Julai 4: Trump aapa kushinda wapinzani wake katika hotuba ya siku ya uhuru

Rais wa Marekani Donald Trump ametumia hotuba yake ya maadhimisho ya uhuru kuapa kushinda wapinzani wake huku maandamano ya haki za kiraia yakiendelea kote nchini humo.
Katika hotuba yake, Trump alisema atapigania kulinda 'Maisha ya Mmarekani', huku akishutumu waandamanaji kwa kulenga masanamu ya kihistoria.
Kabla ya hotuba yake, waandamanaji wa 'Black Lives Matter' walikuwa wamekusanyika katika maeneo yaliyo karibu.
Tofauti na Bwana Trump, mpinzani wake katika uchaguzi wa urais wa chama cha Democrat, Joe Biden alisema kila mmoja ana haki ya kupata mgao wa ndoto ya Marekani.
Hotuba ya Trump Julai 4, iliangazia hatua iliyopigwa katika kukabiliana na janga la corona licha ya kuongezeka kwa idadi ya wanaopata maambukizi kote nchini humo.
Wakati akiwa anaendelea kukosolewa kwa jinsi alivyokabiliana na ugonjwa wa Covid-19, Trump alisema kwamba China - kitovu cha virusi vya corona - inastahili kuwajibishwa kikamilifu.
Aidha, rais alishutumu waandamanaji kwa kuharibu masanamu ya wanaotajwa katika historia ya Marekani kupitia maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika siku za hivi karibuni yanayopinga ubaguzi wa rangi.
"Lengo lao ni kuharibu," amesema
Katika hotuba iliyoonekana kuendana na ile ya Ijumaa alipokuwa mlima Rushmore kusini mwa Dakota, Rais aliahidi kushinda wapinzani wake wa mrengo wa kushoto wenye mawazo ya Marxi, wanaopinga serikali, wenye nia ya kufitini na waporaji.
Alizungumza katika bustani ya Ikulu ya Marekani akiwa ameambatana na mke wake Melania, kwenye Umma uliokuwa umejumuisha wanajeshi wa Marekani na wahudumu wa afya.
Akisifia utaalamu wa kisayansi wa Marekani, Bwana Trump alisema hivi karibuni Marekani ama itakuwa na tiba na au chanjo kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus, Juni alionya kwamba huenda wanasayansi wasifanikiwe kupata chanjo madhubuti dhidi ya virusi vya corona na kusema: "Makadirio ni kwamba tunaweza kupata chanjo ndani ya mwaka mmoja. Ikiwa mchakato utaharakishwa, inaweza ikawa chini ya muda huo, lakini itachukua miezi kadhaa. Hivyo ndivyo wanasayansi wanavyosema."

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani ina idadi kuwa ya waliokufa kwa virusi vya corona na kupata maambukizi na imethibitisha maambukizi mapya 43,000 ndani ya saa 24 Jumamosi, kulingana na takwimu za chuo kikuu cha Johns Hopkins. Florida, ambako hasa idadi ya walioambukizwa imeongezeka imerekodi maambukizi 11,458.
Rais hakuzungumzia kuhusu karibia vifo 130,000 ambavyo vinahusishwa na jana la corona.
Alisema Marekani imepima takriban watu milioni 40, na kuongeza kuwa asilimia 99 ya maambukizi ya virusi vya corona havina madhara dai ambalo hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha hilo.
Maneno ya Trump yalifuatiwa na msafara wa ndege za kijeshi juu ya anga ikiwa ni pamoja na zile za kivita za B-52 na F-35.

Chanzo cha picha, Reuters
Kabla ya hotuba ya Trump, waandamanaji wa Black Lives Matter walikuwa wamekusanyika nje ya Ikulu ya Marekani - maandamano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara kupinga ubaguzi wa rangi tangu kuuawa kwa raia mweusi wa Marekani George Floyd mikononi mwa polisi.
Je kipi kingine alichosema Trump?
Akizungumzia janga la virusi vya corona Marekani, rais alisema kuwa utawala wake umepiga hatua na mkakati wao unaendelea vizuri licha ya kuongezeka kwa maambukizi kote nchini humo.
Bwana Trump ambaye anatafuta kuchaguliwa tena mwaka huu anaonekana kuwa tayari kukabiliana na mrengo wa kihafidhina kwa kutoa wito wa uzalengo na kushtumu China kwa kujaribu kuficha ukweli baada ya kutokea kwa mlipuko wa virusi corona dai ambalo China inakanusha.
"Usiri wa China, uongo na kuficha ukweli kulifanya virusi kusambaa kote duniani," Trump alidai.
Akizungumzia mpango wake wa kujenga "Bustani ya Taifa ya Mashujaa wa Marekani ", Bwana Trump alisema kwamba urithi wa nchi hiyo ni wa raia wote.
"Wazalendo waliojenga nchi yetu hawakuwa wasaliti," alisema. "Walikuwa mashujaa."
Marekani iliadhimisha vipi siku ya uhuru wao?
Matukio mengi ya Umma ambayo watu huadhimisha siku ya uhuru yaliahirishwa huku sehemu za ufukweni kama Florida na California zikifungwa na gwaride mijini ambayo imezoeleka ikifutwa.
Joe Biden, mpinzani wa Trump kupitia chama cha Democratic katika uchaguzi wa urais mwaka huu, aliandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisema: "Julai 4, ya mwaka huu, moja ya kitu cha uzalendo unachoweza kufanya ni kuvaa barakoa".

Chanzo cha picha, Reuters












