Virusi vya corona: Trump amesema chanjo itakuwa tayari mwaka huu

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba ana matumaini kuwa Marekani itapata chanjo ya vurusi vya corona kabla ya 2021.
"Tuna uhakika kwamba tutapata chanjo kufikia mwisho wa mwaka huu," amesema wakati wa mazungumzo na kituo cha habari cha Fox News.
Hata hivyo alisema kwamba atakuwa ni mwenye furaha iwapo nchi nyengine itaipiku Marekani katika utafiti, na kuongeza: ''Sijali. Ninachotaka nikupata chanjo tu inayofanya kazi"
Wataalamu wengi wanasema huenda chanjo hiyo ikachukua miezi 12 hadi 18 kuwa tayari.
Wanasayansi kote duniani kwasasa wanajitahiji kutengeneza chanjo lakini wataalamu wengi wanatarajia kwamba itakuwa tayari sokoni kwa halaiki ya watu ifikapo 2021.
Trump alionekana kuwa na matumaini zaidi kuliko washauri kwa makadario ya ni lini dawa hiyo inaweza kupatikana kwa mara ya kwanza.


Wakati huohuo, Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo, awali alisema kulikuwa na ushahidi kwamba virusi hivyo vimetoka China. Lakini hakukanusha taarifa ya kijasusi iliyosema kwamba virusi hivyo sio vya kutengenezwa na mwanadamu.
Mpaka kufikia sasa idadi ya waliokufa duniani ni karibia 250,000, huku wengine milioni 3.5 wakithibitishwa kuambukizwa kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Trump aonya kuwa idadi ya vifo kwasababu ya corona huenda ikafika 100,000

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kwamba huenda watu zaidi ya 100,000 wakapoteza maisha kwasababu ya virusi vya corona nchini Marekani.
Akizungumza kwa njia ya mtandao, Bwana Trump pia alikanusha kwamba utawala wake umechukua hatua za kukabiliana na virusi vya corona kwa mwendo wa kobe.
Zaidi ya watu 67,000 wamekufa kwasababu ya Covid-19 nchini Marekani.
Miongoni mwa watalaamu wanaopingana na imani ya Trump ni Dkt. Anthony Fauci, mtaalamu wa hali ya juu wa magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani na afisa mkuu wa matibabu Uingereza Chris Whitty.
Dr Fauci aliwahi kusema chanjo itachukua miezi 18 kupatikana huku Profesa Whitty, mwezi uliopita alisema uwezekano wa kupata chanjo imara au tiba ndani ya mwaka ujao ni mdogo mno.
Rais Trump pia alikanusha madai kwamba utawala wake umeshindwa kuchukua hatua kwa haraka mwanzoni mwa mlipuko na kusema: "Tulifanya kilichokuwa sahihi."
Badala yake ameshutumu China kwa kushindwa kusitisha usambaaji wa virusi vya corona: "Kwa mtazamo wangu walifanya makosa makubwa na hawakutaka kukubali ukweli. Tulitaka kwenda kuwasaidia lakini wao hawakutaka sisi twende kwao."
Bwana Trump pia alitupia kidole cha lawama maafisa wa kijasusi na kuwashtumu kwa kushindwa kusema lolote kuhusu mlipuko huo hadi Januari 23.












