huo, ametoa shutuma nzito kuhusu madai ya biashara na Hunter Biden, mtoto wa mgombea wa Joe Biden, huko nchini China.

Si mapato ya ushuru wala katika taarifa za kifedha ambazo Joe Biden ameweka wazi hadharani kuhusu kuwepo kwa dalili za mazungumzo na China.

Uwepo wa akaunti ya Trump nchini China ulibainishwa na The New York Times muda mfupi baada ya kuchapisha uchunguzi kuhusu mapato ya ushuru ya rais, ambaye, kulingana na gazeti hilo la Marekani, alilipa tu dola za kimarekani 750 kati ya 2016 na 2017, wakati alipoingia Ikulu.

Alan Garten, wakili wa Shirika la Trump, aliita hadithi ya NYT kuwa "uvumi" na akasema ilizua "mawazo yasiyofaa."

Garten aliliambia gazeti hilo kuwa uongozi wa Hoteli za Kimataifa za Trump "umefungua akaunti na benki ya China ambayo ilikuwa na ofisi nchini Marekani ili kulipa ushuru wa ndani."

"Hakuna makubaliano, wala shughuli yoyote au aina nyingine yoyote ya kibiashara iliyotekelezeka na, tangu 2015, ofisi imebaki kimya," Garten alisema.

"Ingawa akaunti ya benki imebaki wazi, haijawahi kutumiwa kwa madhumuni mengine yoyote," aliongeza katika mazungumzo yake na NYT.

Trump ana biashara nyingi za nje ya nchi, pamoja na viwanja vya mchezo wa gofu huko Scotland na Ireland na mlolongo wa hoteli za nyota tano.

Trump ana viwanja vya mchezo wa golf nchini Ireland

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mujibu wa The New York Times, Trump ana akaunti za benki nchini China, Uingereza na Ireland.

Gazeti la Marekani lilitoa maelezo ya jinsi Trump alivyotaka kufanya biashara katika nchi hiyo ya Asia, hasa tangu mwaka 2012 alipofungua ofisi huko Shanghai.

Habari ya ushuru kuhusu rais iliyochapishwa na NYT inaonesha kuwa rais aliwekeza kwa miaka kadhaa karibu dola za Kimarekani 192,000 katika kampuni tano ndogo zilizoundwa mahsusi kutafuta biashara nchini China.

Hatahivyo, mipango ya Trump huko China imekuwa chini ya uongozi wa Hoteli za Kimataifa za Trump, kupitia umiliki wa moja kwa moja wa Shirika la Maendeleo ya China ya THC, kwa mujibu wa NYT.