Virusi vya corona: Walioathirika na marufuku ya usafiri Kenya sasa wapata mwanga

Wakenya

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC News Swahili
  • Iliyochapishwa

Imekuwa ni miezi karibia mitatu tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoweka marufuku ya usafiri mnamo Aprili, katika miji ya Nairobi, Mombasa na Mandera kabla ya sikukuu ya pasaka.

Baadhi ya watu walipatwa ghafla na murufuku hiyo ambayo iliathiri pakubwa shughuli zao za kila siku hasa ukizingatia kwamba ni jambo ambalo halikuwa linatarajiwa.

Faswila Athuman Omar ni mkaazi wa Nairobi ambaye anaendesha shughuli zake zote za kimaisha mjini humo lakini wakati marufuku inatangazwa alikuwa Mombasa.

Wakati huo alidhani pengeni litakuwa jambo rahisi asijue kilichokuwa kinamsubiri.

'Sina njia ya kupata shilingi'

Faswila anasema janga la virusi vya corona limemuathiri pakubwa kwasababu nyumba yake Nairobi ameifunga kuanzia mwezi wa tatu kikubwa zaidi ni kwamba hajaweza kulipa kodi ya nyumba kwa miezi yote hiyo ambayo amekuwa Mombasa.

''Tatizo ni kwamba kwa sasa hivi sina pa kuweza kupata kodi ya nyumba kwasababu biashara zangu zimesimama kwa kipindi chote hicho''.

Kingine pia alichokipitia ni kuwa ingawa yupo Mombasa kwenye jamaa wake wengi, ameshindwa kumtembelea hata mmoja kwa hofu ya ugonjwa wa corona.

Faswila Athuman Omar

Chanzo cha picha, Faswila Athuman Omar

Maelezo ya picha, Faswila Athuman Omar mkaazi wa Nairobi aliyekwama Mombasa baada ya kuwekwa kwa marufuku ya usafiri

'Sikuwa na makaazi'

Dennis Gicheru ni mkaazi wa Eldoret ambaye alifungiwa nje ya makazi yake tangu kutangazwa kwa marufuku ya usafiri.

Kinachomletea ujira ni kazi ya kuandaa shughuli kama harusi na matukio mengine. Gicheru alikuwa amekwenda Nairobi kutafuta stakabadhi za kumuwezesha kuendesha biashara yake.

Kwasababu ni safari ambayo hakuitarajia kumaliza siku nyingi na baadhi ya changamoto alizokumbana nazo ni kupata makaazi na alicholazimika kufanya ni kuomba usaidizi kwa rafiki zake angalau apate mahali pa kujisitiri.

''Sikuwa na makazi maalum kwahiyo ilibidi niweze kuomba marafiki hapa na pale waweze kunisaidia siku mbili tatu angalau nipate mahala pa kulala tu siku iweze kupita.''

Aidha Gicheru analalamika kwasababu biashara yake anayofanya eneo la Eldoret imekwama na imekuwa vigumu sana kwake kupata mkate wake wa kila siku.

Imekuwa ni karibia miezi mitatu tangu Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipoweka kanuni za kuzingitiwa kama njia moja ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Watu wamepokeaje tangazo la Rais?

Baada ya hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta ambayo iligusia kulegezwa kwa marufuku kadha wa kadha zilizolenga kudhibiti usambazaji wa virusi vya Corona, raia pamoja na washikadau wa sekta zilizoathirika zaidi wanazungumziaje hatua ya rais Kenyatta.

Kwa Faswila mkaazi wa Nairobi ambaye alilazimka kusalia Mombasa tangu kuanza kutekelezwa kwa kanuni hii, anasema amepokea ujumbe wa Uhuru Kenyatta kufungua mipaka kwa tabasamu kwasababu anaamini kwamba huu ndio mwanzo mpya kwake.

Baada ya tangazo rasmi, Faswila anapanga kurejea Nairobi haraka iwezekanavyo kuanza tena shughuli zake.

Pia rais amefungua sehemu za kufanya ibada kwa umma kwa msharti kwamba miongozo iliyowekwa itafuatwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na ile ya mtu binafsi kama ilivyobainishwa na Baraza linalojumuisha dini tofauti tofauti.

Msahafu

Chanzo cha picha, Reuters

Aidha mafunzo kwa watoto yanayotolewa kanisani pamoja na shule za dini ya Kiislamu kwa watoto maarufu kama madrasa bado kumepigwa marufuku.

Sheikh Juma Ngao mwenyekiti wa kitaifa wa baraza kuu la ushauri kenya, anasema amepokea kwa furaha taarifa za kufunguliwa kwa maeneo ya ibada kwa masharti.

Sheikh Juma Ngao ameongeza kuwa wao walishaanza kutoa mafunzo kwa maimamu wao na bado zoezi hilo linaendelea kuhusu masharti yaliyowekwa na kufahamisha viongozi wa kidini athari za corona.

''Masharti yaliyowekwa tutahakikisha yanazingatiwa ili misikitini kusiwe ni mahali pa watu kuambukizana maradhi wao kwa wao.''

Sheikh Ngao amesema kwamba Waislamu watahitajika kuswali na barakoa, wazingatie kutokaribiana na ikiwezekana kila mmoja abebe mswala wake mwenyewe kutoka nyumbani.

Sehemu za haja kubwa pia ikiwezekana zitafungwa lakini zile za kutawadhia zitawachwa wazi na kuwepo kwa utaratibu wa kupiga dawa mara kwa mara msikitini punde tu baada ya waumini kufanya ibada na kutoka sehemu hiyo.

Mchungaji Anthony Musembi kutoka maeneo ya Nakuru kiongozi wa kanisa anasema amefurahia tangazo la rais kwasababu haijakuwa rahisi kukaa kwa miezi yote hiyo bila kukusanyika kama kanisa ilivyo desturi yao.

Mchungaji Anthony Musembi

Chanzo cha picha, Mchungaji Anthony Musembi

Maelezo ya picha, Mchungaji Anthony Musembi amezungumzia changamoto zilizopo baada ya rais kutangaza kufungua maeneo ya kuabudu

Lakini kwa mtazamo wake, anaona masharti yaliyotolewa kidogo yana utata kwa kuwa mengine yanazua kizungumkuti mfano lile la watu watakaoruhusiwa sehemu ya ibada kutozidi mia moja au lile la kwamba watu wanaozidi miaka 58 wasijumuike katika sehemu za ibada kwasababu viongozi wengi wa kidini ama Wasilamu au Wakikiristo ni wazee.

Kwa mtazamo wake ni kuwa kundi hili la watu kwa jinsi masharti yalivyo ni kwamba halitaweza kuabudu.

''Ingekuwa ni kheri kama kundi hili lingeambiwa lisitangamane na watu wengine,'' Amesema mchungaji Anthony Musembi.

Mchungaji huyo anaamini kwamba janga hili lipo lakini anasema hilo halimaanishi kuwa hawawezi kuendelea na ibada.

''Tukimuomba Mwenyezi Mungu atatuwezesha na tutaweza kushinda. Hakuna maradhi ambayo yana mshinda Mwenyezi Mungu.'

Pia amesema changamoto nyengine itakuwa ni kufanya ibada bila kuimba au kufanyika chini ya saa moja na kusisitiza kuwa hilo litawabana sana katika kufanya ibada zao na kuomba kupewa uhuru zaidi wa kuabudu.

Lakini wakati masharti yanalegezwa kumekuwa na hofu ya kuongozeka kwa maambukizi wiki zijazo labda kutokee miujiza.

Maoni ya wataalamu

Wanasayansi nchini Kenya wanakadiria kwamba huenda Wakenya milioni 2.6 tayari wana virusi vya corona, hayo yamejitokeza baada ya wanasayansi kupima damu iliyotolewa kwa ajili ya protini inayotumika kwenye mfumo wa kinga.

Kwa mujibu wa data ya utafiti wa Taasisi ya Matibabu Kenya pamoja na Tasisi ya Afya ya Wellcome Trust, takriban watu 550,000 sawa na asilimia 12. 4 ya wakazi wa Nairobi kati ya raia milioni 4.4 tayari walikuwa wamejenga kinga ya mwili kabla ya kutangazwa kwa mgonjwa wa kwanza wa Covid-19 nchini humo Machi 13.

Katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini Kenya (KMPDU) daktari Chibanzi Mwachonda anaonya kuwa hali ya huduma hospitalini ni tete.

''Kumekuwa na ongezeko la maambukizi katika mwezi wa Juni na Julai lakini pia kumekuwa na shinikizo kutoka wa wananchi la kufunguliwa tena kwa shughuli za kiuchumi.''

Kulingana na daktari Mwachonda huenda kipindi hiki ambapo masharti yamelegezwa kikawa muhimu katika kujua kama kweli Kenya iko tayari kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona kikamilifu.

Wahudumu wa afya waambukizwa virusi

Pia kumekuwa na ongezeko la wahudumu wa afya na madaktari kupata maabukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

''Kuna hofu ya kuwa hospitali za wagonjwa Kenya tayari zimejaa lakini tatizo sio corona kwasababu uhaba wa vyumba vya wagonjwa mahututi umekuwepo hata kabla ya corona na sasa hivi hali imekuwa mbaya.''

Kufunguliwa kwa kaunti za Mombasa na Nairobi hakumaanishi kwamba virusi vya corona vimeisha lakini ukweli ni kwamba ugonjwa huo upo katikati ya wananchi na changamoto sasa imerejea kwa raia, je atatimiza masharti yaliyowekwa kupunguza maambukizi?