Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Marekani yaipiku Italia kwa idadi ya vifo duniani
Idadi ya waliokufa kwa virusi vya corona nchin Marekani kwa sasa ipo juu zaidi duniani baada ya kupita idadi ya nchini Italia.
Data za hivi karibuni kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins zinaonesha kwamba zaidi ya watu 20,000 nchini Marekani wamekufa kutokana na janga la corona.
Taarifa hizo zinawadia muda mfupi baada ya kubainika kwamba Marekani ndio nchi ya kwanza kurekodi vifo vya watu zaidi ya 2,000 kwa siku moja.
Gavana wa New York Andrew Cuomo amesema Jumamosi kwamba vifo hivyo vinaendelea kudhibitiwa.
Ndani ya saa 24 alitangaza vifo vipya 783, na kusema kwamba siku kadhaa zilizopita jimbo hilo limeshuhudia idadi ya vifo karibu na hiyo.
"Sio kwamba siku zote idadi hiyo inakuwa hivyo na pia mnaona kwamba imeanza kudhibitiwa ingawa kiwango hicho kinatia hofu," Bwana Cuomo amesema. "Hii ni idadi kubwa inayoonesha vile watu walivyopoteza maisha na machungu wanayopitia."
Jimbo la New York limekuwa kitovu cha mlipuko wa virusi vya corona nchini Marekani, na kurekodi zaidi ya wagonjwa 180,000 kati ya karibia wagonjwa 530,000 waliobainika nchini humo.
Kufikia Jumamosi, kila jimbo la Marekani lilikuwa limetangaza ugonjwa huo kama janga ikiwa ni hatua moja ya kukabiliana na mlipuko huo.
Zaidi ya watu 100,000 wamekufa na Covid-19 kote duniani tangu kuanza kwa virusi hivyo nchini China mwezi Desemba.
Taarifa mpya za corona nchini Marekani ni zipi?
Kufikia Jumapili asubuhi, Italia ilikuwa imeripoti vifo 19,468 vya virusi vya corona huku Marekani ikiwa na vifo 20,608, kulingana na takwimu za hospitali ya Johns Hopkins.
Hadi kufikia sasa, wagonjwa 529,951 wa Covid-19 wameripotiwa kote nchini Marekani.
Daktari Anthony Fauci, mkuu wa magonjwa yanayoambukiza Marekani amesema, nchi hiyo imeanza kudhibiti na kushuhudia kupungua kwa visa na vifo vya ugonjwa wa corona lakini akasisitiza kwamba juhudi za kuuzuia kama vile kutokaribiana ziendelezwe.
Hatua za serikali zilizotolewa na Rais Donald Trump, kwa sasa bado zinaendelea kutekelezwa hadi Aprili, 30.
Rais anakumbana na shinikizo mara mbili, kukabiliana na mlipuko huo huku watu karibia milioni 16 wakipoteza ajira kwa sababu ya virusi hivyo katika wiki za hivi karibuni ilihali hatua zilizochukuliwa zinaendelea kudidimiza uchumi.
Ijumaa alisema kwamba baraza jipya linalojumuisha wafanyabiashara na wahudumu wa afya, litatangazwa wiki ijayo kumsaidia katika kufanya maamuzi magumu zaidi ya ni lini masharti yaliyowekwa yataondolewa.
Hili linawadia wakati ambapo bunge linaendelea kulumbana kuhusu awamu ya pili ya kutolewa kwa fedha za kukabiliana na Covid-19.
Democrats wanataka muswada mpya uliopendekezwa wa dola bilioni 250 kusaidia biashara ndogondogo pia kuruhusu ufadhili zaidi kwa hospitali na serikali za mitaa.
Lakini Jumamosi, viongozi wawili wa Republicans bungeni, kiongozi wa walio wengi katika bunge la seneti Mitch McConnell na kiongozi wa walio wachache katika bunge la wawakilishi Kevin McCarthy, walikataa ombi hilo.
Katika taarifa yao walielezea hatua hiyo kama vitisho visivyo na msingi ambavyo vilikuwa kikwazo kwa uhifadhi wa pesa za kuokoa ajira.