Coronavirus: Kuna haja ya kununua chakula kingi kujiandaa na marufuku ya kutotoka nje?

Tangu nchi mbalimbali duniani kuweka sharti la kutotoka nje kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vyakula kwa urahisi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tangu nchi mbalimbali duniani kuweka sharti la kutotoka nje kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vyakula kwa urahisi
Iliyochapishwa

Dunia ikiwa na makatazo mengi katika maeneo mbalimbali kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, huduma muhimu pia zimekuwa hazipatikani kwa urahisi kwa mfano chakula.

Licha ya kwamba kuna namna ambayo mataifa mengine yamekuwa katika upande wa faida kwa namna moja au nyingine, kwa kujifunza namna ambavyo mataifa mengine yameweza kukabiliana na janga hilo.

Tukiangazia upande wa bara la Afrika, eneo ambalo mlipuko huu wa virusi vya corona ulifika kwa kuchelewa tofauti na mabara mengine duniani, Inawezekana mataifa yake yameweza kujifunza na kuiga kutoka kwa mataifa mengine na hata kuendelea kujifunza namna ya kukabiliana na janga hili.

Jambo la muhimu ambalo limekuwa likiumiza vichwa mataifa mengi, ni suala la kuzuia watu kutotoka nje ili kupunguza uwezekano wa ugonjwa huo kuenea.

Barani Afrika tayari tumeshuhudia mataifa ambayo yamefunga miji au nchi kwa ujumla au kuweka makatazo kama Rwanda, Uganda, Afrika Kusini,DRC na kwingineko.

Katika maeneo hayo ambayo yamefunga miji au nchi, wananchi wamekuwa wakilalamikia huduma muhimu ya chakula na kuhofia kujikimu wakati wakiwa ndani.

Yawezekana kutokana na hofu ambayo imeonekana kwa wengine, ni wakati muafaka kwa mataifa ambayo hayajaanza kuchukua hatua ya kufungia mji kama Tanzania, watu wake kuanza kujiandaa mapema kwa kuchukua tahadhari ya kuepuka changamoto yeyote inayoweza kujitokeza kama mlipuko huu utaendelea kuwepo kwa muda.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa vyakula vinavyonunuliwa kwa wingi vinakuwa salama

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ni muhimu kuhakikisha kuwa vyakula vinavyonunuliwa kwa wingi vinakuwa salama

Wataalamu wanashauri watu kufanya manunuzi ya chakula ambacho si rahisi kuharibika, kama vile; mchele, unga, mafuta, maharage na vyakula vingine ambavyo havihitaji kuwekwa kwenye jokofu ili visiharibike.

Aidha bidhaa nyingine wakilalamikia kuwa si rahisi kuhifadhi hasa umeme ukiwa si wa kuaminika katika mazingira wanayoishi, hivyo hofu ipo katika upande wa kupata hasara kwa vyakula kuharibika.

Hata hivyo kuna wengine wanatamani kujiandaa mapema lakini uwezo ni mdogo wa kuwawezesha kununua vyakula kwa wiki.

"Pesa ninayoipata, inaniwezesha kununua chakula cha siku moja tu, sina namna ya kujiandaa hata kama nikiwa na taarifa kuwa ni vyema kujiandaa."

Usalama wa chakula

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Usalama wa chakula

Kwa nini maeneo ya manunuzi si salama?

Hali ya maambukizi ikiendelea, namna ya kufika katika masoko au maduka kununua bidhaa yaweza kuwa si jambo rahisi kama tulivyozoea haswa katika mazingira yetu barani Afrika.

Ikumbukwe kuwa virusi vya corona vinasambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, pale mtu mwenye maambukizi anapokohoa na chembechembe za maambukizi kusambaa kwa wengine kupitia hewa, kugusana au kushika vitu ambavyo mtu mwenye maambukizi alivigusa.

Sokoni au kwenye maduka makubwa ni maeneo ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi yanatajwa kuwa ni eneo hatari katika kipindi hiki cha mlipuko.

Si rahisi kuepuka kusogeleana na watu kwa mita mbili ukiwa sokoni, ni muhimu watu kuzingatia hili wakati wa kwenda kufanya manunuzi.

Si sokoni tu, ndio eneo hatari, watu wengi bado wanashiriki kutumia mashine za kutolea ATM , usafiri wa umma, koki za kufungulia maji ambayo yako kwenye ndoo katika maeneo mbalimbali na hatari nyingine nyingi.

coronavirus

Taarifa zaidi kuhusu coronavirus:

Lakini kuna namna ya kujikinga na hatari hizo kwa sasa kabla ya tatizo halijawa kubwa :

  • Kunawa mikono kwa sekunde 20 kwa maji na sabuni au kutumia dawa ya kitakasa mikono(sanitiser) kabla ya kufanya manunuzi.
  • Kuepuka kugusa vitu sokoni na kufanya manunuzi wakati mapema
  • Kufanya malipo ya simu ili kuepuka kushika fedha

Chakula kilichoandaliwa tayari ni salama kiasi gani?

Hakuna ushahidi unaosema kuwa ugonjwa wa Covid-19 unaweza kuambukizwa kupitia chakula au wadudu wanaweza kufa kama chakula kikiwa kimepikwa.

Kuagiza chakula ukaletewa nyumbani kunaweza kukapunguza hatari ya maambukizi zaidi ya mtu mwenyewe kwenda kununua.

Hatari ya maambukizi inaweza kuwepo kwenye kile kilichofungashia chakula, na mtu aliyeleta mzigo.