Virusi vya corona: Watu 960 wapatikana na Covid-19 kwa siku, 4 wakiwa na historia ya kusafiri nchi jirani

Iliyochapishwa

Wizara ya afya nchini Kenya imetangaza leo Jumapili kuwa imerekodi watu 960 waliopatwa na maambukizi ya Covid-19.

Idadi hiyo imepatikana baada ya wizara hiyo kupima sampuli za watu 8,261 kutoka maeneo mbali mbali ya nchi katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Idadi hiyo inaifanya idadi ya jumla ya watu waliopatwa na virusi vya corona nchini Kenya kufikia 17,603 - huku idadi ya visa vinarekodiwa vikionekana kupanda kila siku.

Wizara hiyo kupitia Waziri wa afya imesema kwamba zaidi ya wagonjwa 169 wameruhusiwa kuondoka hospitalini, 83 kutoka hospitali na 86 kutoka katika mipango ya huduma za matibabu ya nyumbani , na hivyo kuongeza idadi ya watu waliopona virusi vya corona hadi 7,743.

Pia ilitangaza kwamba wagonjwa wengine wawili wamefariki dunia na hivyo kuifanya idadi ya jumla ya vifo vilivyosababishwa na Covid-19 kufikia 280.

Kati ya wagonjwa 960 , 604 ni wanaume huku 356 wakiwa ni wanawake. Aliyekuwa na umri mdogo zaidi miongoni mwao alikua na mwaka mmoja, huku mwenye umri mkubwa zaidi akiwa na umri wa miaka 88.

Wanne kati ya wagonjwa wapya walikua na historia ya kusafiri, wawili wakiwa ni kutoka Tanzania, mmoja kutoka Rwanda na mwingine kutoka Uganda.

Wakenya walikuwa ni 952 , Muingereza mmoja, wasomali wawili huku wengine wanne wakiwa ni Mtanzania, Muethiopia na Mchina.

Hatua zilizochukuliwa na Kenya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona:

1.Wizara ya Afya na huduma za umma imeanzisha hazina ya kuwasaidia wafanyakazi wa Afya wanaokabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.

2. Wizara ya elimu itachukua hatua kuwalinda wanafunzi kutokana na athari mbaya za hatua zilizochukuliwa kukabiliana na Covid-19

3. Mamlaka ya usambazaji wa tiba nchini Kenya imeondoa masharti ya ununuzi wa vifaa vya kujilinda dhidi ya Covid-19 kwa takriban miezi mitatu ili kurahisishia kaunti kununua vifaa hivyo.

4. Nyumba za watu wasiojiweza jijini Nairobi zitafaidi kutokana na fedha zilizotengwa na serikali kusaidia familia zisizojiweza

5.Bunge litapitisha tena mapendekezo na miswada kuhusu vichocheo vya uchumi.

6. Ili kuhakikisha msaada unagawanywa kwa njia salama, mfuko wa hali ya dharura wa kukabiliana na Covid-19, Kenya na mashirika mengine ya usalama yatashirikiana kuratibu miradi kama ule wa Adopt a Needy Family, ambapo raia wa Kenya wanasaidiana kipindi hiki cha janga kuhakikisha hatua zinachukuliwa bila kufuata urasimu