Virusi vya Corona: Ushahidi wa awali waonesha jinsi inavyoweza kufundisha mfumo wa kinga kudhibiti corona

Iliyochapishwa

Ushahidi wa kwamba chanjo inaweza kuelekeza mfumo wa kinga wa mwanadamu kukabiliana na virusi vya corona kumeripotiwa na kampuni moja ya Marekani.

Kampuni hiyo ya Moderna imesema kwamba kupambana na kinga ya mwili kumebainika kwa watu wanane wa kwanza walioshiriki majaribio hayo salama.

Pia inasemekana kwamba vile kinga ya mwili itakavyo jibu uvamizi mwilini kulifanana kabisa na watu walioambukizwa kirusi chenyewe.

Majaribio makubwa ya kuona ikiwa kweli chanjo ni kinga dhidi ya ugonjwa wa kuambukiza wa corona yanatarajiwa kuanza Julai.

Utafutaji wa chanjo ya virusi vya corona umekuwa ukiendelea kwa kasi ambayo haijawahi kutokea hapo awali, huku makundi karibia 80 kote duniani yakifanyia kazi utafutaji wa chanjo hiyo.

Kampuni ya Moderna imekuwa ikifanya majaribio ya chanjo kwa ajili ya virusi vya corona inayoitwa mRNA-1273, miongoni mwa watu.

Chanjo hiyo ni sehemu ndogo ya chembe za urithi yaani jeni za virusi vya corona ambayo inadungwa wagonjwa.

Haiwezi kusababisha maambukizi au dalili za ugonjwa wa Covid-19 lakini inaweza kufanya kinga ya mwili ikaanza kuchukua hatua ya kujilinda.

Majaribio hayo ya chanjo yaliyosimamiwa na Taasisi ya Taifa ya kupambana na magonjwa na kuambukiza na mzio ya Marekani, ilionesha kwamba chanjo hiyo ilichangia uzalishaji wa kinga ya mwili ambayo inaweza kupambana na virusi vya corona.

Haya hivyo majaribio hayo ya kinga ya mwili yenye uwezo wa kukabiliana na virusi vya corona kumefanyika kwa watu wanane kati ya 45 walioshiriki majaribio.

Watu waliofanyiwa majaribio ama walikuwa wanapewa kiwango cha chini, cha kati au cha juu cha chajo hiyo. Kiwango cha juu cha chanjo kulihusishwa kuwa na athari nyingi.

Hata hivyo kampuni ya Moderna imesema kwamba hata watu waliopewa kiwango cha chini cha chanjo hiyo walikuwa na kiwango cha kinga ya mwili sawa na wagonjwa waliopona Covid-19.

Na kinga ya mwili ilipita kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na ile ya wagonjwa waliopona corona ambao walipewa kiwango cha kati cha chanjo.

Utafiti huo unafahamika kama awamu ya kwanza ya chanjo ya majaribio ya kuonesha kama ni salama wala sio kuangalia kama inafanya kazi.

Itachukua majaribio mengi kuona ikiwa watu wamelindwa dhidi ya virusi.

Hata hivyo, majaribio ya panya yalionesha kwamba chanjo hiyo inaweza kuzuia kuzaliana kwa viruzi kwenye mapafu.

"Data ya majaribio ya awamu ya kwanza, ingawa ni mapema mno, imeonesha kwamba chanjo ya mRNA-1273 inachochea mfumo wa kinga kuchukua hatua kutokana na ukubwa wa maambukizi ya kawaida," amesema Dkt. Tal Zaks, afisa mkuu wa matibabu wa kampuni ya Moderna.

Chanjo iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford

Chanjo ambayo ilianzishwa na chuo kikuu cha Oxford pia inafanyiwa majaribio lakini bado matokeo ya majaribio hayo hayajatolewa.

Hata hivyo, wasiwasi umeibuka kuhusu matokeo ya majaribio hayo yaliyofanyika kwa tumbili.

Majaribio hayo yalionesha wanyama waliopata chanjo walikuwa na dalili kidogo mno na pia hawakupata homa ya mapafu. Hata hiyo hawakupata kinga thabiti ya virusi hivyo na ishara ya virusi ilionekana kwa kiwango kilekile katika pua za tumbili hao kama ilivyo kwa tumbili ambao hawakuwa wamepata chanjo.

Profesa Eleanor Riley, kutoka chuo kikuu cha Edinburgh, amesema: "Ikiwa majibu kama hayo yalipatikana kwa binadamu chanjo hiyo huenda ikatoa kinga ya muda tu dhidi ya virusi vya corona kwa wanaopokea chanjo lakini itakuwa na uwezo mdogo wa kupunguza maambukizi katika jamii kwa upana wake."

Hata hivyo hadi pale majaribio hayo yatakapofanyika kwa binadamu ni vigumu kujua vile chanjo hiyo itakavyofanya kazi kwa mwanadamu.