Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa mto Nile: Misri yakasirika huku Ethiopia ikisherehekea
Wakati Ethiopia inasherehekea mvua iliyonyesha na kuanza kujaza bwawa lake lililoleta utata kuhusu mto Nile, Misri ilikuwa imekasirika.
Kwa kipindi kirefu Misri imekuwa ikipinga mradi wake wa kujenga bwawa kubwa juu ya mto Nile ambalo kunaweza kupunguza kiwango cha maji iinayopokea kutoka mto huo na imetaja mradi wa Ethiopia kama tishio.
Bwawa kubwa la Ethiopia limekuwa likijengwa tangu 2011, na kwa sasa hivi limeanza kujaa maji na litakuwa na bilioni 4.9 za mita za ujazo za maji ya mto Nile baada msimu huu wa mvua.
Hili ni licha ya kuwa Misri imesisitiza kwamba bwana hilo halitajazwa maji bila ya makubaliano ya kisheria kuhusu vile mchakato huo utakavyosimamiwa.
Katika kipindi cha miaka minne hadi sita, bwawa hilo ambalo litakuwa ndio chanzo kikubwa zaidi Afrika cha uzalishaji umeme linatarajiwa kufika mita 74 za ujazo wa maji.
Picha za satelaiti kuanzia mapema Julai zinaonesha bwawa la Ethiopia likijazwa maji:
Misri na Ethiopia, pamoja na Sudan ambayo pia inapokea maji kutoka mto Nile, kwa kipindi kirefu zimekuwa katika majadiliano huku bwawa hilo likiendelea kujengwa.
Nchi hizo zilisaini azimio mwaka 2015 lililozungumzia umuhimu wa kushirikiana lakini Misri inahisi kwamba hilo halijatekelezwa.
Mwaka uliopita, ilitumia muda wake miwngi na hata kutafuta ushawishi kisiasa katika ngazi ya kimataifa, kutafuta usaidizi kutoka kwa Marekani na Umoja wa Ulaya lakini ikaambulia patupu.
Inaonekana kana kwamba Misri imeshindwa nguvu katika mvutano huo.
Imeshindwa kulazimisha Ethiopia kutekeleza kile ilichokiona kama makubaliano ya kimataifa yanayohitaji nchi zilizo upande wa juu wa mto kushauriana na nchi zilizo upande wa chini wa mto kabla ya kufanya maamuzi ya kutekeleza miradi mikubwa ya namna hii.
Hadi kufikia sasa, ni vigumu kutabiri Misri itafanya nini zaidi ya kukubali na kuzuia athari zozote zinazoweza kutokea.
Uongozi wa Misri umesema mara kadhaa kwamba bado unashikilia kutafuta suluhisho kupitia majadiliano.
Serikali hiyo imerejelea mara kadhaa kuelezea mradi wa bwawa la Gerd kama hatua ya kufa na kupona.
Hii itakuwa kweli hasa ikiwa kiwango cha maji kitakachofika Misri kitapungua sana kwasababu ya ujenzi wa bwawa hilo.
Lakini baada ya kuanza kujazwa kwa bwawa la Ethiopia, sasa serikali ya Misri imejitahidi kusimama kidete.
Taarifa rasmi zasema kwamba Misri bado imejitolea kuendeleza mchakato wa sasa wa kidplomasia ambao unaendelezwa na Umoja wa Afrika, na kurejelea msemo wake kwamba haitakubali uamuzi wa upande moja wa Ethiopia.
Ukosefu wa maji
Imesititiza kwamba makubaliano yoyote ya siku za usoni ni lazima yaidhinishe kile inachokiona kama haki za matumizi ya mto Nile hadi mita 55 za ujazo wa maji kutoka mto huo.
Kwa wastani mita za ujazo 49 za maji hutiririka kupitia kijito cha mto Nile kwa mwaka na Ethiopia imekuwa ikikataa kuweka wazi kwa Misri ni kiwango gani cha maji ambacho kitatiririka kwa bwawa hilo. Inachukulia dai la Misri kama matakwa ya makubaliano yaliyofanywa bila nchi hiyo kuhusishwa.
Hatari haijawahi kuwa juu kwa Misri kama ilivyo sasa.
Inaelezea bwawa la Gerd kama tishio lililopo wala sio kuongezea chumvi.
Misri ni nchi iliyo jangwani na inachukuliwa kama yenye uwezo wa chini wa kupata maji.
Benki ya Dunia inatambua nchi kuwa na uhaba wa maji iwapo uwezo wa sehemu kupata maji ya mvua ni chini ya mita za ujazo 1,000 ya maji safi kwa mtu kwa mwaka.
Kilimo
Misri, kiwango hicho ni mita 550 za ujazo kwa mtu kila mwaka kulingana na serikali.
Mto Nile ndio chanzo cha msingi cha maji kwa raia wa Misri, maji ya kunywa na kilimo.
Mgao wake kwa mwaka kutoka mto Nile ni mita za ujazo 55 ambazo sasa hivi zipo hatarini - kiwango ambacho tayari ni cha chini sana ikilinganishwa na kile kinachohitaji kwa matumizi ya msingi.
Kwa Misri, Ethiopia imetumia majadiliano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda mrefu kufumba macho Misri huku wakijitengenezea mazingira ya kudhibiti kabisa mto huo.
Ujumbe wa Twitter wa kusherehekea mwaka wa kwanza wa kujaza bwana Gerd na Waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia, Gedu Andargachew, ambao sehemu ulikuwa unasema…Mto Nile ni wetu" - ulisababisha ghadhabu.
Umethibitisha kile ambacho Misri imekuwa ikihofia kwa muda mrefu na baadhi wakajibu kwa kutoa kila aina ya hofu yao.
"Raia wa Ethiopia wamekataa kuamini kwamba bila mto Nile ni sawa na kusema tutakufa. Wana mito mingi na wanapokea karibu mita za ujazo 950 za maji ya mvua kila mwaka. Sisi tunapokea mita za ujazo 55 pekee, nusu ya kiwango tunachohitaji ambacho pia ni nusu ya kiwango wanachotumia mifugo wao kwa mwaka," amesema raia mmoja wa Misri, Imad-al-Din Husayn katika gazeti la Shorouq.
Mzozo wa kidplomaisa
Kwa upande wake Misri imeanzisha miradi kadhaa ya maji ambayo ni pamoja na kuchakata tena maji chafu ya kilimo, viwanda vya kuondoa chumvi kwenye maji na hata kuonesha azma ya kutaka kubadilisha mifumo ya zamani ya kilimo cha unyunyiziaji maji hadi kilimo cha njia ya kumwagilia matone ya maji.
Lakini sasa kilichopo ni ikiwa Misri itatumia upungufu wa maji nchini humo katika ngazi ya kidplomasia na kuweza kupata uungwaji mkono kimataifa.
Katika jangwa la Sahara na hata Marekani, Ethiopia imeonekana kutumia nafasi yake vizuri.
Mweyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika ni rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Raia wengi wa Misri wanaamini kwamba Afrika Kusini inapendelea Ethiopia.
Ikiwa kutakosekana maafikiano, Misri inaamini kwamba inaweza kurejesha malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta suluhu.
Lakini haina uhakika kabisa ikiwa utaungwa mkono na wanachama wote watano wa kudumu wa baraza hilo.
Taarifa za hivi karibuni zinasema kwamba China na Urusi zitapinga hatua hiyo kwasababu hazitaki kuwe na kitu ambacho siku za baadae kinaweza kutumiwa kama mfano kwa kuwa nchi hizo zenyewe zina mizozo yao ya umiliki wa mito na majirani zao waliopo chini ya mito.
Pia kushindwa kutatua mzozo uliopo kati ya Ethiopia na Misri huenda kukasababisha matatizo zaidi.
Mzozo wa Misri unatokana na ukame na iwapo watu watalazimika kuhama makazi yao huenda kukawa na athari kubwa zaidi kwa eneo zima la Kaskazini mwa Afrika na Ulaya.
Na makundi yenye silaha yaliyopo katika nchi hizo mbili huenda yakawa tishio sio tu kwa Afrika lakini dunia nzima kwa ujumla.