Virusi vya corona: Tanzania yatangaza wagonjwa 7 wapya kisiwani Zanzibar

Wizara ya Afya kisiwani Zanzibar imetangaza wagonjwa saba wapya wa virusi vya corona .
Tangazo hilo linafanya idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona waliothibitishwa kisiwani Zanzibar kufikia 105 na jumla ya 306 nchini Tanzania.
Kulingana na taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari wagonjwa wote wapya ni raia wa Tanzania.

Hatua hiyo inamaanisha kwamba maambukizi yanayozidi ni yale ya wenyewe kwa wenyewe.

Aidha taarifa hiyo iliotiwa saini na waziri wa Afya kisiwani humo imesema kwamba wagonjwa 36 wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya dalili zao za mardhi ikiwemo homa, kikohozi, kifua kubana na kuumwa na kichwa kuisha.
Vile vile taarifa hiyo imesisitiza kwamba wagonjwa wote hao wameshauriwa kusalia katika nyumba zao kwa muda wa siku 14 huku wataalam wa afya wakiendelea kuwafuatilia kwa karibu kabla ya kuruhusiwa kurudi katika shughuli zao za kawaida.
Wakati huohuo serikali kupitia wizara ya Afya , inaendelea kuwasisitiza wananchi ambao wana dalili za homa kali, kukohoa na kupiga chafya kujitokeza katika vituo vya Afya au kupiga simu nambari 190.
Vilevile vyombo vya habari vimetakiwa kupata taarifa za ugonjwa huo kutoka kwa wizara ya Afya.
Mji wa Dar es Salaam umetangazwa kuripoti wagonjwa wengi wa virusi vya corona ikilinganishwa na miji mengine nchini Tanzania.

Msimamo wa serikali ni upi?
Jumatano iliopita, rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliweka wazi kuwa serikali yake haitalifungia jiji la Dar es Salaam.
Licha ya Dar es Salaam kuwa kitovu cha maambukizi, Magufuli amesema jiji hilo la watu milioni sita ndio moyo wa mapato ya Tanzania.
"Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam, hili haliwezekani. Dar es salam ndio centre (sehemu) pekee ambapo collection (makusanyo) ya revenue (mapato) inapatikana kwa nchi yetu...Zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanakusanywa Dar es Salaam," alisema Magufuli alipokutana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo Jumatano.
Pia alisisitiza kuwa kutokana na wingi wa wakaazi wake, ilikuwa ni jambo la kutegemewa kitakwimu kwa jiji hilo kuwa na wagonjwa wengi zaidi.
Awali mapema siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Kassim Majaliwa akiongea kwenye ibada ya kuiombea nchi alisema anatambua kwamba kuna Watanzania ambao wanataka serikali ichukue hatua nyingi zaidi kudhibiti maambukizi ya virusi, lakini ameonya kuwa kila hatua ina faida na hasara zake.
"Ni vyema wajue kila hatua ina faida na hasara zake...Serikali inaendelea kutathmini kila hatua kwa faida na hasara zake kwa jamii. Ni vyema Watanzania mkaendelea kuiamini serikali, kuwaamini wataalamu wetu katika kuchukua hatua ambazo haziwezi kuleta athari zaidi kwa taifa."
Hatua zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi ni zipi?
- Shule zote na vyuo vya elimu vimefungwa mpaka itakapotangazwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini humo.
- Pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
- Magari ya usafiri wa umma hatayakiwi kujaza abiria, na wote lazima wawe wameketi vitini.
- Ndege za abiria zimezuiwa kutua nchini humo.
- Kuanzia Jumatatu ya Aprili 20 ni lazima kwa wakaazi wote wa Dar es Salaam kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya umma.
- Biashara zote za chakula jijini Dar es Salaam zinatakiwa kufunga bidhaa zao na kutoruhusu watu kula kwenye migahawa.












