Du Wei: Balozi wa China Israel anayedaiwa kuaga dunia akiwa usingizini

Iliyochapishwa

Balozi wa China nchini Israel, Du Wei , amefariki nyumbani kwake katika mji wa Tel -Aviv , kulingana na maafisa wa polisi wa Israel na vyombo vya habari.

Bwana Du , mwenye umri wa miaka 57 alipatikana ameaga katika kitanda chake na sababu ya kifo chake bado haijajulikana.

Alikuwa ameteuliwa kuwa balozi mwezi Februari baada ya kuhudumu kama balozi wa China nchini Ukraine.

Balozi huyo alikuwa ameoa na alikuwa na mtoto wa kiume lakini familia yake haijulikani iwapo ilikuwa nchini humo.

Alikuwa akiishi katika mtaa wa Herzliya mjini Tel Aviv.

Msemaji wa polisi nchini Israel aliambia chombo cha habari cha Reuters : Kama taratibu za kawaida maafisa wa polisi tayari wamefika katika eneo la tukio.

Runinga ya Israel Channel 12, ilinukuu vyanzo vya matibabu vilivyosema kwamba balozi huyo alifariki akiwa usingizini.

Katika ujumbe uliochapishwa katika tovuti ya ubalozi huo , muda tu baada ya uteuzi wake wa kuwa balozi, bwana Du aliusifu uhusiano kati ya China na Israel.

Siku ya Ijumaa , ubalozi wake ulimshambulia waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo ambaye alikuwa ameikosoa China kwa jinsi ilivyokuwa inalishughulikia suala la virusi vya corona wakati wa ziara yake nchini Israel.

Katika chapisho lake lililowekwa katika gazeti la Jerusalem Post, ubalozi huo uliyashutumu matamshi ya bwana Pompeo kama 'upuuzi', na kukana madai kwamba China ilificha kuhusu mlipuko huo.