Mwanamke mmoja akamatwa akishukiwa kutuma barua yenye sumu kwenda Ikulu ya Marekani

Iliyochapishwa

Mwanamke mmoja amekamatwa akishukiwa kutuma kifurushi kilicho na sumu aina ya ricin kwenda kwa Rais wa Marekani,Donald Trump.Maafisa wa uhamiaji wa Marekani wameeleza.

Mwanamke huyo ambaye hajatajwa jina alikamatwa kwenye mpaka huko Buffalo, New York , akijaribu kuingia Marekani akitokea Canada, na anaripotiwa kukamatwa akiwa na silaha.

Barua iliyokuwa na sumu kali inaaminika kutoka nchini Canada, kwa mujibu wa wapelelezi.

Barua iligundulika juma lililopita kabla ya kufika ikulu ya Marekani.

Ricin ni sumu hatari ambayo ishawahi kutumiwa katika shambulio la kigaidi siku zililizopita.

Ricin huzalishwa kutoka kwa usindikaji wa maharagwe ya castor, mmea katika familia ya Euphorbiaceae. Mbegu zake hutumiwa kutengeneza sumu.

Ni sumu hatari, ambayo kumeza, kuvuta harufu yake au kudungwa sindano, kunaweza kusababisha kichefu chefu, kutapika, kutokwa na damu ndani mwili na kuzuia viungo muhimu vya ndani kukosa kufanya kazi na hatimaye kifo.

Serikali ya Trump haijasema chochote kuhusu ripoti hiyo.

Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na maafisa wa ulinzi wa siri wanachunguza barua hiyo ilitumwa kutoka wapi na ikiwa kuna nyengine zilitumwa kupitia huduma za posta za Marekani.

"Kwa sasa hakuna tishio linalojulikana kwa usalama wa umma ," FBI iliambia CNN katika taarifa siku ya Jumamosi.

Mshukiwa huyo anashukiwa kuwa huenda alituma sumu hiyo pia huko Texas, kwenye gereza na ofisi ya maafisa wa polisi.Taarifa ya Shirika la habari CNN limeeleza.

Uwepo wa sumu hiyo ulibainika na FBI .

Idara ya polisi nchini Canada ilisema siku ya Jumamosi kuwa inashirikiana na FBI kuchunguza barua hiyoiliyotumwa kwenda Ikulu ya Marekani.

Hakuna dawa ya kuikata makali

Mtu akishambuliwa na sumu hii anaweza kufariki baada ya kati ya saa 36 hadi 72, kulingana na kiwango cha dawa, kwa mjibu wa Kituo cha Marekani cha kudhibiti na Kuzuia magonjwa (CDC).

Ricin ilishawahi kutumiwa kufanya mashambulio ya kigaidi. Na inaweza kutengenezwa kuwa silaha kwa mfumo wa unga, gesi au chembe chembe.

Unaweza kusoma pia:

Ikulu ya White House na majengo mengine ya umma yameshawahi kupokea kifurushi cha sumo ya ricin.

Mwaka 2014, mwanamume mmoja katika jimbo la Mississippi alifungwa miaka 25 jela kwa kumtumia barua iliyokuwa na sumu ya ricin kwa rais wa zamani Barack Obama na maafisa wake wengine.

Miaka minne baadae, 2018, afisa mkongwe wa jeshi la wanamaji alishutumiwa kwa kutuma barua iliyokuwa na sumu kwa Pentagon na White House.