Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Masaibu ya Celine Njoki aliyebakwa na wanaume zaidi ya 20
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Celine Njoki ana umri wa miaka 34 ,na ni mama ya watoto 3 . Ni vigumu sana kwa mtu kuweka akilini mwake mahangaiko na uchungu mwingi ambao mama huyu amepitia katika miaka yake duniani .
Japo maisha yake yamekumbwa na huzuni kutokana na historia yake ya kubakwa mara tatu katika mazingira tofauti ,amepiga moyo konde kuishi maisha ya furaha kama alivyosimulia .
Simulizi ya ubakaji wa kila mara .
Mahangaiko yake kutokana na ubakaji yalianza usiku mmoja mwezi Juni mwaka wa 2016 hatasahau , wakati ule mama huyu wa watoto watatu hakuwa na makazi ya kuishi , kwa hiyo alikuwa analala mitaani, katika nyumba moja iliyokuwa mahame.
Anakumbuka saa za usiku wa manane alivamiwa na wanaume aliowahesabu kuwa kumi na watano, wote walim'baka mmoja baada ya mwingine , na kumuacha akiwa ameumizwa sehemu za siri kiasi cha kuhitaji upasuaji , alihitaji kushonwa mara kadhaa ili aweze kwenda haja zake kama kawaida .
"Ni kisa ambacho kilitokea ghafla , nilikuwa kwenye usingizi mzito sehemu niliyokuwa nina lala, wanangu wakati huo walikuwa wanaishi na shangazi yangu , sijui genge la wanaume hao lilitokea wapi lakini kitendo walichonifanyia walikuwa kama wanyama waliokuwa hawajali kilio au mayowe niliyokuwa napiga "Celine anakumbuka.
Aidha mama huyo anasema kuwa anashuku kuwa wanaume hao walikuwa wezi , waliokuwa wametekeleza uhalifu sehemu fulani na walikuwa hapo kugawa mali ya wizi. Ndiposa wakamvamia akiwa amelala mle.
Baada ya kisa hicho ilibidi asaidiwe na wasamaria wema , kwani alikuwa hana uwezo wa hata kutembea ilikuwa vigumu mno kwake. Kwa mwezi mmoja alipata matibabu , sio tu ya mwili wake bali pia alipitia matibabu ya kiakili kutokana na unyama aliyofanyiwa .Anatambua rafiki wake mmoja aliyemshika mkono kwa kumtambulisha kwa shirika mmoja la kuwasaidia wanawake , shirika hilo lilimpangia nyumba na kumsaidia kwa ajira .
Maisha yalionekana kurudi kama kawaida , na alihisi kuwa angeyasahau yaliomfanyikia , ila mengi yalikuwa yanamsubiri mbele.
Siku moja mnamo mwezi Desemba mwaka wa 2017 alipokuwa anatoka kazini , masaa ya jioni alivamiwa tena akiwa barabarani na wanaume aliyowahesabu kuwa wasita , wote walimbaka mmoja kwa mwengine . Maumivu na nyuzi za kale zote ziliraruka kutokana na kasi ya ubakaji .
"Hawa walionibaka hawakuniibia chochote , ninashangaa kwa kuwa haikuwa usiku lakini walifaulu kunishika kwa nguvu , baada ya kumaliza walichokifanya waliniacha hapo nikiwa hoi, nilimpigia simu rafiki wangu aliyekuja kuniokoa alinipeleka hospitalini . Krisimasi ya mwaka huo ilinipata nikiwa bado hospitalini ," anakumbuka Celine .
Celine alifanyiwa upasuaji mwengine sehemu za haja kubwa kwa kuwa alikuwa ameharibiwa tena wakati wa ubakaji .
Baada ya miezi minne , Aprili mwaka wa 2018 ubakaji mwengine ulimkuta
"Walivunja nyumba yangu wakati wa usiku , wanaume hao walikuwa wamevalia barakoa , lakini nadhani kuwa ni wale wale walionibaka barabarani , kwani nilizifahamu sauti zao na hata kunusa manukato waliokuwa nayo ." anakumbuka Celine
Hali hii ya ubakaji mara tatu , ilimuacha hoi , mwanadada huyu anakumbuka akiwa kama mtu aliyepagawa na ambaye hakuwa anaelewa kinachoendelea katika maisha yake , anakiri kuwa wakati huo alihisi kana kwamba alikuwa mzoga uliyosalia kuzikwa .
Kisa cha ubakaji wa mwisho kilimtoa moyo wa kuendelea na maisha yake , kwani alianza kujiuliza ni kwanini anakuwa muathiriwa wa ubakaji kila wakati ?
Vile vile alianza kuwa na uoga wa kutembea pekee yake kwani allikuwa na wasiwasi kila mara alipokuwa anakutana na wanaume barabarani .
Celine anasema kuwa visa hivyo vyote viliripotiwa katika vituo vya polisi lakini hadi sasa hakuna hata mmoja amekamatwa .
Pandashuka za malezi na maisha yake Celine
Celine Njoki alizaliwa katika mazingira ambayo ndoa kati ya wazazi wake haikudumu . Mwanadada huyu anakumbuka akiwa na miaka minne hivi mamake aliondoka na kakake aliyekuwa mdogo , tangu wakati huo Celine hakuwahi msikia wala kumuona mama yake .
"Mimi sijui sura ya mama yangu ilivyo ,ila jamaa wangu walikuwa wanasema kuwa muonekano wa sura yangu na mama ni kama pacha , mama alituacha na kaka yangu tukiwa wadogo , hatujui kilichojiri ila malezi ya utotoni mama hakuwepo "Celine anasema .
Baba yake Celine alifanya kila awezalo kuwapa watoto wake mapenzi ya mama na ya baba , na maisha ya kawaida . Celine alipohitimu miaka 7 baba yake aliaga dunia baada ya kuugua . katika umri mdogo Celine hakuelewa kifo kilimaanisha nini, wala hakuna aliyejitolea kuwafariji kwa kupoteza baba .Anachofahamu ni kuwa ghafla aligundua baba hayuko tena , aliachwa mikononi mwa bibi au nyanya .
Baada ya mazishi ya baba yake baadhi ya jamaa wa babake kwa mfano binamu wa baba na wajomba walianza kuishi kwao .
Wakawa wanalala nyumbani kwao , binamu zake walikuwa wamekuja kuishi huko kuendeleza masomo yao .
Ila wingu jeusi lilisubiri Celine katika utoto wake wa miaka 7 alianza kubakwa na kunajisiwa na binamu wa baba yake . Celine anasema kuwa binamu huyo alikuwa na miaka kati ya 25-26 kitu kilichoanza kama tabia ya binamu wa baba kumtomasa kiliendelea kuwa kitendo cha kila siku cha unajisi .
Binamu alimtishia kumuua ikiwa angetoboa siri iliyokuwa inaendelea mle nyumbani .
Mwanadada huyu hakujua wa kumgeukia , tabia yake ilibadilika mno na akawa msichana mtukutu na mwenye vituko . Hakuna mtu aliyekuwa anaelewa ni kwanini alikuwa na tabia za usumbufu.
Celine anasema kuwa alikuwa anaona aibu kumweleza mtu yeyote , hata bibi hakufahamu kuwa Celine alikuwa anapitia masaibu ya ubakaji kila siku.
Kitendo hiki kiliendelea tangu akiwa miaka 8-14 hadi wakati binamu wake aliondoka kule nyumbani kwao na ilisalia kuwa siri
Kushika Mimba .
Celine alipohitimu miaja 15 alianza uhusiano wa kimapenzi na kijana mmoja , Mwanadada huyu anasema kuwa kwa mara ya kwanza alihisi kupendwa , mara tu alishika mimba na akajifungua mtoto wa kwanza akiwa na miaka 16.
Maisha yalibadilika mno , alitelekezwa na walezi wake , na akaanza maisha ya malezi ya mtoto . Uhusiano wake na yule baba ya mtoto uliharibika wakati huo .
Mtoto alipofikisha mwaka mmoja na miezi kadhaa Celine na yule mpenzi wake walirudia mapenzi tena na akiwa na miaka 17 alijipata ujauzito wa pili .
Kipindi hicho baba ya watoto wake wawili alifanikiwa kusafiri Marekani kwa ajira , lakini wakati huo alikuwa anatuma fedha za matumizi kwake Celine .
"Jamaa wangu walikuwa hawataki hata kuniona , walinitizama kama msherati na ambaye hafai, hata mtoto wa pili nilijifungulia ndani ya nyumba nikiwa pekee yangu nusura nipoteze uhai wangu . Baada ya bibi kufariki ni shangazi mmoja tu aliyekuwa anasimama na mimi , kweli maisha yalikuwa machungu" Celine anasema
Baada ya miaka miwili baba ya watoto alirejea kutoka Marekani , waliamua kuanza maisha kama mke na mume , na hata Celine alishika mimba ya tatu , ila mambo yalikuwa tofauti . Mume wake alikuwa hajali , kwa mfano alikuwa na tabia ya kuwaleta wapenzi wengine ndani ya nyumba yao
"Nakumbuka nikiwa na mimba ya miezi 5 , mume wangu alirejea nyumbani na wanawake wawili wote walikuwa ni walevi. Wote watatu waliingia bafuni na kuanza kufanya ngono huku wakipiga kelele za kila aina , nilihisi kuwa watoto wangu wakubwa walikuwa wanayasikiza yaliokuwa yanafanyika , nilisongea pale bafuni na kumweleza mume wangu wapunguze kelele, pale pale alitoka kwa hasira na kuniburuza kwa nguvu hadi nje , alinirushia nguo pamoja na watoto wangu na kunieleza niondoke kwake " Celine anakumbuka
Mwanadada huyu anasema kuwa mume wake alimrushia fedha kama dola mia mbili , hapo ndipo alianzia maisha ya malezi ya watoto akiwa mzazi wa kipekee.
Maisha ya kuwalea watoto wake hayakuwa rahisi ndiposa wakati mwengine alijipata akilala mitaani au kwenye nyumba ambazo hazina watu .
Maisha yalivyo sasa
Watoto wake kwa sasa wana umri wa miaka 18 , 16 , 10 mtawalia. Mwezi februari mwaka huu alifunga ndoa na mumewe licha ya masaibu mengi maishani mwake , mume wake amemkubali pamoja na kuwaridhi wanae .
Celine ni mmoja wa wanawake ambao wanazungumzia sana kuhusu ubakaji kama njia ya kuhamasisha jamii , na pia kuhakikisha kuwa wasichana au mabinti wanaelewa jinsi ya kujikinga na kujilinda.