Coronavirus: 'Maisha yangu yako hatarini kwasababu ya Corona'

Chanzo cha picha, Lucy Watts
Lucy Watts, 26, amabye alituminikwa tuzo ya Malkia anajitayarisha kufa iwapo atapata virusi vya corona.
Ulemavu alionao unamfanya kuwa katika hatari ikiwemo viungo vyake kushindwa kufanyakazi na ugonjwa mapafu anaougua unahitaji uangalizi kwa saa 24.
Chama cha madaktari Uingereza kilitoa mwongozo unaotayarisha madaktari kufanya maamuzi ambayo yatazua maswali ya kutoa kipaumble kwa wagonjwa wenye uwezo mkubwa wa kupona, Lucy anahofia kwamba iwapo atapata virusi vya Covid-19 basi hakuna uwezekano wa yeye kunusurika kifo.
"Maisha yangu hayathamaniwi kwa misingi ya ulemavu nilio nao na mahitaji yangu ukilinganisha na maisha yangu na kile ambacho nimechangia katika dunia hii," anasema.
Hiki ni kifupi tu cha kile ambacho Lucy aliandika kwenye blogu yake siku kadhaa zilizopita, akijaribu kuelezea hali yake.


Chanzo cha picha, Lucy Watts
Bila shaka yoyote ninafahamu kwamba katika kipindi hiki cha Covid-19 mimi sio miongoni mwa watakaonusurika kifo.
Hii ni sehemu ya tiba kupitia kuandika, imejaa hasira, machungu na hofu. Nikujribu kutafuta amani na kujitahidi kupata ushindi.
Na huu ndio ukweli.
Nitajitenga kwa muda wa wiki 12 au pengine hata zaidi. Ninahitaji usaidizi kwa saa 24 na kawaida, wanaonihudumia ni wauguzi wanaoshughulikia wagonjwa mahututi kwa saa 16 kwa siku, lakini wauguzi wangu huenda wakaagizwa na wizara ya afya kwenda kuhudumia wengine muda wowote tokea sasa. Mama yangu anaweza kunihudumia lakini kuifanya kazi hiyo kwa saa 24 ni changamoto kubwa.
Kwasasa tunachukua tahadhari ya hali ya juu kujilinda dhidi ya maambukizi. Pia nimeamua kufanya maamuzi magumu kwa kusema kwamba iwapo nitapa Covid-19, sitajisumbua kwenda hospitali.
Kwasababu nitachukuliwa kama mtu dhaifu sana, asiye na uwezo wa kupona na pia itakuwa vigumu kwangu kuacha kutumia mashine ya kupumulia - kwasababu kwa upande mwengine misuli yangu ni dhaifu na hivyo, itakuwa vigumu kwangu kupona na kurejea kama kawaida.
kwa mtu kupata matibabu ya Covid-19 kinachozingatiwa sana ni ikiwa muathirika ana uwezo mkubwa wa kupona.
Imekuwa vigumu kukubali hili siku za nyuma. Hata mimi mwenyewe silifurahii. Inachukiza na kughadhabisha kuona kwamba maisha yangu yanaangaziwa kwa misingi ya ulemavu nilio nao, badala ya maisha yangu na kile ninachoweza kubadilisha katika dunia hii.

Chanzo cha picha, Lucy Watts
Mimi ni wa 9 katika orodha ya watu wenye ushawishi mkubwa Uingereza, nimepokea tuzo kutoka kwa Malkia kwasababu ya huduma zangu kwa watu wenye ulemavu na 2019 nilijumuishwa katika Shirika la Sanaa la Malkia kwa kujitolea kwangu kuhakikisha haki za wamelavu.
Nina zaidi ya kile ambacho kimethibitisha umuhimu wangu katika dunia hii lakini hili si chochote si lolote katika janga hili la Corona.
Nimebadilisha mioyo ya watu wengi na akili zao kupitia kazi zangu, shauku yangu, ujuzi na tajriba nilionayo.
Lakini maisha yangu hayataangaliwa kwa kuzingatia kama yenye umuhimu wakati maamuzi yatakuwa yanafanywa kutokana na upungufu wa vifaa na idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corora. Kwasasa tuna wakati mgumu wa kukabiliana na virusi hivi wakati ndio mwanzo janga lenyewe linaanza kujitokeza.
Uamuzi wa kutoenda hospitali nitakapopata virusi ni wangu binafsi, lakini suala la kupata matibabu haliko katika uwezo wangu.
Ni lazima nikubali kwamba maisha yangu sio kipaumbele na hayawezi kunusuriwa.
Lakini hata kama hilo linanifanya kuwa na hasira na kufadhaika, ni mtu mwenye kufahamu uhalisia. Ninajua kwamba kukabiliana na ugonjwa wa Corona ni kutoa kipaumbele kwa wale ambao wameonesha uwezo wa kupona.
Mwili wangu uko katika nyakati zake za mwisho.

Chanzo cha picha, Lucy Watts
Kuna mengi yanayoendelea ndani ya miwili wangu - nina ugonjwa usiojulikana ambao unasababisha seli kushindwa kutengeneza nguvu ya kutosha kwa viungo vyangu na misuli kufanyakazi.
Inafika wakati viungo vyangu vinashindwa kufanyakazi kwasababu ya tatizo la mapafu, mfumo wa kupumua ni dhaifu, maumivu makali ya kongosho ambako pia kunasababisha matumbo kuwa na matatizo mara kwa mara, kinga ya mwili isiyoweza kukabiliana na magonjwa na pia hivi karibu nilianza tatizo la maumivu ya viungo licha ya kwamba asiilimia 80 ya muda wangu huwa nina homa.
Pia nimefanikiwa kukabiliana na ugonjwa wa maambukizi kwenye damu- historia hiyo unaonaje?
Je kwa orodha hiyo ya magonjwa, huoni kama mwili wangu unarekodi nzuri tu ya kunusurika kifo licha ya kwamba mwili wangu ni dhaifu?
Lakini je nina uwezekano mkubwa wa mimi kunusurika virusi vya Corona kwa kuzingatiwa maisha ya wengine?
Ni mtihani mkubwa sana kwangu, kuhisi kwamba nastahili kupigania maisha yangu kwa namna yoyote ile lakini pia najua kwamba juhudi za kupigania kuishi huenda kukasababisha kifo kwa mwengine.
Nimepitia mengi, huzuni, kukataliwa, hasira, na mfadhaiko wa akili lakini licha ya haya yote bado ninakataliwa.
Hili sina shida nalo lakini kile ninachopinga ni kwamba maisha yangu hayana thamani.


Sikubaliani na wazo la kwamba hakuna maana ya kunusuru maisha yangu lakini naelewa tumefikaje huku.
Najua sio kuwa ninalengwa ila ni janga tu ambalo limetokea na taifa lina raslimali kigodo.
Nataka kuendelea kuishi kwasababu nina mengi ya kufanya, mipango chungu nzima na mawazo tele.
Maisha yangu ni muhimu, lakini pia yako hatarini.
Lakini tuko kwenye janga na wahusika wakuu katika kukabiliana nalo wanastahili kufanya maamuzi ya kuumiza moyo. Maamuzi ambayo ni ya uonevu lakini bado yatafanyika.
Nashukuru wahudumu wote wa afya na kile ambacho kinafanywa na kila mmoja katika kipindi hiki, naweza kunusurika au pia nikafa.
Hatahivyo, kile ninachoweza kusema ni kwamba, wahudumu wa afya wamekuwa na mchango mkubwa sana maishani mwangu.
Maisha yangu ni muhimu sasa na hata baada ya hili. Nimejitengenezea hadhi ninayoifurahia.

Ingawa Lucy anafikiria tu kwamba hataweza kutibiwa hospitali na uzuri ni kwamba hadi kufikia sasa bado yuko salama dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, mwongozo wa chama cha madaktari Uingereza, umetahadharisha madaktari kwamba watahitajika kufanya maamuzi magumu ya ni nani atakayepata matibabu ya dharura kujaribu kuokoa maisha yake ikiwemo wale watakaotumia mashine ya kupumulia.
Mwongozo huo unasema: "Inakubalika kisheria kuangalia ni wagonjwa gani mutawapa kipaumbele," na kutaka madaktari kulifikiria hilo.
Chama cha madaktari Uingereza kimesema kuwa meneja na madaktari wakuu wataangalia ni nani wa kupelekwa katika chmba cha wagonjwa mahututi na wagonjwa ambao wanaonekana kukaribia kufa au pengine wanahitaji usaidizi zaidi itakuwa vigumu kupewa kipaumbele katika matibabu ya dharura.
Julian Sheather, mshauri wa chama cha madaktari cha Uingereza amesema: "Katika hali ya sasa, swali halitakuwa ni vipi tunaweza kutoa huduma bora kwa kila mmoja, lakini namna unavyoweza kunusuru wengi.
"Itakuwa jambo la busara kunusuru maisha ya wagonjwa watatu ambao huenda wakapona kuliko kutoa kipaumbele kwa mgonjwa mmoja ambaye matumaini ya kunusurika kifo ni ya chini.













