Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Simon Tu: Msafirishaji wa mihadarati afungwa gerezani baada ya kuligonga gari la polisi
Msafirishaji mmoja wa mihadarati amehukumiwa kifungo jela nchini Australia baada ya kugongana na magari mawili ya polisi yalioegeshwa .
Simon Tu alikuwa akisafirisha kilo 260 za dawa aina ya methamphetamines, wakati alipokosa mwelekeo na kugonga magari hayo Julai 2019.
Maafia wa polisi walilisaka gari hilo na kumtoa Tu , kabla ya kupata mihadarati hiyo yenye thamani ya hadi $95m.
Sasa amehukumiwa kifungo cha miaka sita na nusu jela.
Wakati alipokamatwa afisa wa polisi Glen baker aliambia vyombo vya habari kwamba ilikuwa miongoni mwa njia rahisi zaidi ya kumkamata mlanguzi wa mihadarati ambayo haijawahi kufanyika na maafia wa polisi wa kituo cha New South Wales ".
Mwaka uliopita , Tu aligonga magari hayo ya polisi ambayo yalikuwa hayana mtu ndani yake , na yalikuwa yameegeshwa nje ya kituo cha polisi cha Eastwood mjini Sidney , na kusababisha uharibifu mkubwa kwa gari moja la polisi .
Aliendesha gari hilo bila kusimama , lakini tukio hilo likanaswa katika kanda za video za CCTV na mashahidi wakailezea gari lake kwa polisi. Saa moja baadaye maafisa wa polisi walimkamata bwana Tu.
Aliwaambia kwamba alikuwa anapeleka chakula , lakini hatua yake ya kukataa kuwatazama machoni na kubabaika kuliwafanya maafia hao kulipekua gari hilo hatua iliofichua maboksi 13 yaliojazwa kilo za mihadarati ya methamphetamine, inayojulikana kama ice.
''Tu alikua na deni kubwa wakati huo hatua iliomfanya kutumia pombe na mihadarati kila siku'', ilisema mahakama ya Downing Centre District Court ..
Amedaiwa kuelezea kifungo chake gerezani kama mwamko mpya.
Hakimu Penny Hock alitoa hukumu yake siku ya Ijumaa.
''Ni uendeshaji mbaya wa gari wa mshukiwa huyo uliomfanya kujikuta katika mikono ya polisi'' , alisema.
Hakimu Hock alisema kwamba kukamatwa kwake kulikuwa kwa bahati mbaya kwa mshukiwa lakini faida kubwa kwa jamii.
Tu anaweza kuachiliwa na sheria ya kuwaachilia wafungwa wenye makosa madogo mwezi Julai 2023.
Huku matumizi ya dawa ya methamphetamine yakiwa yamepungua nchini Australia katika miaka ya hivi karibuni , serikali inasema kwamba uharibifu unaosababishwa na dawa hiyo unaongezeka.