Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Muuguzi wa wagonjwa wa corona ambaye huenda akarejeshwa kwao kwa lazima.
Mahakama ya juu zaidi nchini Marekani inasikiliza kesi ambayo huenda ikaweka maelfu ya watu hasa watoto ambao waliingizwa nchini humo kinyume cha sheria na wazazi wao katika hatari ya kurejeshwa katika nchi zao.
Sheria inayofahamika kama Dreamers Act (iliyopitishwa 2012) inatoa fursa kwa watoto kama hao kufanyakazi na kusoma kama ilivyo kwa waliongia nchini Marekani kwa njia halali lakini Donald Trump anataka kubadilisha sheria hiyo.
Baadhi ya walio katika hatari ni wafanyakazi wa afya wanaokabiliana na janga la corona.
Mwanzoni mwa Aprili, foleni ya magari ya maafisa wa polisi taratibu ilionekana ikizunguka hospitali ya Winston-Salem, North Carolina, huku mweko wa buluu ukionekana kwenye mwanga wa jua.
Ilikuwa ni heshima, walisema, kwa wafanyakazi wa afya wanaohatarisha maisha yao kutibu wagonjwa wa Covid-19.
Lakini kwa Jonathan Vargas Andres, muuguzi wa chumba cha kuhudumia wagonjwa mahututi wa Covid-19 katika hospitali hiyo, anasema hayo yote yanaweza kuwa yasiyo na maana yoyote.
Amekuwa akifanyakazi katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa miaka minne pamoja na kaka yake na mke wake ambao pia ni wauguzi na wiki moja iliyopita hospitali hiyo imepokea idadi kubwa ya waathirika wa virusi vya corona.
Jonathan pia hana viza au stakabadhi zinazoonesha ameingia nchini humo kwa njia halali na katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo atajua ikiwa nchi ambayo anahatarisha maisha yake itafanya maamuzi ya kumrejesha nyumbani kwao.
"Nitajitahidi nisifikirie hilo kwasababu ninapochukua muda mrefu kufikiria suala hilo ninachoka akili," Jonathan anasema kwa sauti ya chini."
"Inatia hofu zaidi ya kitu kingine chochote."
Sheria ya Dreamers (Watoto walioingizwa bila stakabadhi kufanya kazi na kusoma)
Jonathan ni miongoni mwa wanaofaidika kutokana na sheria hiyo - ambapo utawala wa Obama kuanzia 2012 ulipitisha sheria kuruhusu wale walioingizwa nchini Marekani kinyume cha sheria wakiwa watoto na wazazi wao kusoma na kufanyakazi.
Sheria hiyo iliwaruhusu kufanyakazi na kupata kibali cha kusoma. Jonathan aliingia Marekani kutoka Mexico akiwa na miaka 12.
Mwaka 2017, Donald Trump alisitisha mpango huo na kwa sasa unapitiwa tena na mahakama ya juu zaidi nchini Marekani.
Na siku yoyote ile, Jonathan huenda akaambiwa kwamba hana haki ya kufanyakazi au kuishi nchini Marekani.
Watu karibia 800,000 wanafaidika na mpango huo wa Marekani. Washauri wa shirika la mrengo wa kushoto la Centre for American Progress, wanakadiria kwamba wahudumu wa afya 29,000 idadi inayojumuisha madaktari, wauguzi, wahudumu wa hali za dharura na wafanyakazi wengine 12,900 wapo katika maeneo mengine kwenye sekta ya afya.
Jonathan anaelezea kazi yake kama mwito. Anapenda sana kuwa muuguzi licha ya kukabiliana na janga miaka minne tu baada ya kuingia kwenye taaluma hiyo.
"Bila shaka inaogopesha unapokuwa pale ndani," anasema. "unakuwa mwoga sana na kila kitu unachoshika."
"Lakini unalazimika kusahau hilo kwa muda kwasababu uko hospitalini kusaidia wengine. Wala sio kuhusu wewe"
Hospitali yake inavifaa vya kujikinga vingi tu. Wanavitumia kwa kubania jambo ambalo linamfanya kuwa na wasiwasi, lakini kigumu zaidi. Ni kutazama watu wakifaa bila kuwa na cha kufanya.
"Inasikitisha na kufadhaisha kuona familia zikiaga wapendwa wao kupitia iPad," anasema. "Sio tu kwamba inauma lakini unachosha kihisia na kiakili."
Wakiwa hospitali wanapata ushirikiano lakini wakati mwengine anahisi kwamba anaishi kwa mashaka sana.
"Ninapokwenda kazini na kuzungumza na wafanyakaza wenzangu, hawajui kuhusu hadhi yangu ya makazi," anasema. "Lakini ninaporejea nyumbani nagundua kwamba mimi sio kama wengine."
"Hata hauna uhakika kama kile unachofanyia nchi yako kitathaminiwa. Na katika kipindi cha miezi kadhaa, huenda ukarejeshwa kwenu."
Maisha yamebadilika
Jonathan alizaliwa Mexico, katika mji mdogo karibu na Puebla, 1990.
Ingawa baba yake alikuwa dereva wa basi familia hiyo ilikumbana na changamoto nyingi.
Anakumbuka nyumba walioishi, haikuwa na madirisha wala maji na sakafu ilikuwa chafu.
Mara ya kwanza baba yake kwenda Marekani ilikuwa mwaka 2000, na miaka miwili baadaye, akapeleka familia yake.
Pamoja na kaka yake na mama yake, walivuka mto unaotenganisha Mexico na Marekani na kutembea jangwani kabla ya kuingia Marekani bila vibali.
Hadi mwaka 2012, familia hiyo iliishi kwa kubahatisha tu. Kama watoto ambao waliingia nchini humo bila vibali wangeweza kwenda shule ya umma lakini sio chuo kikuu cha umma na vyuo vikuu vya kibinafsi vilikuwa ghali mno.
Alipomaliza shule ya upili alifanya kazi za mkono. Alikuwa akiunganisha matairi katika duka moja wakati mpango wa Daca ulipotangazwa.
"Ulibadilisha maisha yangu," anasema. "Sijui namna ya kuelezea. Kufahamu kwamba nitapa fursa ya kufanyakazi kihalali na uwezekano wa kwenda chuo kikuu."
Wakati huo, alikuwa ameishi Marekani kwa miaka 10 na ingawa alikuwa anajihisi kama raia wa Marekani, hakuwa na makaratasi ya kuthibitisha hilo.
Mpango wa Daca ulipoanza yeye pamoja na kaka yake walijisajili kujiunga na jeshi lakini wakakataliwa kwasababu ya hadhi yao ya makazi.
Lakini hamu ya kutaka kuhudumia wengine ikawafanya kugeukia uuguzi.
"Rejea nchini mwako upande wa pili wa mto"
Ingawa anapenda kufanyakazi, miaka minne iliyopita imekuwa ya hofu sana kwake.
Jonathan ameanza kula taya ya meno anapolala. Wakati mwengine hilo hutokea kiasi cha meno kuanza kufura na inauma sana. Ni hali inayomkuta mtu kwasababu ya msongo wa mawazo.
"Nimekuwa na msongo wa mawazo tangu 2015, pale rais Donald Trump alipotangaza kwamba anawania urais na kitu cha kwanza alichofanya kilikuwa ni kushambulia wahamiaji kutoka Mexico."
"Hilo lilikuwa rasmi alipoingia madarakani."
Tangu wakati huo, anasema amekuwa akihisi kuwa na uhasama naye na pia ameshuhudia ubaguzi wa hali ya juu. Anaamini baadhi ya watu kwa sasa wanajiona kuwa na ushupavu wa kubagua wengine.
Anaelezea tukio lililotokea nje ya eneo la kufanya mazoezi kabla ya hatua ya kusalia ndani ambapo mwanaume mmoja alimpigia makelele kwa kusema meneno ya kibaguzi na kumuarifu kwamba arejee nchini mwake upande wa pili ya mto kwasababu aliegesha gari vibaya.
Mahakama ya juu zaidi nchini Marekani inasikiliza kesi ambayo huenda ikaweka maelfu ya watu hasa watoto ambao waliingizwa nchini humo kinyume cha sheria na wazazi wao katika hatari ya kurejeshwa katika nchi zao.