Virusi vya Corona: Idadi ya waliopona corona Kenya yafikia 553

Iliyochapishwa

Wagonjwa 54 wa virusi vya corona wamethibitishwa kupona nchini Kenya , ikiwa ndio idadi kubwa zaidi kutangazwa kwa siku.

Idadi hiyo sasa inafanya waliopona nchini humo kufikia 553.

Hatahivyo taifa hilo limeandikisha wagonjwa 123 zaidi wa virusi vya corona baada ya saa 24 baada ya sampuli 2,112 kuchunguzwa.

Idadi hiyo mpya inaongeza wagonjwa wa virusi hivyo waliothibitishwa nchini humo kufikia 2,216.

Jumla ya sampuli 85,058 zimefanyiwa vipimo kufikia sasa .

Naibu waziri wa Afya Rashid Aman akizungumza na vyombo vya habari , amesema kwamba Nairobi ilikuwa na wagonjwa 44 , Mombasa ikithibitisha wagonjwa 34, Busia 20 na Uasin Gishu 12.

Wagonjwa wapya pia walirekodiwa katika wilaya za Kajiado -3 ,Kiambu -3, Nyeri -3, Kilifi -2, Garissa na Laikipia zikiwa na wagonjwa mmoja mmoja .

Dkt. Aman alitangaza kwamba watu watatu walifariki kutokana na ugonjwa huo na hivyobasi kufanya idadi ya waliofariki kufikia 74.

Kijana wa miaka 12 ni miongoni mwa wale waliofariki.

Taarifa zaidi kuhusu janga la corona Kenya

  • Kenya ilipokea maabara zinazoweza kuhamishwa na vifaa vya kupima kutoka Ujerumani vitakavyosaidia kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 huku idadi ya visa vya maambukizi ikizidi 1,000 .
  • Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza pia kuongezwa kwa muda wa udhibiti wa matembezi ya kuingia na kutoka katika maeneo ya Eastleigh jijini Nairobi na Makazi ya Old Town yaliyopo katika Kaunti ya mwambao wa Kenya- Mombasa hadi kufikia tarehe 6 Juni.
  • Katika siku za hivi karibuni Wizara ya Afya nchini Kenya imekua ikitangaza kuongezeka kwa viwango vya juu kwa maambukizi ya Covid-19 katika Kaunti ya Mombasa.
  • Maeneo mapya yamerekodi visa vipya vya virusi vya corona zikiwemo kaunti za Taita Taveta, Garissa na Meru.
  • Mpango uliopo kwa sasa ni kuwapima watu wengi.''Tumepokea vifaa vya kupima ndio maana tumeongeza shughuli ya upimaji'', alisema Katibu tawala wa wizara ya Afya Rashid Aman .