Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Kenya yarekodi idadi kubwa ya wagonjwa waliofariki na maradhi hayo kwa siku
Idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa corona Kenya inakaribia 300 kulingana na takwimu zilizotolewa na serikali Jumanne.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kwamba watu wengine 14 wamefariki kutokana na virusi hivyo katika kipindi cha saa 24 na hivyobasi kufanya idadi ya waliofariki kufikia sasa kuwa 299.
Aidha idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na maradhi hayo imefikia 18,581 baada ya waziri wa Afya kutangaza wagonjwa wengine 606.
Kati ya wagonjwa hao wapya 583 ni raia wa Kenya huku 23 wakiwa raia wa kigeni , wanaume wakiwa 409 nao wanawake wakiwa 197.
Mgonjwa mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa miezi minne huku mtu mwenye umri mkubwa zaidi akiwa mzee wa miaka 85.
Hatahivyo habari njema ni kwamba wagonjwa 75 wa corona wamepona maradhi hayo , na hivyobasi kufanya jumla ya waliopona nchini Kenya kufikia 7,908.
Wagonjwa hao wanatoka katika maeneo tofauti.
Idadi ya wagonjwa kulingana na kaunti
Nairobi imeandikisha wagonjwa 448, Kajiado 25, Machakos 16, Uasin Gishu 11, Nakuru 11, Kericho 9, Busia 7, Mombasa 7, Garissa 6, Bomet 3, Nyeri 2, Narok 2, Nandi 2, Embu, Lamu, Murang'a zikiwa na wagonjwa mmoja mmoja.
Mjini Nairobi eneo la Embakasi limetajwa kuwa na wagonjwa wengi na waziri huyo amewataka wakaazi kuchukua tahadhari.
Kagwe amewataka wale wanaofanya kazi kutoka nyumbani kujaribu kufanya kazi katika nyumba zao.
''Nimekuwa risasi, umekuwa risasi . Tunaweza kumuua mtu, Tumekuwa hatari'', alisema.
Amewataka wazazi kuwasisitizia watoto wao kuosha mikono , kupaka sanitizer na kuwajibika.
Kagwe aliitikia wito wa rais Uhuru Kenyatta kwa kusema hakuna mtu atakayehurumiwa licha ya wadhfa wake inapokuja katika kuhakikisha kuwa masharti ya corona yanatekelezwa.
Amewataka Wakenya kutoruhusu wageni majumbani mwao ama hata kuzuru mashambani hadi iwapo kuna dharura.
Maafisa wanne wa Afya ni miongoni mwa wale waliofariki kutokana na virusi hivyo nchini.
Muungano wa wauguzi nchini kenya NNAK siku ya Jumanne ulionyesha wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ugonjwa wa Covid-19 miongoni mwa wafanyakazi wa afya kote nchini.
Rais wa NNAK Alfred Obengo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alfichua kwamba kufikia Julai 28 zaidi ya maafisa 500 wa Afya waliambukizwa virusi hivyo.
''Huku mambo haya ya kusikitisha yakitokea tayari tumepoteza wafanyakazi wanane wa afya kote nchini watano kutoka Nairobi na mmoja mmoja kutoka Wajir, Kajiado na Mombasa'', alisema.
Obengo amezitaka serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhakikisha kwamba maafisa wote wa afya wanavalia vifaa vya kujilinda na maambukizi kwa jina PPE.