Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Mkuu wa WHO ana matumaini kuwa chanjo itapatikana mwishoni mwa 2020
Kuna matumaini kwamba chanjo yenye ufanisi dhidi ya virusi vya corona itakuwa tayari mwishoni mwa mwaka huu, Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ulimwengu unahitaji kutumia "rasilimali zote zilizopo" kumaliza ugonjwa huo, ikiwemo kupata chanjo.
"Kuna matumaini mwishoni mwa mwaka huu kwamba tunaweza kuwa na chanjo, kuna matumaini ," Dkt Tedros alisema Jumanne mwishoni mwa mkutano wa siku mbili wa bodi kuu ya WHO.
Hivi sasa, kuna karibu chanjo 40 tofauti kwenye majaribio - pamoja na ile inayotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford ambayo tayari iko katika hatua ya juu ya majaribio.
Lakini Dkt Tedros hakufafanua ni chanjo gani ambayo alidhani itapatikana mwishoni mwa mwaka.
Mpango wa WHO unakusudia kuzipa nchi fursa sawa za chanjo tisa, mara tu wanapopewa leseni na kupitishwa.
Hatahivyo, wanasayansi wameonya kuwa chanjo haitarudisha maisha kuwa ya kawaida kama ilivyozoeleka, kwani inaweza kuchukua miezi kuzalishwa, kusambazwa na kusimamiwa kwa kiwango kikubwa.
Kwa nini chanjo ya virusi vya corona ni muhimu?
Virusi husambaa kirahisi, na watu wengi duniani wako hatarini kupata maambukizi. Chanjo itatoa kinga kwa kuimarisha mfumo wa kinga utakaowezesha kupambana na virusi hivyo kutougua.
Hatua hii itafanya kuondolewa kwa amri za marufuku ya kutotoka nje, na kulegezwa kwa masharti ya kutochangamana.
Lini tutakuwa na chanjo?
Chanjo kawaida inaweza kuchukua miaka, kama sio miongo, kuitengeneza. Watafiti wanatarajia kufanikiwa katika miezi michache tu.
Wataalamu wengi wanafikiri chanjo itapatikana kwa kiasi kikubwa katikati ya mwaka 20121, karibu miezi 12-18.
Ni hatua kubwa sana kupigwa kisayanzi, lakini hakuna hakikisho kuwa itafanya kazi.
Lakini wanasayansi wana matumaini kwamba, ikiwa majaribio yatafanikiwa, basi idadi ndogo ya watu - kama wafanyakazi wa huduma ya afya - wanaweza kupewa chanjo kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Ikumbukwe kwamba virusi vinne vya corona tayari huzunguka miongoni mwa binadamu. Husababisha dalili za kawaida za mafua na hatuna chanjo kwa virusi hivyo mpaka sasa.