Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafuriko yalivyokumba watu milioni sita ya Afrika Mashariki
Idadi ya watu waliokumbwa na mafuriko yatokanayo na mvua za msimu Afrika Mashariki imeongezeka mara tano zaidi katika kipindi cha miaka minne, takwimu za Umoja wa Mataifa zimeeleza.
Karibu watu milioni sita wameathirika mwaka huu huku milioni 1.5 kati yao wamelazimika kuyaacha makazi yao.
Sehrmu ya ukanda huo imerekodi mvua kubwa kuwahi kutokea katika kipindi cha karne moja
Mnamo 2019, tofauti kubwa ya joto kati ya pande za Mashariki na Magharibi mwa Bahari ya Hindi ndio ilikuwa sababu ya kuwepo kwa kwa mvua kubwa.
Takwimu zilizokusanywa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu zinatoa picha ya kutia wasiwasi, anaripoti Catherine Byaruhanga wa BBC.
Idadi ya watu walioathiriwa na mafuriko katika Afrika Mashariki imetoka milioni 1.1 mnamo 2016 hadi milioni nne mnamo 2019, hadi karibu milioni sita hadi mwaka huu - hii ni kabla ya mvua fupi, ambazo kawaida huongezeka mnamo Novemba na kuathiri nchi nyingi katika ukanda.
Sudan, moja ya nchi zilizoathirika zaidi, nyumba za watu 860,000 zimeharibiwa na zaidi ya watu 120 wamepoteza maisha , UN imesema ikinukuu takwimu za serikali.
Karibu kila jimbo nchini Sudan limekumbwa na mafuriko makubwa na katika nchi jirani ya Sudan Kusini, watu 800,000 wameathirika na watu 368,000 wakilazimishwa kuyaacha makazi yao.
"Jamii zote zimekimbilia kwenye maeneo ya juu ili kukwepa kuongezeka kwa maji," UN ilisema katika taarifa yake.
Baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika zaidi nchini Sudan Kusini mwezi uliopita, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wa nchini humo,, Alain Noudéhou, amesema kuwa "maeneo makubwa ya nchi kando ya Mto Nile sasa yako ndani ya maji".
Ethiopia, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu, watu milioni 1.1 wameathiriwa na mafuriko.
Burundi, Djibouti, Kenya, Rwanda, Somalia na Tanzania na Uganda pia zimejumuishwa katika takwimu hizo.