Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ufyatuaji wa risasi Kenosha: Maandamano yatanda baada ya polisi kumpiga risasi mtu mweusi Marekani
Maandamano yameanza tena katika jimbo la Wisconsin nchini Marekani baada ya polisi kumpiga risasi kadhaa mtu mweusi mara kadhaa wakisema kwamba ilikuwa ni kujibu kile walichokiita mzozo uliotokea.
Mwanaume huyo aliyetambuliwa kwa jina Jacob Blake, yuko hali mahututi hospitalini.
Video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha Bwana Blake akipigwa risasi kwa nyuma wakati anajaribu kuingia kwenye gari katika mji wa Kenosha.
Mamlaka huko Kenosha imetangaza kuanza kutekelezwa kwa dharura hali ya kutotoka nje usiku baada ya kuzuka kwa maandamano kutokana na upigaji risasi huo.
Mamia ya watu wameandamana hadi makao makuu ya polisi Jumapili usiku. Magari yakachomwa moto huku waandamanaji wakiwa wanapiga makelele wakisema" Hatuwezi kurudi nyuma".
Katika tahadhari iliyotolewa kwa umma, polisi imesema wanaofanya biashara saa 24 wafikirie kuzifunga kwasababu ya wizi wa kimabavu na matukio ya ufyatuaji wa risasi.
Maafisa walitumia vitoza machozi kutawanya mamia ya waandamanaji waliokiuka hatua ya kusalia ya nje, ambayo imewekwa hadi Jumatatu saa moja asubuhi.
Gavana wa Wisconsin, Tony Evers ameshutumu tukio hilo la ufyatuaji wa risasi dhidi ya Bwana Blake ambaye inasemekana hakuwa na silaha.
"Wakati hatuna taarifa zote kwa sasa, tunachojua ni kwamba huyo sio mtu wa kwanza kupigwa risasi au kujeruhiwa au kuuawa kiholela mikononi mwa maafisa katika jimbo letu au nchini mwetu," alisema katika taarifa.
"Tunachopinga ni utumiaji wa nguvu kupita kiasi na pia jinsi mambo yanavyokuzwa haraka ikiwa ni suala la polisi na mtu mweusi huko Wisconsin."
Sasa hivi jina la Jacob Blake linasambaa sana kwenye mitandao ya kijamii huku maelfu ya watu wakiwa wametia saini wakitaka maafisa waliohusika na tukio hilo la ufyatuaji wa risasi wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
Nini kilichotokea?
Idara ya polisi huko Kenosha imesema kuwa "tukio hilo la ufyatuaji wa risasi lilitokea" muda mfupi baada ya saa kumi na moja jioni Jumapili.
Na kuongeza kwamba maafisa walitoa huduma ya kwanza kwa Bwana Blake, ambaye alipelekwa hospitali huko Milwaukee.
Hata hivyo hakuna taarifa zozote kuhusu kilichosababisha ufyatuaji huo wa risasi.
Idara ya haki ya Wisconsin inachunguza tukio hilo. Imesema kwamba maafisa waliohusika wameagizwa kwenda likizo ili uchunguzi ufanywe.
Katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, maafisa watatu wanaonekana wakionesha silaha zao kwa mwanaume anayesemekana kuwa ni Bwana Blake wakati anatembea kwenye eneo la kuegesha gari.
Na anapofungua mlango na kuegemea kwenye gari, afisa mmoja anaonekana akimshika shati lake na kufyatua risasi.
Kisha risasi saba zinasikika kwenye video hiyo, huku walioshuhudia tukio hilo wakisikika kupiga mayowe na kelele.
Afisa aliyehusika na tukio hilo bado hajatambuliwa rasmi.
Wakili maarufu wa haki za raia Ben Crump ameiambia CNN kwamba familia ya Bwana Blake ilikuwa imewasiliana naye kutafuta usaidizi.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, vijana watatu wa Bwana Blake walikuwa kwenye gari alilokuwa anaingia ndani wakati anapigwa risasi.
"Walimuona polisi akimpiga risasi baba yao. Watakuwa na mfadhaiko wa akili milele. Hatuwezi kuacha maafisa wa polisi waendelee kukiuka majukumu yao wanapotulinda," aliandika.
Alisema mauaji hayo yalitokea baada ya Bwana Blake kujaribu kumaliza mgogoro uliokuwa umetokea awali.
Walioshuhudia pia walizungumza na tovuti ya habari ya eneo la Kenosha kwamba Bwana Blake alikuwa amejaribu kutenganisha vita kati ya wanawake wawili kabla ya polisi kuwasili.
Ufyatuaji huo wa risasi unawadia wakati ambapo Marekani imeghubikwa na wasiwasi kuhusu unyama unaotekelezwa na polisi baada ya mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd mnamo mwezi Mei.
Afisa wa polisi mzungu alipiga goti juu ya shingo ya Bwana Floyd kwa takriban dakika 9 kabla ya kufa katika jimbo karibu na Wisconsin la Minnesota
Afisa huyo, Derek Chauvin, ameshtakiwa kwa mauaji.
Pia unaweza kutazama:
Aidha kifo cha Bwana Floyd kilisababisha maandamano ya Black Lives Matter kote Marekani na duniani.