Virusi vya corona: Je maiti ya mgonjwa wa corona inaweza kusambaza virusi hivyo?

Iliyochapishwa

Mji wa Ecuador wa Guayiquil ulikumbwa na hali mbaya wakati wa mgogoro wa mazishi uliotokea katikati ya mwezi Machi.

Picha za makumi ya majeneza na miili ilioonekana barabarani kutokana na ukosefu wa fursa za kuwazika zilionyesha sura mbaya zaidi za mlipuko wa virusi vya corona duniani.

Mbali na kuanguka kwa mfumo wote wa afya katika mkoa wa Guaya, ulioathirika zaidi na ugonjwa huo nchini Ecuador, tatizo jingine lilikuwa lile la hofu ya kugusa maiti.

Ecuador ilithibitisha zaidi ya vifo 6,700 katika kipindi cha siku 15 katika eneo la Guaya.

Mlipuko huo wa vifo nchini Ecuador unaelezea kile kinachoendelea katika mataifa mengine ya America ya kusini.

'' kulikuwa hakuna udhibiti. Hofu ilisababisha vyumba vingi vya kuhifadhi maiti kufungwa kulingana na rais wa shirika la wakurugenzi wa maziko'', aliezungumza na BBC.

''Ukweli ni kwamba Ecuador iko nyuma katika mfumo wa mazishi na haina maelekezo yoyote kutoka kwa serikali kukabiliana na tatizo kama hilo'', alisema kiongozi huyo mwenye kundi la vyumba zaidi ya 700 vya kuhifadhia maiti nchini humo.

Wasiwasi kuhusu kile cha kufanya na jinsi ya kushughulikia miili ya waliofariki kutokana na gonjwa la Covid 19, ama hata wagonjwa wenye dalili uliongezeka katika taifa hilo la America ya kusini.

Katika mji wa Mexico, mabaraza ya miji yalitoa mapendekezo yao kutofanya mazishi ama hata kufanya upasuaji huku usafirishaji wa miili nje ya mji ukizuiliwa.

Baadhi ya wakaazi waliandamana kuzuia kuzikwa kwa waathiriwa wa ugonjwa huo kulingana na chombo cha habari cha Reuters.

Lakini je miili ya watu waliokufa kutokana na virusi inaweza kusambaza ugonjwa? je mazishi yanaweza kufanyika na je wanapaswa kuchomwa ama kuzikwa? Tunaangazia masuala haya.

Maambukizi yanaweza kuzuiliwa

Iwapo uangalifu wa makini utatekelezwa na ushikaji wa miili hiyo kufanywa kwa makini, hakuna sababu ya kuogopa kwamba mtu anaweza kuambukizwa Covid 19 kulingana na shirika la Afya duniani WHO katika muongozo wake kwa BBC Mundo.

''Isipokuwa katika visa vya magonjwa kama vile Ebola na homa ya Marburg'', kulingana na WHO.

Ni mapafu ya mtu aliyefariki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Influenza ambayo yanaweza kusababisha maambukizi iwapo mfu hakushikkwa kwa makini wakati wa upasuaji, lakini maiti haziwezi kusambaza ugonjwa, liliongezea shirika hilo.

Hiyo haimaanishi kwamba virusi hivyo vimekufa na mwathiriwa, kwasababu katika wagonjwa walio na tatizo kubwa la mapafu, mapafu hayo na viungo vingine vinaweza kuwa na virusi hivyo vilivyo hai.

lakini virusi hivyo vinaweza kutolewa wakati wa upasuaji wa maiti kwa kutumia misumeno ya stima ama uoshaji wa ndani unaotekelezwa na wafanyakazi wa vyumba vya kuhifadhia maiti.

Watu wa uhusiano wa karibu na wapendwa wa mwathiriwa wa Covid 19 wanapaswa kusubiri wataalam waliopata mafunzo na waliovalia nguo za kujilinda dhidi ya virusi hivyo ili kuweza kumuandaa mpendwa wao kwa mazishi ama kuchomwa.

Je kunaweza kuwa na mazishi?

WHO haikatazi kwamba mazishi yafanyike, lakini inataka yafanyike na tahadhari kubwa. Iwapo familia inataka kuuona mwili , bila kuushika , wanaweza kufanya hivyo iwapo watachukua tahadhari zinazohitajika hususan usafi wa mikono.

familia zinapaswa kupewa maelekezo ya kutoshika mwili na kuubusu, kulingana na shirika hilo.

Mbali na hayo wanapaswa kuendelea kutekeleza masharti ya kutokaribiana na watu wengine na uoshaji wa mikono wa mara kwa mara.

Hatahivyo hairuhusiwi kwa watu wazee na wale walio na kinga zilizodhoofu kukaribiana moja kwa moja na mwili wa mtu aliyeaga dunia kutokana na virusi vya corona.

Je maiti hao wanafaa kuzikwa ama kuchomwa?

Chaguo la kuwazika ama kuwachoma waathiriwa litategemea uamuzi wa familia yake.

Kuna madai kwamba watu wanaofariki kutokana na ugonjwa unaoweza kusambazwa kupitia hewa wanapaswa kuchomwa lakini hilo sio kweli, inasema WHO.

Wale wanaopaswa kuwa na nguo za kujilinda katika mazishi ndio watu wanaoruhusiwa kuuzika mwili huo kaburini.

Katika maeneo ambayo hayana ibada za mazishi ama ni tamaduni zinazopaswa kuandaa mazishi mtu anayeyasimamia anapaswa kujilinda.

Mtu huyo anapaswa kuvalia glavu, kujilinda macho, kuvaa barakoa, kuosha mikono na nguo baada ya kumaliza shughuli hiyo kulingana na WHO.

Sio lazima kutupa mali ama nguo za mwathiriwa, lakini tahadhari kama vile kushika vitu hivyo na glavu na kuviosha na sabuni mbali na kuvinyunyizia dawa za kuuwa vidudu zinapaswa kuchukuliwa.