Virusi vya Corona: Je virusi vya corona vinasambaa kwa kasi ya kiwango gani afrika?

    • Author, Na Peter Mwai na Christopher Giles
    • Nafasi, BBC Reality Check
  • Iliyochapishwa

Afrika kwa sasa inashuhudia ongezeko la haraka la wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona, na vifo pia vinaongezeka, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Tumetathmini hali ilivyo barani na kuangalia ni mataifa gani ambapo hali inazua wasiwasi zaidi.

Corona inaenea kwa kasi kiasi gani?

WHO ilisema mapema mwezi Juni kwamba ugonjwa huu ulikuwa unaongeza kasi ya kusambaa Afrika, ingawa kwa kuangalia idadi halisi, bara hili bado linachangia idadi ndogo sana ya wagonjwa wote wa corona duniani.

Lakini idadi inaongezeka. Ingawa ilichukua siku 100 kwa Afrika kufikisha visa 100,000 vya maambukizi, ilichukua siku 18 pekee kwa idadi hiyo kuongezeka mara dufu na kuwa 200,000. Idadi hiyo iliongezeka tena mara dufu na kufikia wagonjwa 400,000 katika siku 20 na sasa idadi inakaribia nusu milioni.

Ongezeko la visa vya maambukizi Afrika sasa linaanza kuonekana kama ilivyotokea katika maeneo mengine duniani yaliyoathiriwa pakubwa na virusi vya corona.

Na mataifa mengi Afrika sasa yanashuhudia kusambaa kwa virusi hivi kwenye jamii, kwa mujibu wa WHO.

Hii hutokea wakati ambapo mtu anaambukizwa Covid-19 bila kutangamana na mtu aliyefahamika kuwa na virusi vya corona iwe ni kutoka nje ya nchi au ndani ya nchi. Hali hii huifanya vigumu kufuatilia kusambaa kwa virusi.

WHO wanasema mataifa 30 katika kanda yao ya Afrika (ambayo haijumuishi Misri, Sudan, Somalia, Djibouti, Libya, Tunisia na Morocco) zinashuhudia kuenea kwa virusi kwenye jamii.

Ni mataifa gani yaliyoathirika zaidi?

Mataifa mawili yanayoongoza kwa visa vya wagonjwa ni Afrika Kusini na Misri. Mataifa hayo mawili yalichangia zaidi ya asilimia 60 ya visa vipya vya maambukizi vilivyoripotiwa barani Afrika mwishoni mwa mwezi Juni.

Afrika Kusini ndiyo inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi, nayo Misri ndiyo yenye idadi ya juu zaidi ya vifo vilivyotokana na corona.

Afrika Kusini ilichukua moja ya hatua kali zaidi Afrika za kuwazuia watu kusafiri na kutangamana ili kuzuia kusambaa vya virusi mwezi Machi.

Lakini visa vimekuwa vikiongezeka pakubwa baada ya masharti kulegezwa Mei na Juni.

Mkoa wa Cape Magharibi, ambapo jiji la Cape Town hupatikana, limechangia karibu nusu ya visa vyote vya maambukizi nchini humo na zaidi ya nusu ya jumla ya vifo.

Lakini visa vinaongezeka sana mkoa wa Gauteng ambapo jiji la Johannesburg hupatikana.

Nchini Misri pia, visa vimekuwa vikiongezeka tangu katikati ya mwezi Mei, ambapo visa vilifikia kilele mwishoni mwa Juni kabla ya kuacha kuongezeka sana.

Upo wasiwasi pia kuhusu kinachotokea nchini Nigeria, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika. Taifa hilo lilikuwa la pili kwa ongezeko la vifo vilivyotokana na Covid-19 baada ya Afrika Kusini katika ripoti ya WHO iliyotolewa 1 Julai.

Angalizo: Ramani, jedwali na mchoro unaobadilika wenyewe kwenye makala hii vyote vinatumia takwimu kutoka chanzo tofauti kuhusu Ufaransa tofauti na zilizotumiwa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins University, jambo ambalo linachangia idadi ya jumla ya visa kuwa chini kidogo. Takwimu za Marekani pia hazijajumuisha Puerto Rico, Guam au visiwa vya Virgin vya Marekani.

Mauritania magharibi mwa Afrika pia imeshuhudia ongezeko kubwa la visa, na taifa hilo limekuwa miongoni mwa mataifa yanayoandikisha ongezeko kubwa zaidi wiki za karibuni.

Ni vyema kusisitiza kwamba yapo baadhi ya maeneo barani Afrika ambapo visa vya wagonjwa havijakuwa vingi sana, kwa mfano Afrika Mashariki.

Ni watu wangapi wanafariki Afrika?

Kwa jumla, kiwango cha vifo vinavyotokana na corona barani Afrika kimekuwa cha chini ukilinganisha na kiwango cha vifo cha wastani duniani. Hii ni licha ya kwamba mataifa mengi Afrika yana mifumo duni ya afya.

WHO inasema hili linaweza kuwa limechangiwa na hali kwamba watu wengi Afrika wana umri mdogo. Zaidi ya asilimia 60 ya watu Afrika wana chini ya miaka 25.

Lakini yapo mataifa matano ambayo yana viwango vya vifo vinavyokaribiana au vilivyo juu ya kiwango cha kadiri cha vifo vinavyotokana na corona duniani ambacho kwa sasa ni 5%:

  • Chad (8.5%)
  • Algeria (6.6%)
  • Niger (6.2%)
  • Burkina Faso (5.5%)
  • Mali (5.3).

Githinji Gitahi, mkuu wa Amref Health Africa, shirika lisilo la kiserikali linalohusika na masuala ya afya barani, anasema viwango hivyo vya juu huenda vikawa viashiria vya viwango vya juu vya maambukizi, lakini pia vinaweza kutokana na viwango vya chini vya upimaji.

Ukifanya vipimo vichache, ndivyo utakavyowagundua watu wachache walioambukizwa, na kwa hivyo viwango vya vifo vinaonekana kuwa vya juu.

WHO inasema pia kwamba matumizi ya wahudumu wa afya kwenye jamii kuripoti visa vya Covid-19 yanaweza kuwa yamechangia kiwango cha juu cha vifo kinachoripotiwa kwa mfano nchini Chad.

Viwango vya upimaji vikoje Afrika?

Mataifa kumi yamechangia asilimia 80% ya vipimo vyote vya corona ambavyo vimefanywa barani Afrika - Afrika Kusini, Morocco, Ghana, Misri, Ethiopia, Uganda, Mauritius, Kenya, Nigeria na Rwanda.

Kuna tofauti kubwa sana katika idadi ya vipimo vinavyofanywa. Afrika Kusini kwa jumla imefanya vipimo vingi zaidi lakini Nigeria ukilinganishwa na idadi yake kubwa ya watu haijafanya vipimo vingi, kwa mujibu wa Our World in Data, shirika lenye makao yake Uingereza ambalo limekuwa likikusanya taarifa kuhusu Covid-19.

Kufikia 1 Julai, Afrika Kusini ilikuwa ikifanya vipimo 27 kwa kila watu 1,000, ukilinganisha na 77 Uingereza na 97 Marekani.

Lakini ikumbukwe kwamba katika baadhi ya mataifa ya Afrika ni vigumu kujua nini hasa kinaendelea kutokana na kutotolewa kwa takwimu au takwimu kutokamilika.

"Ni lazima tutilie shaka kiasi takwimu [za maambukizi] zinazotolewa," anasema Chiedo Nwankwor, mhadhiri wa masuala ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani.

Nchini Tanzania, Rais Magufuli ametilia shaka usahihi wa matokeo ya vipimo vilivyofanywa na maabara ya taifa, na tangu mwishoni mwa Aprili, maafisa wa serikali wamekuwa wakitoa takwimu zisizo kamilifu kuhusu maambukizi, vifuo na vipimo vya corona.

Equatorial Guinea nayo ilikuwa na mzozo na WHO baada ya kumtuhumu mwakilishi wa shirika hilo kuwa alikuwa akichakachua takwimu za Covid-19. WHO ilikanusha tuhuma hizo.

Hata hivyo, taifa hilo limeanza kutangaza takwimu zake tena kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kukinga dhidi ya Magongwa Afrika (Africa CDC).

Na jimbo la Kano, kaskazini mwa Nigeria, karibu vifo 1,000 viliripotiwa mwishoni mwa Aprili, lakini serikali bado haijathibitisha idadi hasa ya vifo hivyo vilivyotokana na Covid-19.