Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini akatwa mshahara kwa matumizi ya ndege ya jeshi

Nosiviwe Mapisa-Nqakula

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bi Mapisa-Nqakula akatwa mshahara na pesa hizo zitaelekezwa katika mfuko wa kukabiliana na virusi vya corona
Iliyochapishwa

Rais wa Afrika Kusini amemkata mshahara waziri wa ulinzi kwa miezi mitatu baada ya kuruhusu maafisa wa chama tawala kusafari kwa kutumia ndege ya jeshi hadi nchini Zimbambwe pamoja naye Septemba 9.

Nosiviwe Mapisa-Nqakula alishtumiwa kwa kuruhusu matumizi ya rasilimali ya taifa kwa sababu za siasa za chama.

Jeshi la nchi hiyo lilikuwa limeeleza kwamba waziri huyo alikuwa katika ziara rasmi ya kitaifa na kwamba aliwafanyia abiria wengine hisani kwa kuwabeba.

Lakini Rais Cyril Ramaphosa aliitaja hatua hiyo kama makosa.

Bi. Mapisa-Nqakula alienda mji mkuu wa Zimbambwe, Harare kuhudhuria mkutano uliokuwa umepangiwa kujadili masuala ya kanda.

Ujumbe kutoka chama tawala cha Afrika Kusini - African National Congress (ANC) - ulikuwa unahudhuria mkutano huo kwa mazungumzo ya dharura na chama tawala cha Zimbambwe Zanu-PF lengo lao likiwa ni kutatua mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini humo.

Lakini wasasiasa wa upinzani walimkosoa vikali waziri huyo kwa sababu aliandamana na ujumbe wa chama cha ANC.

Bwana Ramaphosa, ambaye kipindi anaingia madarakani aliahidi kumaliza sifa mbaya ya chama cha ANC baada ya mwongo mmoja wa kashfa za ufisadi, alisema kwamba "kwa kuandamana na wajumbe wa ANC kwa ndege aliokuwa anatumia, hakufanya uamuzi stahiki unaozingatia uongozi mzuri".

Matokeo yake, alisema ameamua kumkata mshahara Bi. Mapisa-Nqakula na pesa hizo zitaelekezwa katika mfuko wa kusaidia kukabiliana na janga la corona.

Wakati huo huo, chama cha upinzani cha Democratic Alliance kilisema hatua iliyochukuliwa na Bwana Ramaphosa haitoshi.

Suala hilo huenda likajadiliwa zaidi bungeni huku kukiwa na wito wa waziri huyo kufutwa kazi.