Surua DR Congo: Mwanaume anayetembea kwa saa sita ili kusambaza chanjo vijijini DR Congo

Iliyochapishwa

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikikabiliana na mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa wa surua duniani ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watoto 7,000.

Waziri wa afya anasema mlipuko huo umekomeshwa lakini wataalamu wanasema kutokana na viwango vya chini vya chanjo - asilimia 60 pekee - itachukuwa muda kidogo kabla ya mlipuko mwingine wa ugonjwa kushuhudiwa tena.

Mwanahabari Sara Assarsson na mpiga picha Johannes Tegner walikutana na wahudumu wa ambao wanafanya kila juhudi kuhakikisha wanawasilisha bidhaa hiyo muhimu kwa walengwa:

Japo huwezi ukabaini kutokana na viatu vyake visafi, Mulalu Lwesso mara kwa mara hutembea mwendo mrefu wa hadi saa sita kuwasilisha chanjo katika vituo vya afya vilivyoko maeneo ya mashambani.

"Nilianza kusomea uuguzi lakini sikukamilisha masomo kutokana na ukosefu wa karo - sasa natoa msaada wangu mahali unapohitajika. Ni mwendo mrefu na mimi nimeanza kuzeeka. Nimetembea njia hii kila mwezi tangu mwaka 1987," anasema.

Mhudumu huyu wa afya mwenye umri wa miaka 62 anatembea mwendo mrefu kutoka hospitali ya mji wa Mwenga - akitokwa na jasho kwa kubeba mabegani sanduku la chanjo ambalo limewekwa barafu ili kuzihifadhi zisiharibike na kwenda hadi kijijini kwao kuziwasilisha pamoja na dawa zingine na sindano.

Njia zingine za kusafirisha chanjo zinaweza kukumbwa na changamoto.

Malori yanaweza kukwama njiani kwa siku au wiki kadhaa baada ya mvua kubwa kunyesha na kuharibu barabara.

DR Congo, nchi ambayo ukubwa wake ni sawa na eneo zima la magharibi mwa Ulaya, ina karibu kilomita 2,000 sawa na (maili 1,250) ya barabara iliyowekwa lami.

Chanjo hazifanyi kazi zikiwekwa katika mazingira yenye kiwango cha juu cha joto.

Chanjo hizo zinatengenezwa India na kusafirishwa hadi mashariki mwa Goma ambao ni mji wa kiuchumi wa DR Congo, kisha zinasafirishwa kwa boti zikiwa kwenye vifaa maalumu vya kuzihifadhi na kupelekwa hadi hospitali kuu ya Bukavu.

"Zinastahili kuhifadhiwa katika sehemu hii ikiwa na kiwango cha kati ya nyuzi joto 6 hadi 7, lakini tunakuwa na umeme nyakati fulani za siku," anasema Oscar Mutama, ambaye ni msimamizi wa wa shughuli za usambazaji chanjo katika eneo zima la mkoa wa Kivu Kusini.

"Endapo umeme utapotea kwa muda mrefu hatuwezi kuwa na uhakikia chanjo hizi ziko katika hali ya juu ya ubora wake. Hivi karibuni tumebuni mbinu mpya ya kunakili bidhaa zilizoharibika, lakini hatuna uwezo wa kudhibiti ubora wa bidhaa."

Wakati mwingine Bw. Lwesso anaishiwa na fedha za kununua petroli kabla ya safari kukamilika, Hali inayomfanya Lwesso kubeba bidhaa hizo na kutembea mwendo wa kilomita 30 sawa na (maili 18)- baada ya timu yao kushauriana na kufikia uamuzi kwamba kutumia pikipiki itakuwa ghali sana

Mfumo wa afya uliopo sasa DR Congo haukidhi mahitaji huku eneo la mashariki mwa nchi hiyo linalokumbwa na machafuko yaliyosbabishwa na makundi yenye silaha yakichangia mzozo wa kibinadamu na umasikini uliowafanya wakazi kuishi katika mazingira magumu.

Baada ya chanjo kuwasilishwa katika vituo vya afya vijijini, mtoto Zawidi aliye na umri wa miezi tisa atapata chanjo yake ya kwanza.

Ndugu wake wote wamepewa chanjo dhidi ya polio, surua, pepo punda, na kifaduro.

Lakini mmoja wao alipata alipooza wakati nchi ilipokabiliwa na mlipuko wa hivi karibuni wa surua. "Hakuwa mgonjwa sana lakini niliingiwa na hofu kumhusu," anasema mama yao Tantine Katangalo.

Akiwa amembeba Zaiwidi mgongoni, anatembea mwendo wa karibu saa mbili hadi kituo cha afya. Kwasababu watu wanaishi mbali mbali na wametawayanyika ''sehemu tofauti milimani'', hakuna usafiri, kwa hivyo wazazi wanalazimika kuongeza juhudi kuwapeleka watoto wao kliniki, anasema Mkuu wa masuala ya matibabu wa Mwenga, Arsène Mubuto.

Makundi yaliyojihami yamewafanya maelfu ya watu kutoroka makwao kwa miaka kadhaa.

"Tunawaita wahanga wa mzozo," anasema Dk Mubuto. "Kukiwa na machafuko katika kijiji chao watu wanakimbilia kijiji jirani na kurejea makwao hali ikiwa shwari ."

Licha ya changamoto hizo, wakaazi wamefikia malengo ya kupiga vita ugonjwa wa surua : "Tulipogundua mlipuko wa ugonjwa huo mwaka 2019, tulichukua hatua za haraka kufanya kampeni ya pamoja ya chanjo kwa umma. Inaonekana ilifanikiwa."

Je surua ni nini?

Surua ni virusi vinavyosababisha mtoto kuwa na mafua , kuchimua mara kwa mara na kuwa na joto mwilini.

Siku chache baadaye mgonjwa anapata vipele mwili mzima ambavyo vinaanza usoni na kusambaa mwilini.

Wengi hupona , lakini surua inaweza kusababisha ulemavu wa muda mrefu. Inaweza kusababisha kifo hususan iwapo utasababisha homa ya mapafu ama uvimbe katika ubongo.

Inakadiriwa kwamba jumla ya watu 110,000 duniani hufariki kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.

"Wazazi Wengi huwaleta watoto wao hapa japo wanaishi mbali," anasema muuguzi Doms Mushimgwa katika kituo cha afya kilichoko karibu na Mwenga.

"Hakuna visa vya chanjo kukosa kufanya kazi."

"Katika maeneo mengine, nusu ya watoto hawapati chanjo kabisa," anasema Jorge Caravotta, mtaalamu wa afya katika Shirila la watoto la Umoja wa Mataifa, Unicef.

"Wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa ebola tulishuhudia kupungua kwa viwango vya chanjo za mara kwa mara kwa hadi asilimia 25, hali ambayo ilichangia mlipuko mkubwa wa surua kote nchini DR- Congo."

Na kama mkuu wa masuala ya chanjo hospitali katika maeneo ya vijijini Dkt Mubuto anasema: "Hata [siku moja] tukifikia asilimia 100 baadhi ya chanjo zitakuwa zimeharibika zikifikishwa hospitalini."

Zaidi ya watoto 7,000 walio na umri wa Chini ya miaka mitano wamefariki dunia katika mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa wa surua tangu mwanzo wa mwaka 2018, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya DR Congo.

Ukosefu wa lishe bora huwaweka katika hali hatari na pia hufanya kuwa ngumu kwa chanjo kufanya kazi kutokana na hali mbaya ya afya zao, anasema afisa wa Unicef Jorge Caravotta.

"Ni changamoto kubwa cha msingi ni kuwashawishi wazazi kuwapeleka watoto wao kwa chanjo na kuhakikisha wamepewa chanjo zote kwani ndio njia bora ya kuwakinga dhidi ya maradhi hatari ya utotoni "

"Watoto Wengi tunaowatibu baadhi yao wanakabiliwa na utapia mlo," anasema Aline Nabintu, daktari katika hospitali ya Wilaya ya Mwenga .

"Tunawapa vyakula vyenye virutubisho vya haraka kama njia ya dharura ya kuwaokoa na kuomba wapelekwe nyumbani kwasababu hatuna la ziada la kuwafanyia

"Tunashuhudia watoto wakiletwa hapa mara kwa mara kutafuta matibabu wakati wakiwa katika hali mbaya ya kiafya. Ni hali ya kusikitisha."

Lakini sio wote wanaonusurika huku vifo vya kinamama vikiendelea kuongezeka. Hata Japo vifo vya watoto wachanga vimepungua DR Congo tangu miaka ya 1990, karibu asilimia 8.5 ya watoto hawafikishi miaka mitano ya siku yao ya kuzaliwa.

"Chanjo ndio bima halisi ya maisha. Watoto wakiwa wagonjwa wazazi wengi hawawezi kumudu gharama ya kutafuta huduma za afya," anasema Bw. Mushimgwa. "Lakini ni muhimu kwa chanjo kuwasilishwa vituoni hapa kwa wakati unafaa ikiwa zinatakiwa kufanya kazi kama inavyostahili. La sivyo itakuwa usalama wa bure."