Virusi vya corona: Idadi ya wagonjwa Kenya yafikia 758, huku wagonjwa wengine 21 wakithibitishwa

malori Malaba

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Mipaka isiolindwa sasa imetajwa kuwa miongoni mwa maeneo hatari katika maambukizi ya virusi vya corona kulingana na naibu waziri wa Afya nchini Kenya Mercy Mwangangi.

Mwangangi amesema kwamba serikali inaweka mikakati ya kukabiliana na maambukizi zaidi wakati ambapo madereva kutoka Tanzania walipatikana na corona na kuzuiwa kuingia nchini siku ya Alhamisi.

Saba kati yao walipatikana katika mpaka wa Namanga huku mmoja akipatikana katika mpaka wa Isibania katika kaunti ya Migori.

''Kama Jumuiya ya mataifa ya Afrika mashariki tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara katika kukabiliana na tatizo hilo. Tunachunguza maeneo hayo, Wakenya wanapaswa kuwa watulivu'' , alisema.

coronavirus
Maelezo ya sauti, Virusi vy corona: Tanzania yasema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi

Ametoa wito kwa jamii zinazoishi katika maeneo hayo ya mpakani kuwa makini.

''Tangu ugonjwa huu uingie Kenya sote tumeathirika kwa njia moja au nyengine'' , alisema.

Naibu huyo amesema kwamba serikali imekuwa ikiwasiliana na mataifa inayopakana nayo kuhusu viwango vya maambukizi, na imetoa wito kwa raia wanaoishi mipakani kutoa taarifa zozote za wale wanaoingia nchini kwa njia haramu.

Wakati huohuo naibu huyo wa waziri amesema kwamba Kenya imerekodi wagonjwa wapya 21 wa virusi vya corona na kufanya idadi ya wagonjwa waliothibitishwa nchini humo kuwa 758.

madereva wa malori wakifanyiwa vipimo vya corona katika mpaka wa Malaba Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, madereva wa malori wakifanyiwa vipimo vya corona katika mpaka wa Malaba Uganda

Hii ni baada ya sampuli 1,486 kupimwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Kufikia sasa serikali ya Kenya imewapima takriban watu 36,918 tangu kisa cha kwanza kiripotiwe tarehe 13 mwezi Machi.

Mwangangi pia alitangaza kwamba wagonjwa wengine wawili walifariki na hivyobasi kufanya idadi ya waliofariki kufikia 42.

Siku ya Jumatano, madereva 25 waliokuwa wakitoka nchini Tanzania walikutwa na virusi hivyo katika mpaka wa Namanga na kuzuiliwa kuingia Kenya.

Katibu tawala wa wizara ya Afya Rashid Aman alisema kwamba wagonjwa 23 ni raia wa Tanzania , mmoja kutoka Rwanda na mwengine kutoka Uganda.