Virusi vya corona: Je hali iko mbaya kiasi gani nchini Saudi Arabia?

Iliyochapishwa

Kuna wakati ilikuwa maarufu kwa kutotoza ushuru, Saudi Arabia lakini kwa sasa hivi imetangaza kodi ya ongezeko la thamani kuanzia asilimia 5 hadi asilimia 15 na pia kukatiza ruzuku inayotolewa kila mwezi kuanzia mwezi ujao.

Hatua hiyo inawadia wakati ambapo bei ya mafuta duniani imeshuka tena kwa zaidi ya nusu ikilinganishwa na bei yake mwaka mmoja uliopita, na kupunguza mapato ya serikali kwa asilimia 22 huku miradi mingine ya serikali ikisitishwa.

Saudi Aramco, kampuni ya serikali ya mafuta tayari faida yake imepungua kwa asilimia 25 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka sababu kuu ikiwa ni kushuka kwa bei ya mafuta.

"Hatua hizi zinaakisi uhitaji wa haraka wa kudhibiti matumizi na kujaribu kuimarisha bei ya mafuta ambayo iko chini," amesema mchambuzi wa masuala ya Uarabuni Michael Stephens. "Uchumi huo wa kifalme uko katika hali mbaya na itachukua muda kuanza kuimarika na kurejea katika hali ya kawaida."

Covid-19 kwasasa hivi inasababisha maafa katika uchumi wa nchi mbalimbali ambazo zinategemea mamilioni ya wafanyakazi raia wa kigeni wasiokuwa na ujuzi kutoka bara la Asia ambao wengi wao wanaishi kwa makundi na hali yao ya usafi ni duni.

Wakati huohuo, mwanamfalme ambaye bado ni maarufu sana nyumbani, lakini anaonekana kama mhuni katika nchi za Magharibi kwasababu ya kile kinachodaiwa kuwa alichotekeleza katika mauaji ya mwanahabari wa Saudia Jamal Khashoggi.

Imani kwa wawekezaji wa kimataifa bado haijarejea kwa asilimia 100 kuanzia kuuawa kinyama kwa mwanahabari huyo hadi ushiriki wa majasusi wa serikali ndani ya ubalozi wa Saudia uliopo Istanbul 2018.

Vita katika nchi jirani ya Yemen vimekuwwa vikimaliza maafisa wa Saudia kwa miaka mitano na vilipofikia ni kwamba havina tija yoyote, na pia mgogoro na Qatar umeyumbisha amani iliyokuwepo katika mataifa sita ya Baraza la Ushirikiano la Kiarabu la Ghuba.

Sasa basi Je Saudi Arabia imejikuta katika matatizo makubwa?

'Wapi pa kuegemea'

Kwanza, virusi vya corona vimetatiza uchumi wa nchi mbalimbali kote duniani na Saudi Arabia haijasazwa.

Ndio, ina mfuko wa fedha wa utawala, fedha za uwekezaji kwa umma kama njia ambazo inaweza kuzigeukia kukomboa hali thamani yake ikiwa ni $320bn (£260bn; 295bn euros).

Pia kuna kampuni ya Saudi Aramco, ambayo kwa kiasi kikubwa ina milikiwa na serikali, mwaka jana ilisemekana kuwa na thamani ya $1.7 trillion - wakati huo, thamani yake ikiwa ni sawa na kampuni ya mawasiliano ya Google na Amazon kwa pamoja.

Kwa mauzo kidogo tu ya asilimia 1.5 Saudi Arabia imefanikiwa kupata zaidi ya $25bn ikiwa ni kiwango kikubwa cha hisa katika historia yake.

"Saudi Arabia ina maeneo mengi ya kujikomboa," amesema Bwana William Patey, aliyekuwa balozi wa Uingereza kwa Riyadh kati ya 2007-10. "Wanahifadhi nyingi za kuwawezesha kusonga mbele na bado wanaweza kujikwamua kutokana na soko lao la hisa ama lilivyo au hata likiimarika zaidi."

Kwa sasa, tishio kwa nchi hiyo kutoka Iran kunaonekana kupungua kufuatia shambulio la kigaidi la Septemba mwaka jana katika viwanda vyake vya mafuta na baadae, kuuawa kwa kamanda wa jeshi la Iran Qasem Soleimani mwezi Januari.

Mwezi huu, Marekani imeondoa makombora yake yaliyokuwa yametumwa kama hatua ya dharura ya kujilinda. Tishio la ugaidi ndani ya nchi ambalo linaonekana kujificha kutoka kwa kundi la Jihadi lenye kuhusishwa na kundi la Islamic State (IS) na al-Qaeda, likiwa haliwezi kusemekana kwamba limeisha kabisa, zaidi ya kwamba kwa kiasi kikubwa limepungua.

Lakini bado Saudi Arabia inakumbana na changamoto si haba:

Uchumi

Taarifa iliyotolewa wiki hii ya kubana matumizi bila shaka haijapokelewa vyema na raia wengi wa Saudia, ambao wamekuwa na matumaini ya hatma nzuri chini ya mipango makhususi ya kuimarisha uchumi mbali na mapato ya mafuta.

Hata waziri wa fedha mwenyewe alirejelelea mipango hiyo kama hatua zenye machungu. Madhumuni ya mipango hiyo ni kunusuru dola bilioni 26 lakini uharibifu unaosababishwa na Covid 19- na kushuka kwa bei ya mafuta ambako tayari kumegharimu benki kuu ya Saudi kiasi sawa na hicho katika kipindi cha mwezi mmoja tu wa Machi pekee.

Katika kipindi cha robo kwanza ya mwaka kuna nakisi ya bajeti ya $9bn.

Hii sio mara ya kwanza Saudi Arabia imelazimika kuchukua hatua za kubana matumizi. Mei 1998, nilihudhuria mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Kiarabu la Ghuba huko Abu Dhabi wakati ambapo mwana mfalme Abdullah alitoa onyo kali kwa viongozi wenzake wa kanda hiyo ya Uarabuni.

"Mafuta ni $9 kwa pipa," aliwambia. "Wakati wa kuvuna umeshaisha na hautarejea tena. Sasa ni wakati wa sisi sote kupunguza matumizi."

Na baadae, bei ya mafuta ikapanda hadi zaidi ya $100 kwa pipa, lakini haikuchukua muda kabla ya serikali kusitisha ajira na kupunguza miradi ya ujenzi kote nchini humo.

Wakati huu hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Virusi vya corona na kushuka kwa bei ya mafuta kumetatiza miradi yote kote nchini humo na kuzua maswali ikiwa azimio la mpango wa ruwaza ya mwaka 2030 bado inaweza kufikiwa.

Mpango huo ambao unalenga kumaliza tegemezi la tangu mwanzo kwa nchi hiyo katika historia yake la mapato ya mafuta na wafanyakazi raia wa kigeni umetengewa dola bilioni 500.

Maafisa wanasema kwamba hilo bado linaendelea lakini wachambuzi wengi wanaamini kucheleweshwa kwa utekelezaji wa azimio hilo pamoja na kupunguzwa kwa pesa zilizokuwa zimetengwa ni jambo lisilo epukika.

"Sekta ya kibinafsi hasa itaathirika vibaya na hatua ya kubana matumizi, amesema Michael Stephens.

"Hatua za dharura za kubana matumizi zinadhuru watengenezaji wa ajira, jambo ambalo litafanya iwe vigumu zaidi kujikwamua katika kipindi cha muda mrefu."

Msimamo ngazi ya ulimwengu

Sifa ya Saudi Arabia duniani iliharibika vibaya wakati wa mauaji ya mwanahabari Khashoggi na pale ilipobainika kwamba wanajaribu kuficha ukweli.

Hata balozi wa Saudi Arabia Uingereza aliita tukia hilo "doa katika sifa yetu".

Kesi na kufunguliwa mashtaka kwasababu ya mwanahabari huyo ambako baadhi ya washukiwa walipatikana bila hatia, kulisababisha ukosoaji zaidi kutoka makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na taarifa maalum kutoka Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kiholela.

Saudi Arabia bila shaka ni kubwa na muhimu kwa uchumi wake kupuuzwa na duniani.

Hivi karibuni imekuwa ikijitahidi katika mikakati ya uwekezaji wa ngazi ya juu kama vile azma yake ya kutaka kupata asilimia 80 ya hisa ya klabu cha mpira wa soka Newcastle, hatua ambayo imepingwa vikali na mjane wa Khashoggi, Hatice Cengiz, kwa misingi ya kimadiili.

Kwa kiasi fulani, vita ya Yemen vimechangiwa na Saudi Arabia pale ndege zake za kivita zilipotekeleza mashambulio ya anga baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Marekani na Uingereza na kusemekana kwamba huo ni uhalifu wa kivita uliotekelezwa na pande zote.

Lakini vifo vya raia pia vimeongezeka sana kwasababu ya mashambulio ya anga na kuongeza ukosoaji kutoka Washington na kwengineko.

Mafaniko ya vita hivyo ni machache mno zaidi ya kuharibu nchi hiyo maskini ya Uarabuni. Aidha uungwaji mkono kwa Riyadh pia umepungua kwa kiasi kikubwa.

Washirika wake wakubwa ambao wamekuwa wakimuunga mkono mwana mfalme wa Saudia na kiongozi wa nchi hiyo Mohammed Bin Salman ni rais Trump na Putin.

Lakini mwaka huu, kwa kufungulia mifereji ya mafuta na kuharibu soko kimaksudi, aliudhi viongozi hao wawili kwa kusababisha hasara katika soko lao la ndani.

Uhusiano na Iran bado upo katika hali ya vita baridi na wanahasira kidogo na majirani zao Qatar.

Nyumbani mwanamfalme amekuwa akiharakisha mpango wa mabadiliko ya kijamii na kuondoa marufuku ya wanawake kuendesha gari na kuruhusu vile ambavyo vilikuwa mwiko kama sinema, mikusanyiko ya pamoja kati ya wanawake na wanaume mashindano ya magari.

Hivi leo kwa mtazamo wa juuu, Saudi Arabia imebadilika.

Lakini nyuma ya pazia, yeyote yule atakayejaribu kuhoji sera zinazoendelezwa anajiweka katika hatari ya kukamatwa na kuzuiliwa gerezani au hata kufungwa kwa makosa ya kutishia usalama wa taifa.

Mauaji ya kiholela bado yanaendelea nan chi hiyo bado ni miongoni mwa zinazokosolewa pakubwa na makundi ya haki za kibinadamu.

Licha ya haya yote, bado Saudi Arabia ni mshikadau mkubwa katika uchumi wa kimataifa na pia inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa G20 Novemba ingawa washirika wake wanaichukulia kama mwenye kuwatia aibu.

Uwezo wa kisiasa

Akiwa na miaka 34, Mwana mfalme Mohammed Bin Salman anaonekana kuwa mtu asiyetaka kupingwa. Pia anaungwa mkono na baba yake, 84, King Salman, na amekuwa akimuondoa yeyote anayeoonekana kuwa mpinzani wake madarakani.

Binamu yake mfalme Mohammed Bin Nayef, aliyemrithi kama mwana mfalme baada ya mapinduzi yaliyotokea kwenye makazi ya ufalme 2017, ni miongoni mwa viongozi wengi waandamizi ambao wamezuiliwa.