Marekani yatwaa mafuta ya Iran ya thamani ya mamilioni ya madola yaliyokuwa yanaelekea Venezuela

Chanzo cha picha, US Justice Department
Marekani yasema imechukua udhibiti wa meli nne za mafuta za Iran zilizokuwa zinaelekea Venezuela ikiwa ni uzuiaji wa kiwango kikubwa zaidi cha mafuta kuwahi kukamatwa.
Takriban mapipa milioni 1.1 ya mafuta yalikamatwa kwa usaidizi wa washirika wa kigeni, kulingana na Wizara ya Sheria ya Marekani.
Marekani imesema kwamba meli hizo zilikiuka vikwazo ilivyoiwekea Iran.
Balozi wa Iran nchini Venezuela alidai kwamba meli hizo na wamiliki wake havina uhusiano wowote na Iran.
Hakimu alitoa kibali cha kukamatwa kwa mafuta yaliokuwa meli hizo nne baada ya Marekani kufungua kesi mahakamani mwezi uliopita.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumma, Idara ya Sheria ya Marekani imesema kuwa imefanikiwa kukamata meli zilizokuwa zimebeba mafuta ya thamani cha mamilioni ya madola zilizokuwa zinasindikizwa na Jeshi la Iran la Islamic Revolution Guards Corps (IRGC)."
Jeshi la Iran la IRGC ni tawi la vikosi vya Iran ambavyo Marekani ilivitambua kama shirika la kigeni la ugaidi.
"Mafuta yaliyokamatwa sasa yapo chini ya ulinzi wa Marekani," taarifa hiyo imesema, bila kusema tukio hilo lilitokea wapi na lini?
Wizara ya Sheria ya Marekani imesema kwamba punde tu baada ya kutokea kwa tukio la kushikiliwa kwa meli hizo, jaribio la jeshi la Iran la kupanda meli nyengine kama hatua ya kukomboa mafuta yaliyokamatwa halikufanikiwa."
Afisa mwandamizi ameliambia Shirika la Habari la AP kwamba hakuna nguvu ya jeshi iliyohusishwa kwenye tukio la kutwaliwa kwa mafuta hayo na kuwa meli zenyewe hakikushikiliwa. Badala yake, afisa amesema, Marekani ilitishia wamiliki wa meli na manahodha kwa vikwazo kuwalazimisha kuwakabidhi mafuta hayo.
Bado haijafahamika ikiwa meli hizo — Bella, Bering, Pandi na Luna — ziko wapi kwa sasa.
Balozi wa Iran nchini Venezuela Hojat Soltani anaelezea taarifa za kukamatwa kwa mafuta ya Iran kama propaganda za uongo.
"Huu ni uongo mwingine na kitendo cha mapigano ya kisaikolojia kunakotekelezwa na propaganda za Marekani ," aliandika kwenye Twitter.
Wasiwasi kati ya Iran na Marekani umekuwa ukiongezeka tangu Marekani ilipotekeleza uamuzi wa upande mmoja mwaka 2018 wa kujiondoa katika makubaliano ya kihistoria ya mpango wa nyuklia.
Marekani imeiwekea vikwazo vikali Iran na Venezuela kuzuia uuzaji wa mafuta nje ya nchi hizo. Inataka kushinikizo rais wa Venezeulan Nicolas Maduro kuondoka madarakani na kubadilisha tabia ya uongozi nchini Iran.
Ijumma, msemaji wa Wizara ya Sheria Marekani amesema:"Iwapo Marekani itafanikiwa kufikisha mafuta ya Iran yaliyokamatwa katika mahamaka ya Marekani, hatua hiyo inaweza kusaidia kuunga mkono mfuko wa waathirika wa ugaidi nchini Marekani kujumuisha wale waliofadhili badala tu wale wanaothibitishwa kuhusika na ugaidi moja kwa moja."
Pia unaweza kutazama:














