Idris Sultan ashitakiwa kwa kutumia namba ya simu isiyosajiliwa kwa jina lake

Idris Sultan

Chanzo cha picha, Haki miliki ya pichaIDRIS SULTAN-INSTAGRAM

Maelezo ya picha, Kesi dhidi ya Idris imeahirishwa mpaka Juni 9.
Iliyochapishwa

Mchekeshaji maarufu nchini Tanzania Idris Sultan ameachiwa kwa dhamana hii leo baada ya kupandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya kutumia namba ya simu ambayo haijasajiliwa jina lake.

Msanii huyo alikamatwa Jumanne wiki iliyopita baada ya kujisalimisha kituo cha polisi jiji Dar es Salaam.

Baada ya kushikiliwa na polisi kwa zaidi ya wiki moja Sultan amefikishwa katika mahakama ya Kisutu hii leo na kusomewa shitaka la kutosajili nambari ya simu aliyokuwa anaitumia ambayo imesajiliwa kwa jina la mtu mwengine.

Anayetajwa kusajili laini hiyo, Innocent Maiga pia ameshatkiwa pamoja na Bw Sultan kwa kosa la kutoarifu mabadiliko ya umiliki wa laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake.

Msanii huyo ameachiwa kwa dhamana baada ya watu wawili kusaini bondi ya Shilingi za Tanzania milioni 15 kila mmoja, wakili wake Bennedict Ishabakaki ameieleza BBC.

Wawili hao wanatuhumiwa kufanya makossa hayo kinyume cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektoniki na Posta, na endapo watakutwa na hatia watakabiliana na adhabu ya faini isiyopungua Shilingi milioni tano, ama kifungo kisichopungua miezi 12 ama vyote faini na kifungo.

Kesi dhidi ya msanii huyo imeahirishwa mpaka Juni 9.

Kabla ya kufikishwa mahakamani, polisi na wakili wa msanii huyo waliiambia BBC kuwa alikuwa pia akihojiwa kwa tuhuma za kutenda makosa ya kimtandao.

Wakili Ishabakaki pia aliiambia BBC kuwa mteja wake alikamatwa na kuhojiwa na polisi juu ya mkanda wa video uliosambaa mitandaoni hivi karibuni akionekana akiicheka picha ya zamani ya rais Magufuli.

Hata hivyo, hii leo, hakufunguliwa mashtaka yoyote kuhusiana na suala hilo.