Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona Korea Kusini: Wasiwasi wa wimbi la pili baada ya watu karibia 100 kudaiwa kuambukizwa
Alisifiwa kwa hatua za haraka na madhubuti alizochukua kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona na katika kipindi cha muda mfupi alifanikiwa kupunguza maambukizi mapya.
Korea Kusini ilikuwa miongoni mwa nchi za kuanza kufungua tena shughuli za kiuchumi na kurejelelea maisha ya kawaida.
Lakini kwa sasa hivi Korea Kusini imejikuta tena matatani baada ya kutokea kwa mlipuko mpya wa maambukizi ambao bado haujadhibitiwa.
Hadi kufikia Mei 13, nchi hiyo ya bara Asia ilikuwa imeripoti maambukizi 119 ya ugonjwa wa Covid-19, idadi kubwa ikihusishwa na eneo la Itaewon mji maarufu kwa baa, migahawa na vilabu vya usiku hususan kwa wapenzi wa jinsia moja.
Na kuna hofu kwamba idadi halisi huenda ikawa ya juu, kulingana na Kituo cha Korea Kusini cha Kudhibiti Magonjwa.
Mamlaka ilianza kutoa tahadhari baada ya kuthibitisha kuwa kijana mmoja, 29, amepatikana na ugonjwa wa Covid-19 baada ya kutembelea maeneo matano ya mji wa Itaewon kati ya Mei 1 na 2
"Waathirika waliongezeka kwa haraka na kuwa tena angalizo baada ya kuathiri sio tu watu wa mji wa Itaewon, lakini pia watu wengine 30 waliobainika kupata maambukizi katika mlipuko huo wa pili," shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini limeripoti Jumatano.
Miongoni mwa waliopata maambukizi ni mwalimu wa miaka 25 wa eneo la Incheon, magharibi mwa Seoul, ambaye inaaminika alisambaza maambukizi kwa watu wengine wanane katika shule moja ya kibinafsi wakiwemo wanafunzi sita.
Na pia kijana mmoja kutoka mji mkuu wa Korea Kusini ambaye alithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona baada ya kutembelea karaoke katika huo mji wa Itaewon. Mji huu pia una historia ya kuwa makhususi kwa wapenzi wa jinsia moja.
Mashirika ya kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja yameonya kuwa unyanyapaa dhidi ya kundi hilo umeongezeka wakati wa mlipuko huo wa pili huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia na kuwa changamoto katika kudhibiti mlipuko huo.
Kulingana na idadi rasmi za serikali, maambukizi katika mji wa Seoul yalifikia 69, huku watu 14,121 wakithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona, wengi wao wakiwa ni wale walioenda vilabu usiku katika mji jirani wa Itaewon lakini pia wanatafuta wengine wengi wanaoaminika kuwa miongoni mwa walioenda vilabu ya eneo hilo.
Ingawa kuwapata watu hao bado ni changamoto kwa namna ambavyo watu wa jinsia moja huishi nchini Korea Kusini, kwasababu wanaficha taarifa zao ili wasitengwe na jamii na mara nyingi hutoa taarifa za uwongo wanapokwenda kwenye vilabu vya watu wa jinsia moja.
"Tunastahili kuwatafuta wa udi na uvumba na kuwapata haraka iwezekanavyo. Cha msingi ni kuharakisha mchakato mzima," amesema waziri mkuu Chung Sye-kyun.
Kwasababu ya mlipuko mpya, mamlaka imeamua kufunga tena baa na migahawa na kuchelesha kufunguliwa tena kwa shule kwa wiki moja.
Nini Kilichotokea?
Mamlaka ya Korea Kusini ilifungua migahawa na maeneo ya burudani kabla ya sikukuu ya kitaifa ya wiki moja mwishoni mwa Aprili.
Baa, migahawa na vilabu vya usiku katika mji wa Itaewon ilikuwa imejaa usiku wa Mei 1, pale mwanaume huyo, 29, alipotembelea maeneo hayo ambayo mengi huwa ni ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja.
Siku chache baadae, mwanaume huyo alithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona, ingawa hakuonesha dalili za ugonjwa wa Covid-19 wakati alipokuwa anajifurahisha.
Ilikuwa ni maambukizi ya kwanza ya ndani kwa ndani katika kipindi cha siku nne nchini Korea Kusini, ambayo ilikuwa imeripoti waathirika wachache tu wakati janga hilo linafikia kilele nchini humo.
Tangu wakatu huo, serikali ya Korea Kusini imekuwa ikijaribu kutafuta watu karibia 6,000 waliotembelea vilabu mbalimbali katika mji wa Itaewon alipokuwa kijana huyo.
Ili kufanikiwa, nchi hiyo inatumia rekodi ya taarifa za kadi za kufanya manunuzi, video zilizonaswa katika kamera za siri na mbinu nyengine, kulingana na vyombo vya habari vya eneo.
Kisa cha kijana huyo kilikuwa ni cha kwanza kuthibitishwa katika eneo hilo lakini haijafahamika ikiwa eneo hilo ni kitovu cha mlipuko huo wa pili, kulingana na mwandishi wa BBC nchini humo, Laura Bicker.
"Imekuwa ni mtu mmoja katika eneo moja. Lakini kumekuwa na vyanzo vingi vya maambukizi, " alisema hivyo katika mtandao wa Twitter.
Mamlaka imekuwa ikihamasisha kila mmoja aliyetembela baa au maeneo hayo ya burudani kuanzia April 24 hadi Mei 6 kupimwa na kuthibitisha ikiwa amepata virusi vya corona.
Hatahivyo, ukweli wa kwamba bado kuna unyanyapaa mkubwa dhidi ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja nchini Korea Kusini, kuna uwezekano kwamba wengine huenda wakawa na hofu ya kutembelea hospitali kwa misingi ya kutengwa na familia zao au hata kazini.
"Nimesikia kwamba baadhi ya watu hawataki kupimwa kwa hofu ya kukosolewa. Tutajitahidi kwa kila namna kuhakikisha kila mmoja anapimwa bila kuwa na hofu ya kutengwa," amesema Jeong Eun-kyeong, mkuu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Korea Kusini.
Lakini kwanini kumetokea unyanyapaa?
Baada ya kuongezeka kwa waathirka, chombo cha habari cha eneo chenye kuhusishwa na kanisa la Kievanjilisti, lilikuwa la kwamba kuhusisha mapenzi wa jinsia moja na mlipuko mpya wa virusi vya corona.
Tangu wakati huo, vyombo vingine vya habari pia navyo vimefuata mkondo na kusisitizia kwamba mwanaume aliyepatikana na maambukizi ni mpenzi wa jinsia moja na maeneo kuhoji maeneo aliyokuwa ametembelea kwa sababu ni makhususi kwa jamii ya wapenzi wa jinsia moja.
Lakini hali hiyo ilifikia kiwango kingine pale chombo cha habari cha Korea Kusini kiliposema kwamba mwanaume mwengine tena ameambukizwa ugojwa wa Covid-19 na ni mpenzi wa jinsia moja anayeishi eneo la Gangnam, mjini Seoul.
Tangu wakati huo kumekuwa na unyanyapaa dhidi ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja nchini humo, kulingana na madai ya kundi moja linalotetea haki za wapenzi wa jinsia moja.
Wakati huohuo, watu kadhaa waliokuwa kweye eneo hilo wameonyesha wasiwasi wao kwasababu ya uwezekano wa kutengwa na jamii.
"Kampuni yangu ya kadi ya manunuzi imeniambia kwamba wametoa taarifa zangu kwa mamlaka. Nahisi kwamba ninawindwa," mwanaume mmoja amezungumza na gazeti la Uingereza la The Guardian.
"Ikiwa nitapimwa, kuna uwezekano mkubwa kazini kwangu wakagundua kwamba mimi ni mpenzi wa jinsia moja. Nitafutwa kazi na kufedheheka mitaani. Nahisi kana kwamba maisha yangu yote yanakaribia kusambaratika. Sijawahi kufikiria au kuhisi kujitoa uhai siku za nyuma kama ninavyohisi sasa hivi. "