Virusi vya corona: Je magari yenye huduma za 'kukabiliana' na corona China ni 'njama'?

Chanzo cha picha, Getty Images
Watengenezaji magari nchini China wanaangazia wasiwasi wa kiafya kupitia uzinduzi wa magari ambayo yana huduma za kukabiliana na virusi vya virusi.
Magari hayo mapya yanatoa ulinzi sawa na ule wa mtu aliyevaa barakoa mmiliki anapoingia ndani yake.
Baadhi ya makampuni makubwa ya magari yamezindua magari mapya yenye huduma hiyo ikiwemo kampuni ya Geely inayotengeneza magari aina ya black Cabs mjini London.
Biashara ya magari nchini China ilishuka katika robo ya kwanza ya mwaka huku kukiwa na amri ya kutotoka nje kukabiliana na virusi vya corona.
Geely ilikuwa kampuni ya kwanza ya kutengeneza magari kuzindua magari yanye huduma ya kukabiliana na virusi, ikiimarisha kazi yake ya hapo awali ili kuvutia wamiliki wa magari walio na wasiwasi na mazingira mabaya ya hewa chafu katika miji mikuu.
Mradi wake wa magari ya kulinda afya unalenga kuzuia vipande vidogovidogo kuingia ndani ya gari hivyobasi kuwalinda madereva na abiria dhidi ya vitu vyenye madhara.
Geely pia inatengeneza huduma inayozuia bakteria ili vifaa vinavyotumika kuendesha magari pamoja na milango yake kutovutia bakteria na virusi.
''Wateja hutumia wakati mwingi katika magari yao, sawa na 'nyumbani kwao'. Ni kupitia utengenezaji wa bidhaa bora za kiafya ndiposa tunaweza kuafikia mahitaji ya wateja wetu'', alisema msemaji wa kampuni ya Geely.
Utengenezaji wa vifaa vya kulinda afya ya madereva na abiria wao utakuwa mojawapo ya malengo yake ya muda mrefu.
Ili kutokaribiana moja kwa moja na mteja anaponunua gari, kampuni ya Geely inatumia ndege zisizo na rubani kuwapelekea funguo za magari yao wateja hao.
Kampuni ya SAIC inayomiliki kampuni ya magari ya Uingereza MG , imeongezea kifaa mbadala cha taa inayotumika kama chujio ili kusafisha hewa inayotumika katika mfumo wa baridi wa gari hilo.
Kampuni pinzani ya Guangzhou Automobile kwa jina GAC , nayo imezindua mfumo mzima wa kichungi cha hewa miongoni mwa magari yake mengi.
Kampuni ya utafiti kwa jina Frost & Sulivan inafikiria kwamba mikakati hiyo mipya ni njama za kuvutia wateja.
''Ni wazi kwamba kila mtu anajaribu kuweka huduma ya kulinda afya katika magari yao. Vifaa hivi vilikuwa tayari vikitarajiwa lakini Covid-19 imetoa mshawasha mpya'', alisema Vivek Vaidya, mtaalamu wa magari katika kampuni ya Frost & Sullivan.
Sio tu kwamba huduma kama hizi huangazia masuala ya usafi na yale ya kiafya bali zinaweza kutoa tofauti kubwa miongoni mwa bidhaa. Haya hayatakuwa malengo ya China pekee bali ulimwengu mzima.
Madai ya 'njama'
Hatahivyo, Shaun Rein, ambaye ni mkurugenzi katika soko la utafiti nchini China , anapinga: Makampuni yanajaribu kuitumia fursa ya hofu ya corona ili kuuza bidhaa na huduma zao kwa wateja ili kupata malipo".
Mwaka 2015, Tesla iliuza magari yaliokuwa na mfumo wa kupambana na uchafuzi wa mazingira ambao ulipata umaarufu mkubwa nchini China. Mfumo huo uliwalenga wateja waliokuwa na wasiwasi kuhusu hali ya mazingiraya hewa chafu katika miji mikubwa.
''Watengenezaji magari sasa wanajaribu kufanya magari yao kuwa salama dhidi ya virusi. Mimi sio daktari ama mwanasayansi, lakini nawaonya wateja kuchukua tahadhari dhidi ya kampuni yoyote inayosema kwamba bidhaa zake zinapunguza maambukizi ya virusi , hususan vile vya Covid-19'', alisema bwana Rein.
Mapema mwezi huu kampuni moja ya rangi kwa jina Nippon ilisema kwamba imetengeneza rangi yenye uwezo wa kukabiliana na virusi ili kuwalinda wateja kupata maambukizi katika sakafu, ijapokuwa haikuweza kuteja ni aina gani ya virusi.
Kampuni hiyo ya Japan ilisema kwamba rangi hiyo inayowakinga wateja dhidi ya virusi inalenga kutumika katika mahospitali na ilizipa hospitali nne mjini Wuhan, kitovu cha mlipuko wa virusi vya corona.
Hatua hiyo inajiri wakati ambapo mauzo ya kampuni za magari nchini China yameshuka kwa zaidi ya asilimi 80 mwezi Februari , ikiwa ndio mauzo ya chini zaidi katika kipindi cha miaka 20.
Bei kupanda
Huku mauzo ya magari mwezi Machi yakionyesha kupanda kiasi, yalikuwa yameshuka kwa asilimia 43 ikilinganishwa na mauzo ya mwezi kama huo mwaka uliopita.
Takwimu za mwezi Aprili zinaweza kuonyesha kuimarika kwa mauzo huku watu wakirudi kazini lakini wakiwa na wasiwasi kuhusu usafiri wa umma.
Huku mashrti ya kutokaribiana na karantini yakiwa katika fikra zetu, inaeleweka kwamba watu watafanya makosa wakati wanachukua tahadhari na wangependelea kusafiri kwa kutumia magari yao wenyewe badala ya usafiri wa umma.
''Hatua hiyo itaongeza mahitaji ya magari'' ,alisema Gianfranco Casati, afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya ukuaji wa soko la Accenture.
Serikali ya China pia imekuwa ikisaidia katika kuimarisha mauzo ya magari
''Washauri wetu wanasema kwamba itachukua hadi miaka mitatu kwa biashara ya magari kurudia kiwango chake cha mauzo kabla ya mlipuko wa virusi vya corona'', aliongezea bwana Vaidya.













