Virusi vya corona: Kusafisha choo 'kunaweza kurusha virusi vya maambukizi futi 3 hewani'

Chanzo cha picha, Getty Images
Kusafisha au kusukuma maji ya choo cha ndani kunaweza kusababisha wingu ambalo linaweza kuvutwa kwa pua na kusambaza maambukizi, kama vile virusi vya corona, wanasema watafiti.
Wanasayansi wa China walibaini kuwa kuvuta maji yaani (kuflashi) choo kunaweza kusababisha mvuke unaoweza kupanda hadi nje ya bakuli la choo, na kufikia urefu wa mtu au hata zaidi.
Matone hayo yanaweza kuruka hadi umbali wa futi 3- au sentimita 91 - kutoka usawa wa bahari, kwa mujibu wa vipimo vilivyochukuliwa na kompyuta iliyotumiwa na wanasayansi kutoka Chuo kikuu cha Yangzhou.
Kufunika choo wakati wa kusafisha kwa maji kunaweza kuepusha hili.
Kazi hii ya wanasayansi imechapishwa katika jarida la fizikia ya vimiminika yaani Physics of Fluids.

Chanzo cha picha, Getty Images
Virusi vya corona husambaa hewani kupitia matone ya maji maji kwa njia ya kikohozi na kupiga chafya, au vitu vyenye virusi hivyo.
Watu ambao wameambukizwa wanaweza pia kuwa na virusi hivyo katika choo chao, ingawa haijawa wazi iwapo hii inaweza kuwa ni njia nyingine ya kusambaza ugonjwa wa corona kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanasayansi kote duniani wanapima mifumo ya maji ya vyoo na maji machafu kubaini ni vipi baadhi ya watu waliweza kupata maambukizi ya virusi vya corona.
Virusi wengine wanaweza kusambazwa kutokana na uchafu wa vyoo.
Wakati maji yanapomwagwa ndani ya choo wakati wa kuflashi, msukumo wa maji husababisha matone ya maji kupaa juu. Matone hayo ni madogo sana hupaa hewani kwa zaidi ya dakika moja, kwa mujibu wa mwandishi wa utafiti Ji-Xiang Wang na wenzake kutoka Cho kikuu cha Yangzhou nchini China.
Dkt Bryan Bzdek, kutoka kituo cha utafiti cha Chuo kikuu cha Bristol nchini Uingereza anasema, hakuna ushahidi wa wazi kwamba virusi vya corona vinaweza kusambaa kwa njia hii, lakini ni jambo la muhimu kuchukua tahadhari.
"Walioandika utafiti wanasema kwamba, pale inapowezekana, tunapaswa kufunika kiti cha choo, kila tunapovuta maji ili kukisafisha, tusafishe vishikio vya kuvuta maji na kunawa mikono yetu baada ya kujisaidia.
"Huku utafiti huu ulishindwa kuonyesha kuwa hatua zikichukuliwa zinaweza kupunguza kusambaa kwa virusi vya SARS-CoV-2 , virusi vingine vingi vinasambazwa kwa njia ya kinyesi kwa hiyo huu ni usafi unaofaa, hivyo basi ni vema ukaufuata tu."













