Spencon: Jinsi tuhuma za rushwa, vitisho na magenge ya uhalifu zilivyoandama mwisho wa kampuni kubwa ya ujenzi Afrika

    • Author, Joel Gunter na Charles Young
    • Nafasi, BBC Africa Eye
  • Iliyochapishwa

Spencon ilikuwa ni moja ya makampuni makubwa ya ujenzi Afrika Mashariki. Baada ya miaka kadhaa ya shida za kifedha, mabosi wawili raia wa Uingereza waliajiriwa kuinusuru, lakini miezi 18 baadae mabosi hao walikimbia huku mamia ya Wakenya wakipoteza ajira zao. Uchunguzi wa Makala ya BBC Africa Eye unabainisha namna gani kampuni hiyo ilivyoanguka.

Mwezi Julai 2015, mabosi wawili raia wa Uingereza walitafuta eneo la wazi katika ofisi yao jijini Nairobi na kuamua kutengeneza uwanja wa gofu.

Mabosi hao, Andrew Ross na Steven Haswell wakamtafuta mshauri kutoka moja ya klabu maarufu za gofu jijini Nairobi kuwajengea kiwanja hicho.

Miti ikang'olewa na badala yake mashimo madogo ya mchanga yakachimbwa na nyasi za kijani kibichi za kuchezea zikapandwa na kunyunyuziwa maji kwa mfumo maalumu.

"Ni pazuri kwa kiasi gani?" aliandika Haswell kwenye barua pepe aliyoituma kwao Uingereza. "Tutakuwa na eneo la kupigia mpira, tunapanda majani pamoja na neti ya kuzuia mpira."

Ross na Haswell walikuwa Nairobi kwenye kazi maalumu: kuiokoa kampuni kubwa ya ujenzi nchini Kenya Spencon isife.

Walichaguliwa kuwa wakurugenzi na kampuni ya uwekezaji ya Marekani ya Emerging Capital Partners (ECP), ambayo mwaka 2006 na 2007 iliwekeza jumla ya dola milioni 15 kwa Spencon - kati ya pesa hizo, dola milioni 1.5 ni pesa za msaada kutoka serikali ya Uingereza ambazo zililenga kukuza uchumi wa Kenya na kutengeneza ajira.

Lakini Ross na Haswell hawakufanikiwa katika kuiokoa Spencon. Kwa mujibu wa maelfu ya barua pepe, ujumbe wa simu na nyaraka zilizovuja na kuonwa na Makala ya BBC ya Africa Eye, mabosi hao wawili wanaonekana kuwa walijihusisha na msururu wa biashara zenye mashaka wakijaribu kuinusuru kampuni hiyo.

Kwa sasa wawili hao wanatuhumiwa kushirikiana na mtu ambaye alishakutwa na hatia mahakamani kuziibia benki mamilioni ya dola, kuwatishia washirika wao wa kibiashara kuwa watawapelekwa kwa magenge ya wahalifu wa Kenya na kufanya malipo haramu ya pesa taslimu.

Hii ni habari ya miezi 18 ambayo Ross na Haswell walikuwa katika usukani wa Spencon kabla kampuni hiyo kuzama, na kuwaacha mamia ya Wakenya bila kazi, huku wengine wakiwa hawajapokea mishahara yao ya miezi kadhaa.

Bi Nancy Ntinu, mkuu wa zamani wa idara ya Rasilimali Watu wa Spencon, aliitembeza Africa Eye katika eneo ambalo Ross na Haswell walijenga uwanja wao.

"Kuwa na kiwanja cha gofu kwa kampuni ambayo ni muflisi, tena ikiwa katikati ya hali ngumu kifedha ni jambo ambalo lisoyumkinika," anaeleza.

"Ilikuwa ni dhihaka kwa waajiriwa raia wa Kenya kuona kipande hiki kikinyunyiziwa maji kila siku kwa sabaubu mabwana hawa wawili walitaka kucheza gofu.

'Tunaelekea kumpoteza huyu mgonjwa'

Spencon ilipata kuwa moja ya makampuni makubwa ya ujenzi katika ukanda wa Afrika Mashariki - ikiwa na wafanyakazi 5,000 katika kilele chake huku ikijivunia miradi mikubwa ya miundombinu katka nchi saba. Makao yake makuu yalikuwa katika jengo refu katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi, wakiwa majirani na makampuni mengine makubwa ya kimataifa.

Lakini nyuma ya pazia, Spencon ilikuwa na mlima wa madeni. Mapema 2014, ECP, kampuni ya Kimarekani ambayo iliwekeza dola milioni 15 ilichukua hatamu za uendeshaji wa kampuni hiyo kutoka kwa waanzilishi wake.

Novemba 2014, ECP ikamuajiri Ross - ambaye ni mhandiri na mkurugenzi wa biashara ili kuiongoza Spencon katika nyanja zote. Aprili 2015 akaungana na Haswell - mhasibu mwenye uzoefu wa kubadili biashara za Afrika, yeye alipangiwa kusimamia idara ya fedha.

Mshahara wa Haswell ulikuwa dola 25,000 kwa mwezi, Ross dola 30,000.

Kazi yao kuu ilikuwa ni kuboresha hali ya kibiashara ya Spencon ili ECP iiuze kufikia mwishoni mwa mwaka 2016. Walikuwa na miezi 18 tu kufanikisha hilo. Huku biashara ikiwa ukingoni kuporomoka, kazi yao isingelikuwa rahisi katu, lakini mustakabali wa Maisha ya maelfu ya wafanyakazi kote Afrika Mashariki ulikuwa mikononi mwa Ross na Haswell.

Bwana Wycliffe Ochieng, 38, fundi makenika msaidizi alikuwa miongoni mwa wafanyakazi hao. Bw Ochieng aliifurahia kazi yake katika kampuni hiyo. Ajira yake ilimuwezesha kupanga nyumba ndogo jijini Nairobi akiishi na mkewe nab inti yao mdogo. Nyumba ilikuwa na maji na umeme, na akaanza kuwa na ndoto za maisha mazuri na familia yake.

Mwezi Novemba 2016, hatimaye Spencon ilikufa rasmi, Ochieng akajikuta hana kazi na yupo ndani ya deni. Alikuwa akidai miezi kadhaa ya mishahara huku naye akidaiwa miezi kadhaa ya kodi ya pango.

"Alikuwa akitununulia vitu kama viatu na nguo," anakumbuka mkewe, Bi Lynet. "Baadhi ya vitu alivyotufanyia tukiwa mjini ni tofauti kabisa ukilinganisha na hali ya sasa."

Kwa saa familia hiyo inaishi kwenye kibanda kidogo kwenye eneo la wazazi wa Ochieng, maili 230 (370km) kutoka Nairobi. Hawana umeme wala maji. Wanalala kitanda kimoja na mtoto wao.

Ochieng kwa sasa analima ili kuilisha familia yake kadri awezavyo. Baadhi ya siku hupita bila kupitisha kitu kinywani.

"Nilikuwa naitunza familia yangu kama mwanaume anavyotakiwa kufanya," aliiambia Makala ya Africa Eye mwaka jana huku akiwa mwenye huzuni. "Hii hali imeninyongonyeza na kushusha kujiamini kwangu."

Mwezi Julai 2015, Ochieng aliwasili Spencon kuanzan kazi kama fundi makenika msaidizi, akiwa mwenye furaha bila kujua kuwa kama kampuni hiyo tayari ilikuwa kwenye matatizo makubwa. Siku chache baada ya Ochieng kuanza kazi, Andrew Ross aliwaahidi wafanyakazi kuwa hakuna hata mmoja ambaye atapoteza ajira yake. Lakini barua pepe ambayo ilitumwa mwezi Aprili na Steven Haswell inaonesha. Kuwa tayari alishaanza kuwa na khofu.

"Nafikiri tunaelekea kumpoteza huyu mgonjwa!" aliandika. "Tuna pesa ya miezi 4 tu … hali si nzuri."

Mabosi hao walipunguza matumizi mwezi Julai, wakipunguza baadhi ya wafanyakazi na kuhamisha makao makuu ya Spencon kutoka katika viunga vya kifahari jijini Nairobi mpaka kwenye karakana moja iliyomilikiwa na kampuni hiyo nje ya mji.

Lakini pia walianza matumizi.

Wiki moja baada ya kufuta watu kazi, Ross na Haswell walilipa dola 70,000 kujinunulia magari - Range Rover na Volkswagen Touareg. Haswell ameiambia Africa Eye kuwa magari hayo yalitoa taswira ya kampuni ya maana na si ambayo ilikuwa karibu na kufilisika. Ross amedai kuwa magari hayo yalipitishwa na bodi ya kampuni.

Hata hivyo wafanyakazi hawakufurahishwa. "Yalikuwa matumizi ya kifahari," ameeleza aliyekuwa meneja wa vifaa wa Spencon Mike Hyland, ambaye aliratibu manunuzi hayo.

Dickens Omollo, aliyekuwa mkuu wa ulinzi katika karakana alipigwa na bumbuwazi na Range Rover ya Ross. "Tulistaajibia - hii ni pesa nyingi, na hatuna pesa, nab ado anasema anataka kuinyanyua kampuni?"

Ross na Haswell pia waliendelea na ujenzi wa kiwanja chao cha gofu. Mtaalamu ambaye walimuajiri kutoka katika moja ya Klabu kubwa za gofu Kenya alikuwa mbioni kubuni kiwanja cha mazoezi cha kifahari - kikiwa na mashimo mawili ya tani 120 za mchanga.

Mabosi hao wawili wameiambia Africa Eye kuwa kiwanja hicho cha gofu kilitengenezwa kwa gharama ndogo sana na kwa kutumia wafanyakazi na vifaa vya Spencon na kutoa taswira nzuri ya kampuni.

Simeon Randinga, alikuwa na mfanya usafi katika kampuni hiyoalihisi kiwanja hicho hakikuwa kwa ajili ya wafanyakazi wa kada ya chini. "Kiwanja kile kilikuwa nje ya mipaka yetu," amesema. "Kilikuwa chao wawili tu."

Ross na Haswell wameiambia Africa Eye kuwa kiwanja hicho kilikuwa wazi kwa wafanyakazi wote kukitumia.

Mauzo ya punguzo

Kupata kazi Spencon ilikuwa ni kila kitu kwa Randinga. Alikuwa ndio ametoka tu kufunga ndoa, na alishaanza kuwa na khofu kuwa mkewe angelimkimbia kama asingeliweza kumtimizia mahitaji yake. Kipato cha uhakika kutoka Spencon kiliondosha khofu yake. Baada ya miezi michache ya kazi mkewe alijumuika naye jijini Nairobi na wakapata mtoto.

Kufikia katikati ya 2015, Randinga alibaini kitu ambacho kilimtia wasiwasi, anasema - kampuni ilikuwa ikiuza mashine nzima kabisa pamoja na machine mbovu na vyuma chakavu.

"Kwa nini wanauza vitu hivi, niliuliza, 'Hivi ni vitu vizima kabisa, kwa nini mnaviuza? Mnahakika bado tuna ajira?'."

Aliyekuwa nyuma ya usukani wa mauzo hayo ni Tony Sanghani, mshauri wa masuala ya usalama aliyeajiriwa na Ross na Haswell. Pamoja na usalama, mabosi hao walimpa kazi ya kuuza kwa punguzo la bei vifaa vya Spencon. Baadae walidai kuwa hakujua kama Sanghani alikuwa na rekodi ya uhalifu.

Utafiti mdogo tu wa mtandao wa Google unaonesha kuwa Tony na kaka yake walifungwa jela mwaka 2002 kwa washurutisha walinzi wa kampuni yao kuwashambulia watu wawili.

Mike Hyland, aliyekuwa meneja wa vifaa wa Spencon, anaamini kuwa Ross na Haswell walijua fika. "Nina hakika kwa 100% kuwa walijua," anasema. "Nilimwambia Andrew Ross wakati najiuzulu kuwa unafanyakazi na mhalifu." Kwa mujibu wa Hyland, Ross alijibu kuwa: "Inatupasa kufanya kile tunachoweza kufanya." Ross amekana kujua rekodi ya uhalifu ya Sanghani ama kumjibu Hayland kwa namna hiyo.

Barua pepe zilizovuja zinaonesha kuwa Sanghani alikuwa na baraka zote za mabosi hao katika kuuza mali. "Tafadhali mpeni ushirikiano wenu na msaada Tony kubadili mashine za zamani na vipuri kuwa fedha," aliandika Haswell kwenye barua pepe kwenda kwa wafanyakazi wote Oktoba 2015. "Tafadhali hakikisheni Tony anapewa ushirikiano kamili," aliandika Ross katika barua pepe nyengine.

Wakati Randinga na wafanyakazi wengine wa Spencon wakijawa na khofu juu ya ajira zao, Sanghani alikuwa akichukua mshahara mkubwa na kuishi kwenye nyumba aliyopangiwa na kampuni ikiwa na samani zote. Pia alipewa gari na dereva, pia alipewa ahadi ya kupewa bonasi ya pesa akikamilisha mauzo ya vifaa.

"Inaonekana kama yalikuwa mauzo kamili ya kufungasha virago, mali ziliuzwa kwa bei ya kutupa," anaeleza Kabiito Karamagi, afisa aliyekabidhiwa hatamu za Spencon baada ya kufilisika ili kuchunguza mauzo yaliyofanywa na Sanghani nchini Uganda. "Tulichokigungua ilikuwa ni kushushwa kwa thamani sana kwa mali."

Pesa zilizopatikana zilitakiwa kwenda kulipa madeni ya kampuni kwa benki za Uganda, lakini fedha hizo zililipwa kwenye akaunti binafsi ya Sanghani.

Mfanyakazi mmoja wa Spencon alimwandikia Haswell barua pepe na kuuliza juu ya mfumo huo wa malipo na kuuliza kama hautaisababishia kampuni matataizo ya kisheria, Haswell alijibu: "Ni sawa… tunaweza kulipa kwa kutumia akaunti ya benki ya Tony."

Karamagi, afisa muflisi, aliuliza namna gani peza hizo zililipwa na kukaguliwa. "INi hakika kabisa kuwa si jambo la kawaida kuwa fedha hizi hazikulipwa kwenye akaunti ya kampuni na badala yake kampuni binafsi. Ni jambo la kushangaza kabisa," amesema. t's certainly most unusual that these monies are not banked on the company account, but on an individual's account. It is most unusual," he said. "Ni ubadhirifu."

Baada ya kufilisika Spencon iliwekwa chini ya uendeshaji wa - shirika la kimataifa la uhasibu PWC - ambalo liligundua kuwa Sanghani alikuwa akilipwa dola 20,000 kwa mwezi na Ross na Haswell, pamoja na kamisheni ya asilimia 25% ya mauzo. PWC walikiita kima hicho kama cha "kushtusha" kwa muktadha wa kifedha amabao Spencon ilikuwemo.

PWC pia waligundua shimo kubwa jeusi kwenye vitabu vya mahesabu vya Spencon - takribani dola milioni 1.6 ilikuwa haijulikani ilipo. Kwa mujibu wa hesabu za Karamagi, kiasi cha fedha kilichopotea kinaweza kuwa kikubwa zaidi.

Kuna maswali pia juu ya namna mali za kampuni hiyo zilivyouzwa nchini Kenya na PWC tayari wamewasilisha mafaili kwa polisi nchini humo.

"Kulikuwa na nia ya kuwazunguka wakopeshaji, hilo lipo wazi kabisa," anaeleza Karamagi. "Kilichopo hapa ni ubadhirifu, wizi."

Polisi nchini Uganda waeiambia Ugan Africa Eye kuwa wanashirikiana na Interpol kuwahoji Ross na Haswell. Wote wawili wanakanusha vikali kufanya makossa yoyote na kudai kuwa hawakujua uchunguzi wowote wa uhalifu ama malalamiko ya aina yoyote yaliyowasilishwa kwa uongozi (wa Spencon) juu ya mauzo hayo.

Haswell anasema kuwa malipo yalifanyika kupitia akaunti binafsi ya Sanghani ili kulinda fedha hizo dhidi ya wakopeshaji wao ambao walikuwa na amri za "uongo" za mahakama za kuchukua fedha hizo. Kuweka fedha kwenye akaunti ya Shangani kungeliwezesha Spencon "kuzitumia kadri ilivyotaka," ameeleza Haswell.

Wote wawili wanadai kuwa fedha zote ambazo zililipwa kwenye akaunti ya Shangani hesabu yake ilifanyika na thamani ya vifaa ilipandishwa na benki zilitaarifiwa kila wakati.

"Miamala yote ilirekodiwa kwenye akaunti za kampuni na kuridhiwa na bodi," ameeleza Ross.

ECP imeambia Africa Eye kuwa "haikufahamu matendo hayo yanauodaiwa kufanywa na Sanghani" pia "haikuwa na faida yeyote kwa fedha za Spencon kulipwa kwenye akaunti za watu wengine."

Kufikia mwishoni mwa 2016, PWC ilimbana Tony Sanghani kukabidhi akaunti zake lakini aligoma kutoa ushirikiano. Kwa mujibu wa PWC dola milioni 1.6 bado haijulikani ilipo. Africa Eye ilimtafuta Tony Sanghani lakini alikataa kuzungumza.

'Kuna harufu ya rushwa'

Mwezi Disemba 2015, matumaini ya Ross na Haswell ya kuinusuru Spencon yalikuwa yapo kwenye deni ambalo kampuni hiyo ilikuwa ikiidai serikali ya Kenya kwa kandarasi ya kutengeneza mtambo wa kuchakata maji taka mjini Mombasa mwaka 2000.

Deni hilo lilithaminishwa na Spencon kufikia dola milioni 16.5. Pia kulikuwa na ahadi ya malipo ya ziada katika mikataba ya Ross na Haswell: endapo malipo ya deni hilo yangelipitishwa, Ross angelipata bonasi ya kufikia dola 80,000 na Haswell kufikia dola 64,000.

Mabosi hao walikuwa wakikaribia kuingia katika moja ya kurasa chafu za sakata la Spencon.

Kabla ya malipo, serikali ya Kenya ilitaka kwanza hati halali waliyopewa Spencon kuthibitisha kukamilisha ujenzi huo, lakini kulikuwa na tatizo: Spencon hawakuweza kuiona.

Walikuwa na siku 10 tu za kuwasilisha hati hiyo mahakamani. Mwananasheria wa Spencon Rose Osiemo alifunga safari ya haraka kwenda Mombasa, ambapo alipata barua kutoka kwa Katibu wa Kaunti kuagiza kutolewa kwa hati mpya. Lakini alipoenda kwenye idara husika inayotoa hati, akakumbana na kikwazo.

Ujumbe wa WhatsApp alotuma siku sita mbele unainisha kikwazo husika - kuna mtu alikuwa akitaka kulipwa dola 80,000 pesa taslimu.

Haswell akamtaarifu Tony Sanghani kujiandaa, kisha akamtumia ujumbe Osiemo kumfahamisha.

"Nimemweleza (Shangani) kinachoendelea … amekubali kuwa unaweza kumuomba ili awaminye kidogo kama utataka???"

Hata hivyo Bi Osiemo alidai kuwa mtu wake anataka kutojulikana. "Wanataka isalie kati yangu mimi na wao ama la watajulikana," alimjibu Haswell.

Kama malipo yalikuwa ya kawaida, kwa nini yalikuwa yanalipwa kwa fedha taslimu, na kwa nini Bi Osiemo alikuwa akifanya siri mtu anayelipwa?

Bi Osiemo alitaka apatiwe pesa hizo mapema ili awahi ndege ya asubuhi kupatia mtu wake, na kusababisha hali ya haraka ya kuzisaka. Haswell alikuwa Tanzania. "Kwa sasa nipo benki kuchukua I'm now in bank getting $80k taslimu kwa ajili yako," alimtumia ujumbe Bi Osiemo. Pia alimtaarifu Ross kwa kumtumia ujumbe: "Najaribu kutoa $80k taslimu kutoka SCB (Benki ya Standard Charted) Tanzania. Nitasafiri nazo (kwa ndege) usiku wa leo."

Haswell akarejea Nairobi na kumkabidhi bahasha mbili Bi Osiemo zilizojaa noti, na akawahi ndege ya asubuhi akisindikizwa na Tony Sanghani.

"Kumbuka ni watu 11 ndio wanaojua kuwa unasafiri na $80k," Haswell alimwandikia ujumbe na kumweleza: "Kuwa makini na salama."

Bi Osiemo alimlipa mhusika na kupata barua iliyothibitisha kuwa ujenzi ulikamilika. Lakini hata hivyo mpango huo ulifeli - pesa ambazo serikali ilikuwa ikidaiwa na Spencon hazikutolewa.

Africa Eye ilimuonesha Ushahidi wa malipo ya dola showed 80,000 Bwana Jeremy Carver, mwanasheria aliyesaidia kutunga sheria dhidi ya rushwa nchini Uingereza.

"Malipo ya $80,000 yameorodheshwa vyema kwenye makaratasi niliyoyaona," amesema Carver. "Inaonekana kama rushwa, kuna harufu ya rushwa na imelipwa na watu wanaofanya kazi kwenye kampuni ambao kwa uwazi kabisa wanajaribu kulifanya jambo hilo kuwa siri."

Kwa mujibu wa sheria ya Uingereza, endapo raia wa nchi hiyo atahusika na vitendo vya rushwa, atakuwa ametenda kosa na haijalishi ni wapi madai hayo ya rushwa yametokea.

"Kwa wakurugenzi wa Kingereza, na hakika mtu yeyote aliyehusika na malipo, kwa kile kinachoonekana tu kwa sasa inabidi wachunguzwe," ameeleza Carver.

Bi Osiemo amekanusha kutoa hongo ya fedha taslimu kwa mtu yeyote ili kufanikisha madai ya ujenzi wa Mombasa. Ameeleza kuwa fedha zile zilikuwa ni za malipo ya mshauri ambaye (hakutajwa jina) alipewa kazi na Spencon naye akaajiri wahandisi wane wanaojitegemea kukagua eneo la mradi na kuandika ripoti ya kuthibitisha kuwa ujenzi umekamilika. Bi Osiemo anadai alipatiwa hati na mmoja wa hao wahandisi.

Taarifa aliyotumiwa kwa barua pepe kwa Haswell siku moja baadae inaorodhesha matumizi ya dola 80,000, bila ya mkandarasi yeyote kutajwa. Ross amekataa kuongelea kuhusu madai ya malipo hayo, huku Haswell akisema hakuwa na taarifa za kwanini malipo hayo yalirekodiwa kwa namna yalivyorekodiwa.

Wote wamekataa kusema nani alipokea dola 80,000 na kwa nini ililipwa taslimu, wakisema pesa ilenda kwa wakala wa kukusanya madeni. Wamekanusha vikali kuwahonga maafisa wa serikali, na kusema kuwa ujumbe wa WhatsApp na barua pepe vimetafsiriwa nje ya muktadha wake.

Ross amesema yeye na Haswell waliitaarifu bodi ya ECP juu ya maendeleo ya deni kwa serikali na watu ambao walikuwa wakishirikiana nao. ECP imesema kuwa haina taarifa yeyote ya namna gani hati mbadala ilipatikana.

Familia ya kihalifu

Katika harakati zao za kuibadili Spencon ili iuzike, Ross na Haswell walihitaji kuitenganisha kampuni hiyo na historia yake mbaya. Lakini walikwamishwa na kesi iliyofuguliwa na familia ya Patel iliyoanzisha kampuni. Kesi ilikuwa ikipinga kwa kampuni hiyo kuchukuliwa na ECP mwaka 2014.

Pragnesh Patel, ambaye baba yake alianzisha Spencon mwaka 1979, ameiambia Africa Eye kuwa Ross na Haswell walimualika kwenye kikao katika hoteli ya Kempinski jijini Nairobi mwezi Disemba 2015 kumpa ofa ya Spencon kumuachia hisa za umiliki wa eneo la thamani kwa maendeleo endapo ataiondoa kesi hiyo mahakamani.

Patel anasema alipowauliza nini kitatokea endapo atakataa, mabosi hao wawili wakamtajia jina la anayetaka kulinunua eneo hilo - familia ya Akasha.

Akina Akashas ni genge la kuogopwa Kenya. Agosti 2019, Batktash Akasha alihukumiwa miaka 25 jela nchini Marekani kwa kuendesha mtandao wa kusafirisha dawa za kulevya ulimwenguni. Mwezi Januari mwaka huu, ndugu yake Ibrahim alihukumiwa miaka 23 kwa kosa hilo pia.

Tony Sanghani ni mmoja wa watu anayewajua vyema akina Akasha. Kwa mujibu wa Ushahidi uliotolewa mahakamani, akina Akasha walimpiga vibaya kwenye vita ya magenge ya dawa za kulevya mwaka 2014 kiasi cha Sanghani kuishia kulazwa katika hali koma.

Pragnesh Patel anasema aliingiwa na khofu. Anasema aliondoka na kwenda kutafakari nini cha kufanya, kisha akamuomba Ross wakutane kwa mara ya pili na mara hii akarekodi mazungumzo yao kwa siri kupitia simu yake.

Katika rekodi ya mazungumzo hayo, Patel anasikika akimuuliza Ross kama uhusiano na Akasha ni wa kweli.

"Ni kweli Pragnesh," Ross anajibu. "Hatufanyi mchezo hapa, ni kweli."

"Hili ni suala zito," akasema Patel. "Wajua familia ya Akasha ni sawa na Al Capone. Hata wakijua tu kuwa najaribu kuzuia kuuziwa eneo, wanaweza kunitumia muuaji ama vitu vya aina hiyo."

Hiyo ilikuwa ni moja ya mara nyingi ambazo Patel alipaza sauti yake juu ya khofu kuwa kampuni inaweza kuuzwa kwa akina Akasha. Si hata mara moja, katika mkanda mzima uliorekodiwa ambapo Ross anasikika akipingana na khofu ya Patel.

Ross ameiambia Afrika Eye ya kwamba ni uongo na upuuzi kuwa alimtisha Patel kwa kutumia jina la familia ya Akasha family. Pale Africa Eye ilipomtumia nakala ya rekodi ya mazungumzo, alisema kwamba hakuna sehemu yeyote aliyowataja akina Akasha.

Haswell amesema kuwa hakuna wakati wowote ambao Spencon ilijaribu kufanya biashara yeyote na akina Akasha na kudai kuwa Patel alikuwa akijaribu kumuingiza Ross kwenye mtego. Amesema kuwa hakuwajua akina Akasha mpaka pale Patel alipowataja.

'Ukipiga chafya unapoteza'

Kufikia katikati ya mwaka 2016, hali ya Spencon ilikuwa mahututi. Siku za mwisho za uhai wa kampuni zilikuwa zikijongea katika ofisi zao za makao makuu kwenye karakana ya matengenezo nje kidogo ya jiji la Nairobi.

Nancy Ntinu, mkuu wa kitengo cha Rasimali Watu alikuwa akifanya kazi kwa karibu na Ross na Haswell. Mishahara ya wafanyakazi ilikuwa ikiyoyoma na wafanyakazi walikwa wakijawa na hasira. Wengi wao akiwemo Ntinu walikuwa hawajapokea malipo kama ilivyostahili kwa miezi kadhaa.

"Nilikuwa nalia kila siku maana sikuamini hali amabayo nilikuwa nimejikuta nayo," ameeleza.

Ntinu ameiambia Africa Eye kuwa Ross alipitia orodha ya wafanyakazi, na kumwamuru yupi wa kumlipa na yupi wa kutomlipa.

"Kulikuwa na mfanyakazi mmoja mwanamke ambaye alikuwa kwenye likizo ya uzazi na akamkata jina lake. Nikauliza kwa nini, akasema, 'Ukipiga chafya unapoteza'."

Ntinu anadai kuwa kuna mtu mmoja amabaye alikuwa lazima alipwe - Ross. "Alikuwa akijilipa," amesema.

Ross ameiambia Africa Eye kuwa wafanyakazi waliokuwa wakipokea kima cha chini kabisa ndio waliokuwa wakitangulia kulipwa na hata mshahara wake ulikuwa ukichelewa mara kadhaa. Alikanusha kutumia msemo, 'Ukipiga chafya unapoteza'.

Wakati huo, wafanyakazi wa Spencon waliendelea na kazi bila malipo wakiamini kuwa kampuni ingeliokolewa. Wycliffe Ochieng, fundi makenika msaidizi anasema kuwa kutolipwa kulikuwa kunaathiri ndoa yake. Mkewe alianza kujenga dhana ya kuwa Ochieng anatumbua mshahara wake na mwanamke mwengine. Hatimaye mke akaondoka, hali iliyomlazimu kumpeleka binti yake kwa wazazi wake mamia ya maili ili yeye aendelee kufanya kazi jijini Nairobi.

Simeon Randinga, mfanya usafi, ilimbidi aanze kumkimbia mwenye nyumba wake kwa kukosa pesa ya kulipa kodi ya pango. "Tulijikuta tunaenda nyumbani bila pesa mwishoni mwa mwezi," anaeleza. "Mwenye nyumba yupo hapo anakusubiria na wewe pia unahitaji chakula, lakini hauna kitu."

Hata hivyo hakufikiria kwenda kumlalamikia Andrew Ross. "Kumfikia ilikuwa ka kwenda peponi," anasema.

Ross alikuwa kwenye likizo ya kucheza gofu nchini Uturuki aliposaini makaratasi ya kuitangaza Spencon kuwa muflisi. Jijini Nairobi wapiga mnada walishaanza kuzishikilia mali za kampuni huku wafayakazi wakizua rabsha za kupinga hatua hiyo.

Baada ya kurejea Nairobi Ross aliitisha mkutano wa wafanyakazikuwatai habari za kufilisika. Walipandwa na hasira, kkundi la wafanyakazi 15 walimfuata Ntinu wakitaka majibu. "Unazungumzia watu wenye hasira, ambao hawana kitu cha kuzilisha familia zao," anasimulia.

Ntinu alijua kwamba mambo yamekwishafika fikia tamati. Aeiambia Africa Eye amepoteza malipo ya miezi saba -taribani pauni 39,000.

Baada ta takribani miaka 40 katika biashara Spencon ilitoweka. Muda mfupi baadae wakafuatia Ross na Haswell.

"Tulisikia tu asubuhi moja kuwa wamepanda ndege na kurejea Uingereza," ameeleza Ntinu. "Na hivyo ndivyo ilivyotokea."

Ross na Haswell wameiambia Africa Eye kuwa wanajivunia muda wao katika kampuni ya Spencon, wakisema waliiongoza katika kipindi kilichojaa changamoto pamoja na kurithi madeni, lakini walifanya kazi yao kwa mujibu wa sheria na kila wakati walikuwa wakishauriwa kisheria. Wamesema pia wanaelewa hasira na kuvunjika moyo kwa wafanyakazi na kujitenga na tuhuma za kufanya makosa ya aina yoyote.

Wanasema iliwabidi wakimbie Kenya kwa sababu walikuwa wanapokea vitisho, na waliendelea kufanya kazi za Spencon bila malipo kwa miezi minne.

Miaka mitatu unusu baadaye, wote wawili wameajiriwa katika nafasi za juu kwenye makampuni ya Uingereza.

Wengi wa wafanyakazi wa Spencon hawakupata bahati kama hiyo ya kupata ajira mpya. Hakuna hata mmoja aliyelipwa madeni ya mishahara yao.

Simeon Randinga, aliyekuwa mfanya usafi kwa sasa anauza mkaa ili aendelee kuitunza familia yake. Anasema alipambana dhidi ya fikra za kutaka kujiua. "Usipokuwa na kazi unakuwa mtu usiye na manufaa, hauwezi kumsaidia mtu yeyote. Hauwezi kuilisha familia yako, hauwezi kulipa pango la nyumba. Hata kuoga haiwezekani kwa kuwa huwezi kununua sabuni."

Wycliffe Ochieng, fundi makenika hakuwahi tena kurejea katika nyumba ile ya Nairobi ambayo ilimfanya apate ndozo za maisha bora - mwenye nyumba wake alimfurusha na kufungia vitu vyake vyote ndanai ya nyumba. Kitu pekee alichosalia nacho ni ovaroli la Spencon na kofia ngumu ya usalama kwenye ujenzi. Zamzni alikuwa akijisikia fahari kuvaa mavazi hayo, anaeleza, yalimfanya ahisi kuwa amefanikiwa. Wakati mwengine binti yake humwambia ayavae ili wacheze, lakini amepungua uzito kulinganisha na enzi za Spencon, na mavazi hayo kwa sasa yanampwaya.

Ochieng mara kadhaa huzungumza na wafanyakazi wenzane wa zamani wa Spencon kwa kutumia simu ya kulipia iliyo jirani. "Wakati mwengine napokea simu - Hello, rafiki yangu, unaweza kunikopesha shilingi 100?" Hiyo ni sawa na dola 1 tu. Lakini hana.

Baada ya kukaa miezi mitatu bila malipo mwaka 2016, Ochieng akiwa na kundi la wafanyakazi wengine wa Spencon walienda kuuharibu uwanja wa gofu ambao ulijengwa na Ross na Haswell. Mkanda wa video ulirekodi vitendo vyao vya kupinga kutolipwa.

"Kama uonavyo, hakuna mtu amabaye alikwa na furaha," anaeleza Ochieng, hukua kiangalia video hiyo. "Hakuna hata mmoja aliyekuwa anacheka."