Nyota wa Misri wa TikTok na Instagram aadhibiwa vikali kwa 'utovu wa maadili'

Iliyochapishwa

"Tulisalia na mshtuko. Hakuna hakufanya kosa lolote- dada yangu sio mhalifu," amesema Rahma al-Adham, akimzungumzia dada yake mdogo mshawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii nchini Misri.

Mawada, 22, mwanafunzi wa chuo kikuu, mwezi uliopita alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka maadili ya kifamilia Misri.

Alikamatwa Mei baada ya kuweka mtandani video kwenye mtandao wa TikTok na Instagram ambapo alikuwa anaigiza kuimba nyimbo maarufu na kucheza densi akiwa amevalia nguo za mitindo ya kisasa.

Mwendesha mashtaka alionesha kwamba video zake zilifuata mienendo isiyofaa.

Mawada anawafuasi zaidi ya milioni tatu katika mtandao wa TikTok, na wafuasi milioni 1.6 katika mtandao wa Instagram.

"Alichotaka ni kuwa maarufu na mashuhuri tu," Rahma anasema.

'Wasichana wa TikTok'

Mawada ni mmoja kati ya wanawake vijana waliofungwa jela mbali na kupigwa faini ya karibu dola 20,000 (£15,300; 17,000 euros).

Watano hao wanafahamika kama "TikTok girls" yaani "Wasichana wa TikTok". Mbali na Mawada, kundi hilo linajumuisha nyota mwingine katika mitandao ya kijamii anayefahamika kama, Haneen Hossam, na wengine watatu ambao hawakutajwa majina yao.

Rahma anasema dada yake alikuwa mwanamitindo katika mitandao ya kijamii na anafamika kwa majina ya mitindo kadhaa. "Alikuwa mtu mwenye shauku sana. Alikuwa na ndoto kubwa ya kuwa muigizaji wa kike.

"Kwanini yeye? Baadhi ya waigizaji wa kike mavazi yao yanachukuliwa kama mazuri yaani yenye kukubalika katika jamii. Hakuna anayewagusa au kuwataja," anauliza kwa hasira.

Kulingana na kundi la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, waendesha mashtaka walitumia picha 17 za Mawada dhidi yake kama ushahidi wa "mienendo yake isiyokubalika katika jamii".

Mawada alisema picha hizo zilivujishwa kutoka kwenye simu yake iliyoibiwa mwaka jana.

Rufaa dhidi ya kesi hiyo ni Agosti 17 licha ya kwamba Rahma hana matumaini kabisa ya kifungo cha dada yake kupunguzwa.

Baada ya kusikia uamuzi huo, Mawada alizimia, kwa mujibu kwa wakili wake, Ahmed Bahkiry. "Ilimuumiza moyo sana- mashtaka dhidi yake hayana msingi wowote."

"Gerezani sio suluhisho, hata kama baadhi ya video zake zinakwenda kinyume na maadili na utamaduni wetu," anaongeza. "Gereza hufanya watu kuwa wahalifu. Badala yake mamlaka ingeamua kugeukia vituo vya kurekebisha tabia."

Nchini Misri kinachoshuhudiwa ni hisia mchanganyiko dhidi ya kesi hiyo. Wengi wao ambao ni Waislamu wasiopendelea madabiliko, wanachukulia video za TikTok kama za Mawada kuwa utovu wa maadili.

Wengine wanasema wasichana hao walikuwa tu wanajiburudisha na hawastahili kuwa gerezani.

Huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakichukulia kufungwa kwa wasichana hao kama jaribio la mamlaka kukandamiza uhuru wa kujieleza na ishara ya kile kinachofahamika na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty kama "mbuni mpya za kukandamiza na udhibiti mitandao ya kijamii".

Kuna wanaharakati wanausema, kuna makumi ya maelfu ya wafungwa wa kisiasa nchini Misri ikiwemo wanaopigania uhuru, wenye misimamo ya Kiislamu, wanahabari na mawakili wa haki za binadamu.

Hata hivyo, rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi anasisitiza kwamba hakuna wafungwa wowote waliodhamiriwa nchini mwake, huku taifa hilo likihoji uhakika wa taarifa za ukosoaji za makundi ya haki za binadamu.

'Onyo kwa vijana'

Miongoni mwa wanaotaka wasichana hao kuachiliwa huru ni Tume ya Misri ya Haki na Uhuru, shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini Cairo.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Mohamed Lotfy, anasema kesi hiyo inaonesha wazi ubaguzi wa kijinsia.

"Wanawake wanaruhusiwa tu kujieleza kwenye mitandao ya kijamii kwa kufuata miongozo ya serikali," anasema. "Wasichana hao wanashutumiwa kwa kukiuka maadili ya kifamilia ya Misri, lakini hakuna ambaye amewahi kuelezea kinagaubaga maadili hayo."

Hata ikiwa wataachiliwa huru, Bwana Lotfy anasema, tayari kuna onyo lililoelekezwa kwa wasichana vijana.

"Mamlaka imeweka wazi: hauko huru kusema au kufanya unachotaka, hata kama hauna uhusiano wowote na siasa kabisa. Kuna yale ambayo haustahili kabisa kuyakiuka."

Katika miezi ya hivi karibuni, ofisi ya mwendesha mashtaka ya umma imetoa taarifa ikionesha kile inachokiita "Hatari iliyopo inayotishia vijana wetu kupotea kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii, ambao hawapati usimamizi mzuri".

Ilitoa wito kwa wazazi kusaidia vijana kutotumbukia kwenye mitindo ya maisha ya kiholela, wanapotafuta umaarufu na mafanikio".

"Wanafuata njia haramu kujitafutia pesa, kwa imani potofu kwamba hii ni aina fulani ya uhuru wa kujieleza," amesema.

Wakati huohuo, matokeo ya kile kilichotokea, Rahma anasema mama yao sasa hivi ni nadra sana kuondoka kwenye kitanda chake".

"Analia kila wakati," amesema. "Wakati mwingine huamka usiku na kuuliza ikiwa Mawada amerudi nyumbani."

Pia unaweza kutazama: