Mwanamfalme wa Saudi ashutumiwa kwa kutuma mamluki Canada

Iliyochapishwa

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman ameshutumiwa kwa kutuma mamluki nchini Canada ili kumuua aliyekuwa afisa wa ujasusi wa Saudi.

Mpango huo wa kumuua Saad al-Jabri ambao haukufanikiwa ulifuata muda mfupi baada ya mauaji ya mwanahabari aliyeuawa nchini Uturuki, Jamal Khashoggi, nyaraka zilizowasilishwa katika mahakama ya Marekani zimedai.

Bwana Jabri, afisa mstaafu wa serikali ya Saudi Arabia, alikimbilia ughaibuni miaka mitatu iliyopita.

Tangu wakati huo amekuwa akipewa ulinzi binafsi mjini Toronto.

Mpango huo wa mauaji inasemekana kuwa ulifeli baada ya maafisa wa mpaka wa Canada kuanza kushuku kikosi hicho walipokuwa wanajaribu kuingia nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Toronto Pearson, nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinaonesha.

Kwa miaka mingi, Bwana Jabri, 61, alikuwa kiungo muhimu katika huduma ya ujasusi ya siri Uingereza na mashirika mengine ya kijasusi ya nchi za Magharibi nchini Saudi Arabia.

Mashtaka yanasema nini?

Malalamiko ya kurasa 106 ambayo bado hayajaidhinishwa, yalifunguliwa Washington DC, yakimshutumu mwanamfalme kwa kujaribu kumuua Bwana Jabri ili kumyamazisha.

Bwana Jabri anasema hilo ni kwasababu yeye anajua taarifa nyeti. Nyaraka inasema hayo ni pamoja na ufisadi na usimamizi wa kikundi cha mamluki nje ya nchi kilichopewa jina la kikosi cha Tiger.

Wanachama wa kikosi cha mamluki cha Tiger walihusika na mauaji ya mwanahabari Khashoggi, aliyeuliwa ndani ya ubalozi wa Saudi, mjini Istanbul 2018, nyaraka iliyowasilishwa mahakamani inasema.

"Sehemu ya madai ni nyeti, ikiwa ni pamoja na tarifa za udhalilishaji na nyingine zenye ushahidi kuhusu mshtakiwa bin Salman na kumbukumbu ya Dkt. Saad inavyoangazia nukuu alizosema akibashiri kuuawa kwakwe," nyaraka hiyo inasema.

"Hiyo ndio sababu mshitakiwa bin Salman anataka auawe, na pia ndio sababu bin Salman amekuwa akifanyia kazi lengo hilo kuhakikisha linafanikiwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita."

Baada ya kutoroka Saudi Arabia 2017, Bwana Jabri alikimbilia Canada kupitia Uturuki.

Anadai kwamba Bwana Mohammed bin Salman alifanya majaribio kadhaa ya kumrejesha Saudi Arabia, kiasi cha hata kutuma ujumbe wa kibinafsi, ikiwemo ule uliosema: "Bila shaka hatimae tutakukamata tu".

Wakati huo, chini ya wiki mbili baada ya kifo cha Khashoggi, Bwana Jabri anasema kikundi cha mamluki cha Tiger kilisafiri hadi Canada nia ikiwa ni kumuua.

Nyaraka za Mahakama zinasema kundi hilo - linalojumuisha mwanaume mmoja kutoka idara aliyokuwa - walikuwa wamebeba mabegi mawili yenye nyaraka zinazohusishwa na mahakama.

Hata hivyo, maafisa wa mpaka wa Canada "waliwashuku kwa haraka" na wakakatazwa ruhusa ya kuingia baada ya kufanyiwa mahojiano, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama.

"Kama haitoshi Bin Salman alipeleka kundi hilo Amerika Kaskazini kumuua Dkt. Saad," madai hayo yanasema.

Bwana Jabri anamshutumu mwanamfalme huyo kwa kufanya jaribio la kutekeleza mauaji ya kiholela kwa kukiuka sheria za ulinzi wa waathirika wa mateso Marekani na pia uvunjaji sheria ya kimataifa.

Aidha, serikali ya Saudia haikujibu ombi la kuzungumza na BBC.

Waziri wa usalama wa umma nchini Canada Bill Blair amesema hawezi kuzungumzia kesi hiyo lakini serikali yake inafahamu kuhusu tukio ambapo raia wa nchi za kigeni wamejaribu kufuatilia au kutoa vitisho kwa raia wa Canada na wale wanaoishi Canada."

"Ni jambo lisilokubalika kabisa na hatutavumilia vitendo vya raia wa kigeni kutishia usalama wa raia wa Canada au usalama wa raia wetu na wakaazi wake. Raia wa Canada wawe na uhakika kwamba mashirika yetu ya usalama yana ujuzi na raslimali stahiki, kubaini, kuchunguza na kujibu vitisho vya aina hiyo," amesema.

"Tutachukua hatua stahiki kuhakikisha raia wa Canada na wanaoishi nchini kuwa wako salama na pia tunatoa wito kwa watu kuripoti vitisho vyovyote vya aina hiyo kwa mamlaka ya sheria."

Mei, BBC iliripoti kwamba watoto wa Jabri wameshikwa mateka, kulingana na kijana wake mkubwa, Khalid.