Virusi vya Corona: Wagonjwa 12 zaidi wapatikana na virusi hivyo Kenya na kufanya idadi kufikia 122

Iliyochapishwa

Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) nchini Kenya imefikia 122 baada ya watu wengine 12 kuthibitishwa kuwa navyo ndani ya saa 24 zilizopita.

Katibu wa kudumu katika wizara ya Afya Mercy Mwangangi amesema kwamba kati ya raia hao waliopatikana na virusi hivyo ni Wakenya 11 na raia mmoja wa Somalia.

Aidha amesema kwamba Kenya imepoteza mgonjwa mwengine kupitia virusi hivyo na kufanya idadi ya waliofariki kufikia watu 4.

Amesema kwamba mgonjwa huyo ni mvulana wa miaka sita ambaye alikuwa akiugua ugonjwa uliokuwa ukiathiri kinga yake.

Tayari maafisa wa afya waliokuwa wakimhudumia mvulana huyo katika hospitali kuu ya Kenyatta jijini Nairobi wamewekwa katika karantini.

Serikali ilianzisha utengenezaji wa barakoa ambazo zitasambazwa katika serikali za kaunti na kwa wenyeviti wa sekta ya bodaboda na matatu

Washonaji pia wataruhusiwa kutengeneza barakoa kutokana na vifaa fulani na wameshauriwa kuuza kwa bei ya chini.

Kaunti pia zitaajiri maafisa 5000 wa afya katika kipindi cha siku saba zijazo kuanza sasa.

Siku ya Alhamisi waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kwamba watu wengine wawili walipoteza maisha yao kutokana na maambukizi ya virusi hivyo.

Waziri huyo pia alipiga marufuku usafiri wa Wakenya kuelekea katika maeneo ya mashambani akionya kwamba huenda wakapeleka maambukizi ya virusi hivyo katika maeneo hayo.

Amesema kwamba serikali imewapima watu 662 katika kipindi cha saa 24 ambapo takriban watu 29 wamepatikana na virusi hivyo.

Kagwe amesema kwamba wagonjwa 28 kati ya wale waliopatikana na virusi hivyo ni raia wa Kenya huku mmoja akiwa raia wa DR Congo.

''Kati ya wagonjwa hao 29, 13 ni wanaume huku 16 wakiwa wanawake na tayari 23 kati yao wanahudumia karantini'', alisema Kagwe.

Waziri huyo amesema kwamba visa hivyo vinaathiri Wakenya waliopo kati ya umri wa miaka 16 hadi 64.

Wakenya waonywa kusafiri mashambani siku kuu ya Pasaka

Vilevile Mutahi Kagwe alizindua mikakati ya kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo hatari.

Alitangaza kwamba wahudumu wote wa usafiri wa umma watalazimka kuvalia barakoa huku akionbgezea kwamba visa vya maambukizi vitaongezeka katika siku chachge zijazo , akiwataka Wakenya kuwa watulivu na kufuata maelezo yaliowekwa na wizara ya Afya.

''Tulieni sitaki kuwatishia idadi hii itaongezeka na kuongezeka zaidi'', alisema waziri huyo wa Afya.

Naibu gavana aliyedaiwa kusababisha maambukizi apona na kukamatwa

Waziri huyo vilevile amesema kwamba naibu wa gavana katika kaunti ya Kilifi Gideon Saburi amepona virusi hivyo .

''Naibu gavana huyo amepona virusi hivyo baada ya kupimwa mara tatu . Na sasa tutawacha sheria ichukue mkondo wake'', alisema Kagwe.

Hatua hiyo inajiri baada ya wizara ya Afya nchini Kenya kutangaza kwamba mgonjwa wa kwanza na watatu waliopatikana na ugonjwa huo wamepona.

Wagonjwa hao Brenda Cherotich na Biian Orinda walizungumzia kuhusu uzoefu wao wakiwa karantini.

Kufikia siku ya Jumatano, serikali ilikuwa imefanikiwa kupima watu 300 katika kipindi cha saa 24 ambapo kati ya visa hivyo 22 walikutwa na ugonjwa huo.