Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Imani za kidini zinasaidia au zinadidimiza mapambano dhidi ya corona?
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Katikati ya mwezi Machi mwaka huu nchi ya Malaysia ilifunga shule, ofisi na sehemu za ibada katika juhudi za kupambana na kuenea kwa virusi vya corona, baada ya kubaini mikusanyiko katika misikiti ilichangia pakubwa mlipuko wa ugonjwa huo.
Mikusanyiko ya kidini imechangia pia kuenea kwa corona katika nchi ya Pakistan, India, Iran, Brunei na mataifa mengine kadhaa.
Fauka ya hilo, baadhi ya viongozi wa kidini wameonesha kukinzana na ukweli wa mambo kuhusu corona.
Askofu Gerald Glenn, katika jimbo la Virginia nchini Marekani alifariki kwa virusi vya corona baada ya kupuuza tahadhari za wataalamu wa afya na kuapa kutofunga kanisa lake.
Afrika pia haijasalimika na misigano ya viongozi wa kidini na uhalisia wa mambo. Hadi mwishoni mwa mwezi Machi, zaidi ya Wachungaji 20 wa makanisa walikamatwa nchini Uganda kwa kupotosha kuhusu corona.
Akiwemo Mchungaji maarufu Augustine Yiga wa kanisa la Revival, Kampala. Miongoni mwa Wachungaji hao wapo waliowaambia waumini wao kwamba wanayo dawa ya corona, baadhi walisema hakuna corona Afrika ama Waafrika hawaathiriki na ugonjwa huo.
Nchini Kenya, maafisa wa usalama wameendesha operesheni kadhaa zilizofanikisha kuwakamata waumini wabishi waliokuwa wakiendesha ibada za mikusanyikoa katika makanisa hata baada serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufu mikusanyiko.
Tanzania bado mikusanyiko ya kiimani kwa Waislamu na Wakristo inaendelea kufanyika hadi sasa katika baadhi ya misikiti na makanisa, wakati ambapo visa vya maambukizi ya ndani vinazidi kuongezeka.
Ni misikiti michache na madhehebu machache ya Kikristo yaliyokubali kuzifunga nyumba za ibada, lakini mingi ya milango ya nyumba hizo bado iko wazi mchana na usiku.
Swali muhimu linalozuka katika mazingira haya ni hili; misimamo hii ya kiimani inayohusishwa na dini, ikiwemo kukusanyika au viongozi wa dini kutoa kauli za utata na kupotosha, yanasaidia katika juhudi za kupambana na corona au yanahatarisha kukuwa kwa janga hili?
Padri wa Kanisa Katoliki na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, Leon Maziku anasema, "huwezi kuwa na dini zinazovunja sheria, dini zina haki ya kuabudu na zina wajibu wa kutii sheria za nchi".
Maelfu ya watu wameambukizwa duniani kote na mamia wamefariki. Katika mataifa mengi ya Afrika, ugonjwa wa corona uko katika hatua za awali.
Viongozi wa kidini na waumini hawapaswi kuzifanya imani zao kuwa kizingiti katika mapambano haya.
Hili ni janga linaloweza kumpata yeyote akiwa na umri wowote, bila kujali aina ya Mungu anayemuabudu au nyumba ya ibada anayoingia.
Imefika wakati wa kukubaliana na ushauri wa wataalamu wa afya kuhusu hatari ya mikusanyiko isiyo salama. Mengi ya maambukizi ya sasa hayasababishwi tena na wageni kutoka nje, ni raia wa ndani wao kwa wao wanaambukizana.
Kila mmoja anapaswa kuwa na matumizi tu sahihi ya akili, kuelewa ya kuwa mikusanyiko ni hatari na haipaswi kuendelea kuwepo, si lazima kusubiri bakora za Polisi.
Padri Maziku anatofautiana kabisa na viongozi wa dini wanaojihalalishia kukusanya waumini wakati huu wa corona katika nchi ambazo zimeshapiga marufuku mikusanyiko, "kama nchi inasema hairuhusu mikusanyiko, si halali kiongozi wa dini kusema sisi tunamsikiliza Mungu na hatusikilizi serikali".
Viongozi wa dini wana nafasi zote mbili, kati ya kuhuisha mapambano dhidi ya corona au kuyadidimiza. Kufunga sehemu za ibada katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kuwasisitiza waumini wasikilize serikali na wataalamu wa afya, huko ni kutia nguvu juhudi za kupambana na corona.
Au kinyume chake, kuendesha ibada za mikusanyiko kwa siri, kufanya ukaidi na kuwapa waumini matumaini hewa yasiyo na ushahidi wala uhakika wa kufanikiwa, huko ni kudidimza juhudi za kupambana na corona.
Janga lisilo na tiba linazidi kutapakaa, hakuna mtaalamu wa afya wala serikali yoyote duniani iliyothibitisha na kutoa shaka ya kuwa mikusanyiko ya kidini ni salama dhidi ya kuenea kwa janga hili. Kimsingi sio salama katika namna yoyote ile, kama ambavyo sio salama mikusanyiko mengine yote.
Ikumbukwe, moja ya vitendo vilivyochangia kuenea kwa virusi vya Ebola katika nchi za Afrika ya Magharibi na DR Congo, ni watu kuacha ushauri wa wataalamu wa afya na kuchukua hatua zilizochangia familia kuambukizana.
Kuliripotiwa matukio mengi ya familia kupeleka wagonjwa wa Ebola bila ya tahadhari katika makanisa kuombewa na kwa waganga wa kienyeji kuliko kuwapeleka hospitali.
Ni vitendo vya kiimani vilivyochangia Ebola kuenea, ikasababisha maelfu ya watu kupoteza maisha. Kosa lililofanyika ni kushindwa kuchora mstari wa mpaka kati ya imani kwa viongozi wa kidini na waganga wa kienyeji na ule uhalisia wa mambo kama ulivyoelezwa na wataalamu wa afya.
Kosa ambalo halipaswi kurudiwa wakati huu wa corona.
Mwanazuoni wa Kiislamu na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Tanzania, Sheikh Abdi Kassim Jiba anasema, "kwa sheria za Kiislamu inawezekana watu kuswali nyumbani wakati wa janga kama la corona. Uislamu haujakataza watu kuswali nyumbani ikibidi. Ndio maana misikiti ya Makka na Madina ikafungwa".
Tukumbuke corona inaenezwa kwa njia ya hewa na kugusana, dalili za ugonjwa zinachukua siku kadhaa hadi mwathirika atakapo jisikia sasa ni mgonjwa, mikusanyiko ya aina yoyote inatoa nafasi ya wazi watu kuambukizana bila kujijua.
Hatupaswi kusahau, Afrika ni bara ambalo mataifa yake yana huduma duni za afya. Tafsiri yake ni; watu wa bara hili ndio wanaotakiwa kuchukua tahadhari zaidi wakijua kuwa hospitali zao hazina uwezo wa kutosha kuwahudumia ikiwa maambukizi yatakuwa makubwa.
Sisitizo muhimu kwa wakati huu ni lilelile, chukua tahadhari zinazoshauriwa na wataalamu wa afya, na acha kuelekeza masikio katika mambo yasiyo na uhakika wala ushahidi katika kufanikiwa kwake, kufanya kinyume ni kuhatarisha afya yako na za wengine.
Hapa sina maana ya kusema hata yale maombi yasiyo hatarishi hayafai, dunia hii kila mtu na imani yake. Yasiyofaa ni yale matendo na kauli zinazohusishwa na imani ambazo huhatarisha au kurudisha nyuma juhudi za kukabiliana na corona. Ikiwemo mikusanyiko na kauli za kupotosha.
Dini zina mafundisho mazuri ambayo yanaweza kusaidia pakubwa mapambano haya. Sheikh Jiba anasema, "katika uwanja wa afya, Uislamu umezungumzia kuhusu majanga ya kuambukiza, umeeleza ya kuwa usiende katika sehemu yenye maradhi wala usitoke kukimbia".
Rashid Abdallah ni mwandishi wa habari katika jiji la Dar es Salaam na mchambuzi wa siasa na migogoro ya Afrika.