Virusi vya corona: Idadi ya wagonjwa yafikia 126 , raia waagizwa kuvaa barakoa

Iliyochapishwa

Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ametangaza kwamba Kenya imethibitisha visa vinne zaidi vya virusi vya corona .

Wanne hao ni Wakenya 3 na raia mmoja wa Pakistan.

Idadi hiyo sasa inafanya idadi ya walioambukizwa kufikia 126 baada ya watu 12 kukutwa na virusi hivyo siku ya Ijumaa.

''Visa viwili ni vya watu waliosafiri kutoka Malawi na Pakistan huku wawili wakiambukizwa virusi hivyo nchini Kenya'' alisema Kagwe.

Umri wao ni kati ya miaka 34 hadi 44. Watatu kati yao ni wanaume huku mmoja akiwa mwanamke.

Idadi ya watu wanaochunguzwa kwa kukaribiana na wagonjwa

Waziri huyo amethibitisha kwamba watu 1,781 waliokaribiana na wagonjwa hao wanachunguzwa.

Katika hotuba yake ya kila siku kuhusu hali ya virusi vya corona nchini Kenya, waziri huyo pia alituma risala za rambirambi kwa rubani wa ndege ya kampuni ya Kenya Airways Daudi Kibati aliyefariki wiki hii kutokana na viruis vya corona.

Rubani Kibati pamoja na wafanyakzi wenzake walifanikiwa kuwasafirisha nyumbani Wakenya kutoka nchini Marekani , alijitolea kwa hali na mali., alisema Kagwe .

Wakenya waombwa kuvaa barakoa

Kiongozi huyo vilevile alitoa masharti mapya ya kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo akiwaomba raia kuvaa barakoa wakati wanapotemebelea maduka ya jumla ama soko lolote lile la wazi .

"Tunawaomba wale wanaotembelea maduka ya jumla kuanza kuvaa barakoa mara moja'' , alisema.

Waziri Kagwe pia alisema kwamba serikali ina uwezo wa kutengeneza vifaa vya kujilinda dhidi ya virusi hivyo PPE.

Wahudumu wa afya wahakikishiwa usalama wao

Aliwahakikishia wafanyakazi wa Afya kwamba sasa watakuwa salama .

Matamshi yake yanajiri kufutia malalamishi kutoka kwa madaktari kuhusu ukosefu wa mavazi ya kujilinda kwa wale wanaotibu wagonjwa wa virusi hivyo.

Amesema kwamba wizara ya afya imeimarisha huduma za hospitali ya Kenyatta University na tayari wagonjwa 20 wanaougua virusi vya corona wamelazwa.

Alitangaza kwamba maabara za serikali hususan ile ya Kemri tayari inahusika na utafiti mkali ambao utaisaidia Kenya kutengeneza vifa vyake vya kupima virusi vya corona.

Waziri huyo amesema kwamba watu waliokuwa katika karantini wamepatikana na virusi hivyo akiongezea kwamba hatua hiyo huenda ikasababisha maambukizi zaidi baada ya baadhi yao kukiuka miko iliotolewa.

Kutokana na hilo Kagwe amesema kwamba Serikali imeongeza muda wa kutengwa kwa wale waliopo katika karantini hadi siku 14 zaidi