Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano Uingereza: Zaidi ya watu 100 wamekamatwa baada ya kutokea vurugu jijini London
Zaidi ya watu 100 wamekamatwa baada ya kutokea kwa maandamano ya ghasia mjini London Jumamosi, kwa mujibu wa Polisi.
Polisi walivamiwa na waandamanaji, ambao wengine walikuwa wanaharakati wa mrengo wa kulia baada ya maelfu yao waliokuwa wamekusanyika kusema kuwa wanalinda masanamu yasiharibiwe.
Waziri Mkuu Boris Johnson alisema: "Uhalifu unaofanywa kwa misingi ya ubaguzi hauna nafasi katika maeneo yetu."
Aidha uchunguzi unaendelea baada ya mwanaume mmoja kuonekana akikojoa karibu na kumbukumbu ya PC Keith Palmer, aliyeuawa 2017 katika uvamizi wa Westminster 2017.
'Chuki'
Waziri wa mambo ya ndani Priti Patel amesema "kudhalilishwa kwa kumbukumbu ya PC Palmer ni aibu kubwa".
Kamanda wa Polisi Bas Javid aliongeza: "Tunajua kwamba kuna picha ya chuki inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayomuonesha mwanaume mmoja anayeonekana akikojoa kwenye kumbukumbu ya afisa wa polisi, PC Palmer.
"Tumeanzisha uchunguzi mara moja na tutakusanya ushahidi wote tunaoweza kupata na kuchukua hatua stahiki."
Mbunge Tobias Ellwood, aliyetoa huduma ya kwanza kwa PC Palmer alipokuwa anakufa baada ya kudungwa kisu katika majengo ya bunge na Khalid Masood 2017, anasema picha ya mwanaume akikojoa kando tu ya kumbukumbu hiyo inachukiza.
Ameiambia BBC: "Mwanaume huyo alikuwa anajua anachotenda, anastahili kujitokeza na kuomba msamaha."
Mwanaume akamatwa kwa kukojolea kumbukumbu PC Keith Palmer
Mwanaume mmoja amekamatwa akishutumiwa kukojoa kwenye kumbukumbu ya Westminster iliyotengenezwa kwa ajili ya Keith Palmer.
Inaaminika tukio hilo lilitokea Jumamosi mchana.
Bwana Palmer, 48, alidungwa kisu akiwa kazini katika shambulio la Westminster la Machi 22, 2017. Ni mmoja kati ya watu watano waliouawa na Khalid Masood.
Mwanaume huyo ambaye amekamtawa na polisi kwa sasa hivi anazuiliwa katika kituo cha Essex baada ya kujipeleka mwenyewe kituoni.
Jiwe la kumbukumbu liliwekwa eneo la Carriage Gates, Westminster, pale ambapo PC Palmer alivamiwa.
Aidha polisi imesema jiwe hilo ni ukumbusho kwa kujitolea na ujasiri wa afisa PC Palmer.
Maandamano Uingereza.
Jumamosi, maandamano kadhaa ya amani yanayopinga ubaguzi wa rangi yamefanyika katika mji wa London na kote nchini humo.
Polisi imesema waandamanaji wamekamatwa kwa makosa kadhaa ikiwemo, kufanya vurugu, kushambulia polisi, umiliki wa silaha, kuvuruga amani, kuwa walevi na kusababisha vurugu pamoja na umiliki wa dawa za kulevya daraja la A.
Inasemekana maandamano hayo yamekiuka miongozi iliyopo kwa kutekeleza vurugu.
Wakati makundi makubwa ikiwemo ya waandamanji wa mrengo wa kulia yakitanda kote Uingereza, kumekuwa na ghasia kati ya waandamani na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia.
Maafisa sita wamepata majeraha madogo katika maandamano hayo.
Taarifa kutoka idara ya utoaji wa huduma ya mgari ya kubeba wagonjwa London zimethibitisha kutibu watu 15 ikiwemo maafisa wawili wa polisi.
"Sita kati yao - wote wakiwa ni raia - na wamepelekwa hospitali."
Waandamanaji wa vuguvugu la 'Black Lives Matter' walitaka watu kutoshiriki maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika mwishoni mwa juma kwa hofu ya kwamba huenda kukatokea vurugu na makundi ya mrengo wa kulia.
Huko Brighton, maelfu walipanga foleni katika eneo la pwani kuashiria maandamano ya amani kabla ya kuelekea mjini.
Maandamano yamekuwa yakitokea kote duniani baada ya kifo cha Gorge Floyd aliyekufa mikononi mwa polisi mwezi uliopita ncini Marekani.
Maeneo mengine yaliyoshuhudia maandamano ni pamoja na Liverpool, Chelmsford na Newcastle, ambapo waandamanaji wanaounga mkono vuguvugu la Black Lives Matter wamekabiliana na makundi mengine yanayopinga maandamano hayo.