'Wanamgambo wa Kiislamu wawatorosha wafungwa 1,300' waliokuwa gerezani mjini Beni

Iliyochapishwa

Zaidi ya wafungwa 1,300 wametoroka gerezani Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo mjini Beni baada ya watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa kiislamu kushambulia eneo hilo, maafisa wameeleza.

Wanamgambo wa ADF wanadhaniwa kutekeleza shambulio hilo ili kuwatorosha wafuasi wa kundi hilo, meya ameeleza.

Wafungwa 100 pekee walisalia kwenye gereza la Kangbayi, meya huyo alisema.

Kikundi cha wapiganaji wa ADF kiliundwa zaidi ya miaka 20 iliyopita nchi jirani ya Uganda kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu.

Lilihamia Mashariki mwa Congo baada ya kufukuzwa na jeshi la Uganda kutoka kwenye ngome zake.

Kundi hili halijasema chochote kuhusu madai ya kuhusika na shambulio hilo.

Meya wa mji wa Beni, Modeste Bakwanamaha aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa washambuliaji walifika wakiwa katika kundi kubwa na kufanikiwa kuvunja mlango wa gereza kwa kutumia kifaa cha meme.

''Tunaamini kikundi cha ADF kimefanya tukio hili,'' alinukuliwa akisema.

Polisi waliweza kuwakamata wafungwa 14 waliotoroka, Redio ya nchini humo inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa,Okapi imeripoti.

Wafungwa wawili waliuawa kwa risasi wakati wa uvamizi, ulioanza saa kumi unusu saa za eneo hilo, Polisi walieleza kwenye ukurasa wa Twitter.

Msemaji wa jeshi mjini Beni, Luteni Anthony Malushay, ameiambia BBC kuwa operesheni ya kuwakamata wafungwa waliotoroka inaendelea.

Mwaka 2017, mamia ya wafungwa walitoroka kutoka kwenye gereza hilo hilo, linalowashikilia wanamgambo wengi- wakiwemo wapiganaji wa ADF

ADF ni moja kati ya makundi mengi ya waasi wanaofanya operesheni zake Mashariki mwa Congo, eneo lililo na utajiri wa madini ambalo serikali na vikosi vya Umoja wa Mataifa vimekuwa vikifanya jitihada ya kurejesha hali ya utulivu.

Kundi hilo limeshutumiwa kufanya vitendo vya ukatili mkubwa katika mkoa huo.

ADF limeripotiwa kuwaua raia 570 tangu jeshi la Congo lilipoanzisha operesheni dhidi yao mnamo Novemba mwaka jana.