Je ni kwanini sukari imeadimika Tanzania?

Takwimu raasmi za serikali ya nchi hiyo zinaonesha kuwa kwa mwaka 2019/2020 mahitaji ya sukari yanakadiriwa kuwa tani 710,000 kati ya hizo tani 545,000 ni kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani na tani 165,000 ni kwa mahitaji ya viwandani.
Iliyochapishwa

Kwa wananchi wa maeneo mengi ya Tanzania, sukari imekuwa ni bidhaa ghali na adimu.

Kilo moja ya sukari kwa bei ya kawaida huuzwa kwa wastani wa shilingi 2,500 za Tanzania (takribani $1) lakini katika wiki za hivi karibuni bei hiyo imepaa mpaka kufikia shilingi 5,000 (takribani $2) katika baadhi ya maeneo.

Upatikanaji wake pia umekuwa wa shida, huku "hakuna sukari" ikiwa ni jibu ambalo limekuwa la kawaida katika maduka mengi ya rejareja jijini Dar es Salaam.

Maswali ya wapi sukari inapatikana na kwa kiasi gani yamekuwa ni moja ya mada kubwa mitandaoni nchini Tanzania.

Serikali ya Tanzania hata hivyo, inalaumu baadhi ya wafanyabiashara kuwa wanatengeneza uhaba huo kwa makusudi ili wailangue kwa wanunuzi kwa bei ya juu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mnamo Aprili 22 aliagiza Wakuu wa Mikoa nchini humo kuwakamata wafanyabiashara wote ambao wamekuwa wakiuza sukari kwa bei ya shilingi 4,500 ambayo ndiyo ilikuwa ya juu zaidi kwa wakati huo.

Majaliwa alisisitiza kuwa nchi hiyo haina uhaba wa sukari, msimamo wa kutokuwa na uhaba pia umetolewa na waziri wa Viwanda na Biashara Bwana Innocent Bashungwa. Waziri Bashungwa kupitia ukurasa wake wa Twitter alidokeza kuwa maafisa wa Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na maafisa wa vyombo vya ulinzi.

Je, kama hakuna uhaba wa sukari kwa nini nchini humo kwa nini bidhaa hiyo imeadimika. Kuna mambo kadhaa ambayo yanaelezea hali ilivyo kwa sasa Tanzania nayo ni:

Uwiano wa uzalishaji wa ndani dhidi ya mahitaji

Nchini Tanzania kuna viwanda vikubwa vinne vya sukari, viwili vikiwa mkoani Morogoro, mkonai Kilimanjaro kimoja na Kagera kimoja. Pia kuna kiwanda kimoja cha kati kilichopo mkoani Manyara.

Takwimu raasmi za serikali ya nchi hiyo zinaonesha kuwa kwa mwaka 2019/2020 mahitaji ya sukari yanakadiriwa kuwa tani 710,000 kati ya hizo tani 545,000 ni kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani na tani 165,000 ni kwa mahitaji ya viwandani.

Gazeti la serikali la Habari Leo nchini Tanzania mwezi Novemba lilimnukuu Katibu katika wizara ya viwanda Profesa Joseph Buchwashaija akisema kuwa uwezo wa uzalishaji wa viwanda vilivyopo Tanzania kwa mahitaji ya kawaida ya nyumbani ni tani 378,449 ambayo ni sawa na asilimia 67.7 ya mahitaji.

ni viwanda vikubwa vinne tu ambavyo vinaruhusiwa kuagiza sukari kutoka nje ya Tanzania ili kuzui pengo la uzalishaji wao.
Maelezo ya picha, ni viwanda vikubwa vinne tu ambavyo vinaruhusiwa kuagiza sukari kutoka nje ya Tanzania ili kuzui pengo la uzalishaji wao.

Waziri wa Kilimo wa Tanzania Japhet Hasunga hii leo ameliambia Binge la nchi hiyo kuwa, mpaka kufikia mwezi Aprili,2020 uzalishaji wa sukari nchini humo ulifikia tani 298,948 ambayo ni sawa na asilimia 86 ya lengo.

Ili kuziba nakisi ya mahitajikuna utaratibu maalumu wa kuagiza kutoka nje bidhaa hiyo ambao Tanzania inautumia.

Mfumo wa uagizaji nje wa sukari

Kwa sasa ni viwanda vikubwa vinne tu ambavyo vinaruhusiwa kuagiza sukari kutoka nje ya Tanzania ili kuzui pengo la uzalishaji wao.

Waziri Hasunga ameliambia Bunge kuwa mwezi Machi serikali ilitoa kibali kwa vimanda hivyo, Kilombero, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na TPC Moshi kuagiza tani 40,000 nje ya Tanzania.

"…Katika kikao cha pamoja na wawakilishi wa wazalishaji, serikali, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na Bodi ya Sukari kilichokaa chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tulikubaliana bei ya sukari haitapanda kwa kuwa gharama zilikuwa chini.," ameeleza Hasunga.

Hasunga hata hivyo amesema kuwa kumekuwa na ufichwaji wa sukari na badhi ya wafanyabiashara licha ya serikali kutoa bei elekezi ya bidhaa hiyo.

Pia amesema kuwa mlipuko wa janga la corona umesababisha kuchelewa kwa kuingia sukari iliyoagizwa na kuwa baadhi ya meli zilizobeba shehena hiyo kufaulisha kwenye meli nyengine na kuchelewesha kufika.

Ameliambia bunge kuwa, kufikia sasa tayari tani 4,000 zimeshawasili Tanzania na kuanza kusambazwa huku tani nyengine 21, zikitarajiwa kuingia nchini humo mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Mei.

Mfumo huu wa Tanzania kuwatumia wazalishaji wa ndani kuagiza sukari kutoka nje umetokana na mabadiliko yaliyofanywa mwanzoni mwa utawala wa rais John Pombe Magufuli.

Mwezi Januari 2016, Rais Magufuli aliagiza kuwa vibali vyote vya kuagiza sukari vitolewe na Ikulu baada ya kuwa na malamiko juu ya mfumo ambao uliruhusu wafanyabiashara kuingiza sukari nchini humo.

Walalamikaji wakuu walikuwa ni viwanda vya ndani wakidai wafanyabiashara walikuwa wakiingiza sukari na kuiuza bei ya chini na kufanya soko la viwanda vya ndani kuwa gumu.

Pia kulikuwa na malamiko kuhusiana na ubora wa sukari zinazoingizwa, baadhi zikidaiwa kuwa ni za viwandani ambazo hazikufaa kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani.

Mwishowe serikali ikaja na mfumo wa kuviruhusu viwanda vya ndani kuagiza wenyewe sukari nje ili kudhibiti malalamiko ya 'kuharibiwa soko'.

Uhaba kipindi cha masika

Kwa nini sukari imeadimika tanzania?

Uhaba mkubwa wa sukari pia ulitokea kipindi kama hiki mwaka 2016. Kipindi ambacho sehemu kubwa ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla inapitia katika mvua kubwa za masika.

Kutokana na mvua hizo mashamba ya miwa ambayo yanazunguka viwanda hivyo hujaa maji na uzalishaji huwa ni mgumu.

Hivyo imekuwa ni ada kwa viwanda vya sukari nchini Tanzania kusitisha uzalishaji katika kipindi cha mwezi Machi mpaka Mei. Katika kipindi hicho cha kupisha mvua kubwa viwanda hivyo pia hutumia fursa ya kusimama kwa uzalishaji kutengeneza ama kurekebisha mashine zao.

Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea mpaka sasa, waziri Hasunga hii leo ameliambia Bunge pia kuwa ni kiwanda kimoja tu ambacho kimeonesha kuwa kipo tayari kwa ajili ya kurejea katika uzalishaji kufikia mwishoni mwa mwezi huu. Hata hivyo hakukitaja kiwanda hicho.