Virusi vya Corona: Bunge la Kenya lafuta kikao, huku Wakenya wakionywa kuhusu wakati mgumu

Iliyochapishwa

Kikao cha bunge nchini Kenya kilichotarajiwa kufanyika siku ya Jumatano katika mji mkuu wa Nairobi kimefutiliwa mbali.

Spika wa bunge Justin Muturi aliambia vyombo vya habari kwamba kikao hicho kilifutwa baada ya rais Uhuru Kenyatta kuweka marufuku ya kutosafiri nje na kuingia Nairobi.

Mji wa Nairobi na maeneo mengine katika eneo la pwani yametajwa kuwa maeneo hatari ya virusi vya corona nchini humo.

Masharti hayo ya usafiri yanalenga kuzuia kuenea kwa virusi hivyo hadi maeneo mengine huku dunia ikitarajiwa kusherehekea siku kuu ya Pasaka wikendi hii.

Madai ya wabunge kupatwa na virusi vya corona

Lakini gazeti la Daily Nation nchini Kenya na lile la The Star yamenukuu vyanzo vilivyosema kwamba baadhi ya wabunge walikutwa na virusi vya corona katika bunge hilo siku ya Jumatatu.

Tayari baadhi yao wamelazimishwa kwenda karantini baada ya kurudi kutoka ziara za ng'ambo mapema mwezi Machi.

Uongozi wa bunge hilo uliwataka wabunge kufanyiwa vipimo ndani ya bunge hilo.

Magazeti hayo yanaripoti kwamba matokeo ya makumi ya wabunge waliopimwa wikendi yalitoka siku ya Jumatatu.

Yanasema kwamba kati ya wabunge 50 waliopimwa 17 kati yao wamepatikana na virusi vya ugonjwa huo.

Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe

Tangazo hilo la kufutwa kwa kikao hicho maalum siku ya Jumatano lilisema kwamba vikao vya kawaida vitaendelea JUmanne ijayo sawa na kalenda ya bunge.

Kenya imethibitisha visa 172 vya wagonja wa virusi vya corona kufikia sasa ikiwemo vifo sita.

Onyo la wakati mgumu siku zijazo

Wakati huohuo Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amewataka Wakenya kujiandaa kwa wakati mgumu katika siku chache zijazo huku taifa hilo likiripoti visa vingine 14 siku ya Jumanne.

Idadi hiyo imeongeza visa vya ugonjwa huo kufikia watu 172 lakini inatarajiwa kupanda baada ya waziri huyo kutangaza kwamba serikali itaanza kufanya vipimo vya wafanyakzi wote wa umma na vituo vya karantini.

Waziri huyo aliambia Wakenya kujiandaa kwa habari mbaya zaidi kwa kuwa mikakati yote ambayo imekuwa ikichukuliwa imeshindwa kuzuia kuenea kwa mlipuko wa ugonjwa huo.

Amesema kwamba licha ya kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo ipo chini, Wakenya hawafai kupumzika.

''Tunakabiliwa na wakati mgumu …jiandaeni kwa kila njia'', alisema.

''Jiandaeni kukabili hali ambayo haijawahi kutukabili. Najua tutaweza kuupita wakati huu kutokana na usaidizi tunaopata'', aliongezea.

Hatua kali

Waziri huyo aliongezea kwamba seriikali itachukua hatua kali iwapo itahitajika kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.

Kuanzia leo siku ya Jumatano Wakenya hawataruhusiwa kuingia na kutoka katika kaunti nne - Mombasa, Nairobi, Kilfi na Kwale kwa kipindi cha wiki tatu.

Hatua hiyo inaongezea masharti ya awali yaliotangazwa ya kutotoka nje nyakati za usiku kuanzia mwendo wa saa moja usiku hadi saa kumi na moja asubuhi kila siku.

Waziri Kagwe amesema kwamba rais Uhuru Kenyatta aliamua kuchukua hatua hiyo kutokana na kisa kimoja cha mgonjwa wa virusi hivyo kilichoripotiwa mandera , baada ya mwathiriwa kusafiri kutoka Mombasa.

Kuhusu vifaa vya kupima ugonjwa huo, waziri huyo amesema kwamba zaidi ya vifaa 200,000 vinatarajiwa kuingia nchini katka kipini cha siku 7 zijazo.

.