Virusi vya corona: Kenya yatoa muongozo mpya wa usafiri kudhibiti maambukizi

Chanzo cha picha, KQ
Hakutakuwa na haja ya kujitenga kwa lazima kwa wasifiri na watalii wanaowasili nchini Kenya ikiwa hawaoneshi dalili za ugonjwa wa Covid-19, kulingana na tangazo la serikali.
"Abiria wote hawatalazimika kuwekwa kwenye karantini wanapowasili kutoka maeneo waliotoka ikiwa kiwango cha joto la mwili sio zaidi ya nyuzijoto 37.5 na kama hawana kikohozi cha kuendelea, hawana matatizo ya kupumua na wala kuonesha dalili zingine za mafua. Hili ni muhimu kwasababu hatutarajii mtalii kuja katoka maeneo aliotoa kisha awekwe karantini kwa siku 14."
Ili kuimarisha hatua za usalama za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, Waziri wa uchukuzi James Macharia amesema viwanja vya ndege kote nchini vitaruhusiwa tu wafanyakazi na wasafiri pekee isipokuwa kama msafiri anahitaji huduma maalum.
"Kanuni mpya pia zinajumuisha hatua za kupunguza kutangamana kati ya wahudumu wa ndege na abiria, maafisa wa usalama na abiria na wafanyakazi wa viwanga vya ndege na mizigo ya abiria katika uwanja wa ndege.''
Bwana Macharia amesema kwamba lengo la hatua zilizochukuliwa ni kuhamasisha watalii ili kuimarisha sekta hiyo ambayo imeporomoka vibaya kipindi hiki cha virusi vya corona.
Waziri wa uchukuzi pia ametangaza kwamba huduma ya treni ya mwendo kasi 'Madaraka Express' itaanza tena shughuli za uchukuzi Jumatatu kwa safari za miji ya Nairobi na Mombasa mara moja kwa siku.

"Huduma ya treni itakuwa na mabehewa 10 kwa abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 600 kwa usafiri wa mara moja ( sawa na asilimia 50 ya idadi jumla ambayo wangebebwa kwa hali ya kawaida) na behewa moja litatengwa kwa watu wanaoshukiwa kupata maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19," Waziri amessema.
Waziri Macharia amesema kuwa katika kisa cha kwamba mtu atakuwa anashukiwa kuwa na virusi vya corona, wahudumu wa ndege watakuwa karantini nyumbani huku wale waliokuwa kwenye mistari miwili ya abiria anayeshukiwa kuwa na dalili za virusi vya ocorona watapimwa.
"Pale kutakapokuwa na mtu anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19 kwenye ndege, wahudumu wa ndege watakuwa karantini nyumbani. Ikibainika kwamba hawajapata mambukizi ya virusi wataruhusiwa kurejelea shughuli zao za kawaida. Na pale ambapo wahudumu watalazimika kusimama kwa muda wakati wa safari, wahudumu wa ndege hawataruhusiwa kuondoka katika vyumba vyao vya kulala isipokuwa tu kwa hali ya dharura," Waziri amesema.
Waziri wa uchukuzi James Macharia amerudia agizo la rais Uhuru Kenyatta kwamba usafiri wa anga utaanza tena Julai 15, 2020, na kuongeza kwamba hadi kufikia sasa ni ndege 5 pekee ambazo zimetimiza masharti yaliyowekwa.












