Marekani kuondoa wanajeshi 12,000 Ujerumani kama hatua ya kimkakati

Iliyochapishwa

Marekani itaondoa wanajeshi wake karibia 12,000 waliopo Ujerumani katika kile kinachoelezwa kama hatua ya kimkakati ya kupanga tena wanajeshi wake Ulaya.

Takriban wanajeshi 6,400 watarejeshwa nyumbani huku wengine wakipelekwa katika nchi zingine ambazo ni washirika wa Nato kama vile Italia na Ubelgiji.

Rais Donald Trump alisema hatua hiyo imetokana na Ujerumani kushindwa kufikia malengo ya Nato upande wa pesa za matumizi kwa ajili ya ulinzi.

Lakini hilo limepingwa vikali bungeni hasa wale wanaoamini kuwa hatua hiyo itaimarisha Urusi.

Maafisa waandamizi wa Ujerumani pia nao wameonesha wasiwasi wao.

"Hatutaki kuendelea kudanganywa," Bwana Trump amewaambia wanahabari katika Ikulu ya Marekani Jumatano muda mfupi baada ya tangazo hilo. "Tunapunguza wanajeshi kwasababu hawalipii gharama zao."

Kwa kipindi kirefu, Bwana Trump amekuwa akilalamika kwamba washirika wa Nato wa Ulaya wanastahili kuongeza kiwango chao cha matumizi kwa ajili ya ulinzi wao wenyewe. Aliongeza kuwa washirika wa Nato hawastahili kutegemea Marekani kuchukua mzigo mkubwa zaidi wa gharama za kuendeleza muungano huo.

Majadiliano kati ya washirika wa muungano huo yanazingatia kile walichokubaliana kwamba pesa za matumizi kwa ajili ya ulinzi angalau zifike asilimia 2 ya mapato jumla ya taifa yaani GDP kufikia 2024.

Ujerumani pamoja na nchi zingine nyingi bado hazijafikia malengo hayo.

Waziri wa Ulinzi Mark Esper wakati anatangaza uamuzi huo, alisema kwamba hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuhamisha wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo.

Alisema "ni mkakati muhimu na uhamisho utakao kuwa na munafaa na ambao bila shaka yoyote utasaidia katika kufikia kanuni za msingi za kuimarisha Marekani".

Hatua hiyo imepangiwa kugharimu serikali ya Marekani dola bilioni kadhaa na pia itapunguza uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani kwa zaidi ya asilimia 25.

"Ndege za kivita zitahamishwa hadi Italia huku baadhi ya wanajeshi huenda wakahamishwa Poland," Bwana Esper amesema.

Hata hivyo umauzi huo umekosolewa na maafisa wa Ujerumani, huku mwenyekiti wa kamati ya masuala ya mambo ya nje akisema kuwa hilo huenda likadhoofisha muungano wa Nato.

Na mkuu wa jimbo la Bavaria, Ujerumani, Markus Soeder, alisema anasikitishwa na uamuzi huo. "Hatua hiyo inakuwa mzigo kwa uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani," amewaambia wanahabari.

Pia kulikuwa na ukosoaji wa pande mbili Marekani. "Hili ni jeraha la kujitakia... dhidi ya maslahi ya raia wa Marekani," amesema seneta wa Democratic Jack Reed.

Seneta wa Republican Mitt Romney alielezea uamuzi wa kuondoa majeshi kutoka Ujerumani kama "makosa makubwa na fedheha kwa rafiki na mshirika".Mpango huo ulitangazwa mara ya kwanza na Bwana Trump mwezi uliopita, alipoishutumu Ujerumani kwa kukosa kuwajibika upande wa malipo yake kwa Nato.

Pia aliishutumu nchi hiyo kwa kuchukua hatua zinazoathiri Marekani kibiashara.

Aidha, alidai uwepo wa majeshi Ujerumani unawafaidi kwasababu wanajeshi hao hufanya manunuzi nchini humo.

Vikosi vya jeshi vya Marekani nchini Ujerumani ni urithi wa tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia Ujerumani iliposhindwa.

Ujerumani sasa hivi ndio mwenyeji wa idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani waliopo Ulaya, ikifuatiwa na Italia, Uingereza kisha Uhispania.

Baadhi ya maafisa wa Marekani wanaoishi Ulaya pia wanasaidia katika oparesheni za nchi ambazo sio wanachana na idadi ya wanajeshi wa Marekani inabadilika huku wakihamishwa ndani na nje ya Ulaya.