Coronavirus: Kwa nini kuna hali ya sintofahamu katika mpaka wa Namanga na Holili?

Madereva wa Tanzania wamelalamika kuwa vyeti vyao vimekuwa vikikataliwa wanapoingia nchini Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Madereva wa Tanzania wamelalamika kuwa vyeti vyao vimekuwa vikikataliwa wanapoingia nchini Kenya
Iliyochapishwa

Mipaka miwili ya Tanzania na Kenya eneo la Namanga na Holili imefungwa tena baada ya kuibuka hali ya sintofahamu kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa kati ya nchi hizo mbili.

Madereva wa Tanzania wamelalamika kuwa vyeti vyao vimekuwa vikikataliwa wanapoingia nchini Kenya hali inayosababisha taharuki kubwa miongoni mwa madereva wa Tanzania wanaovuka mpaka wa Namanga kuingia nchini Kenya.

Mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe ameeleza kuwa hakuna ushirikiano mzuri walioupata walipokuwa wakifuatialia kilichojiri katika mpaka wa Namanga.

Akiongelea adha wanayopata madereva wa malori wa Tanzania wanapoingia upande wa Kenya Mkuu huyo wa wilaya amesema suala hilo halijatolewa ufumbuzi na serikali ya Kenya ili kuondoa adha hiyo.

''Haiwezekani kwamba dereva amepimwa siku mbili tatu zilizopita kisha anarudia tena kwenda kupimwa eneo jingine kwanza tumeona kitendo hicho ni kitendo cha dharau.''

''Lakini cha pili huwezi kuvunja makubaliano bila kuwa na taarifa zozote za msingi. Alisema Bwana Mwaisumbe.

Kwa sasa hakuna shughuli zozote zinazoendelea, mpaka wa Namanga umefungwa.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, kuna magari zaidi ya 500 yaliyoegeshwa Arusha, Longido na mengine Namanga.

Wakizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, madereva wa Kenya wamekiri kuwepo kwa changamoto kwa madereva wa Tanzania wanapoingia upande wa Kenya , wakisema kuwa Kenya inakiuka makubaliano.

''Upande wetu wa Kenya hawazingatii kama Tanzania inavyozingatia sisi kwao wanatukubalia kutumia cheti tunachotoka nacho Kenya lakini Kenya hawakubali vyeti vya madereva wa Tanzania wakiingia upande wa Kenya hali hii inatusababisha tuumie sisi sote.'' Alisema Joseph Kariuki

Mpaka wa holili hali ikoje?

Mpaka wa Namanga ni moja ya mipaka ambayo imefungwa kutokana na sintofahamu iliyoibuka tena baina ya Tanzania na Kenya
Maelezo ya picha, Mpaka wa Namanga ni moja ya mipaka ambayo imefungwa kutokana na sintofahamu iliyoibuka tena baina ya Tanzania na Kenya

Biashara katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Holili pia imekuwa katika hali ya sintofahamu hali ambayo pia imefanya serikali ya mkoa kuingilia kati suala hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa haiwezekani kutokuwa na hali ya usawa katika biashara ambapo ni kinyume cha makubaliano.

''Huenda wiki ijayo mapema tukakaa pamoja kama msimamo wao hautaathiriwa na msimamo wetu wa kukataa madereva wao wasipite pia kwa kuwa hata wao tukiwapima tunawakuta wana virusi.''

''Haiwezekani kwamba biashara ifanyike upande mmoja tu, haiwezekani upande mmoja tu waingie na kutoka halafu huo huo upande ndio utangaze kufunga mpaka, huohuo upande ndio unaotumia mpaka kwa uhuru hapana.''

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa sasa bidhaa za Kenya hazitapita mpakani hapo, na magari yao hayatapita yasiyo na mzigo wa Tanzania.

Serikali ya Kenya imesema nini?

Waziri wa afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ameonesha kukerwa na baadhi ya madereva wasiofuata sheria akieleza vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na madereva wa malori wawapo safarini.

Waziri wa afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ameonesha kukerwa na baadhi ya madereva

Chanzo cha picha, Ministry of Health Kenya /Twitter

Maelezo ya picha, Waziri wa afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ameonesha kukerwa na baadhi ya madereva

Amesisitiza kuwa madereva wote wa malori lazima wapime virusi vya corona angalau saa 48 na kupata hati wanapokuwa hawana maambukizi zoezi linalopaswa kufanyika kabla ya kuanza safari.

''Tumegundua kuwa madereva wengi huanza safari kabla ya kupimwa na kupata nyaraka muhimu, wakitegemea kupimwa kwenye eneo la mpaka hali inayosababisha msongamano mkubwa usio wa lazima na ucheleweshaji unashuhudiwa katika maeneo ya mipaka yetu, huku ni kutokuwa na nidhamu jambo ambalo halikubaliki na halitavumilika, ninawataka maafisa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya madereva wanaolikuka utaratibu.'' Alisema Waziri Kagwe.

''Wengine wanafika boda wakiwa na vyeti vyao wanafuata sheria, lakini wanakaa siku mbili kwa kuwa wasio na vyeti wamezuia barabara, hata ukiangalia unaona kuna shida ya watu kutokuwa na nidhamu''

''Tuna shida pia upande wa Tanzania, hayo ni mambo mengine na tunasema ukija lazima uwe na cheti na ukiwa huna cheti huwezi ingia Kenya, kama ambavyo Mkenya ilivyo kwake hawezi kuingia Uganda au Tanzania kama hana cheti.''

Waziri Kagwe amesema cheti kinachotakiwa lazima kiwe cheti chenye maana kinachotambulika na maabara inayotambulika na Shirika la Afya duniani, WHO.

Unaweza pia kusoma:

Viongozi wa Tazania na Kenya walizungumzia mzozo wa mipaka

MAFULI NA KENYATTA

Chanzo cha picha, Anadolu Agency/Getty

Mipaka hii imefungwa tena baada ya awali kufunguliwa baada ya viongozi wa juu wa Kenya na Tanzania kufanya mazungumzo na kuafikiana kufungua mipaka hiyo lakini kukiwa na masharti ya kufuata ili kuondoa hali ya sintofahamu katika maeneo hayo muhimu kwa ustawi wa uchumi wa mataifa hayo mawili.

Viongozi wa Tanzania John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta waliwaagiza Mawaziri wa Uchukuzi na Wakuu wa Mikoa iliyopo katika pande zote za mpaka wa Tanzania na Kenya kukutana na kutatua mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa malori ya mizigo kuvuka mpaka huo.

Unaweza pia kutazama:

Maelezo ya video, Coronavirus: Utajuaje kuwa umeathirika na virusi?

Walikubalina kuwa viongozi wa pande zote mbili wanapaswa kukutana na kuutatua mgogoro huo haraka iwezekanavyo ili Watanzania na Wakenya waendelee kufanya biashara zao kama kawaida, na kwamba kuzuiwa kwa malori ya Tanzania yanayokwenda Kenya ama kuzuiwa kwa malori ya Kenya kuja Tanzania hakukubaliki.