Coronavirus: Prince Charles sasa anaweza kutangamana baada ya kukutwa na virusi vya corona juma lililopita

Prince Charles

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Mwanamfalme wa Uingereza Charles sasa yuko huru kutangamana na watu wengine, baada ya kumaliza siku saba za kujitenga toka ilipobainika kwamba ameambukizwa virusi vya corona.

Prince Charles, 71, alijitenga Uskochi, na aligundulia kuambukizwa ugonjwa huo baada ya kuonesha dalili za wastani.

Mke wake Duchess of Cornwall, 72, pia alipimwa lakini hakupatikana na virusi lakini akaanza kujitenga.

Afisa katika jumba la kifalme, alisema mwanamfalme alikuwa katika hali nzuri kiafya na alikuwa anafuatilia masharti ya serikali.

"Makazi ya kifalme Uingereza yamethibitisha leo kwamba baada ya kuwasiliana na daktari, Mwanamfalme wa Wales kwa sasa yuko huru kutangamana na wengine," kulingana na msemaji.

Mwanamfalme Charles alikuwa kwa karantini kwa siku saba katika nyumba ya Birkhall kwenye makazi ya kifalme ya Balmoral.

Kulingana na miongozo ya serikali, yeyote mwenye dalili anastahili kuwa kwenye karantini kwa siku saba, huku kila mmoja anayeishi kwenye makazi yao akitakiwa kujitenga kwa wiki mbili.

Prince of Wales greeting Pierce Brosnan (centre) with a Namaste gesture as he arrives at the annual Prince"s Trust Awards 2020 held at the London Palladium

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Mapema mwezi Machi, kabla ya serikali kutanganza sheria ya watu kutosongeleana, Mwanamfalme Charles alionekana kukwepa kusalimiana kwa mkono

Makazi ya Kifalme ya Buckingham awali yalisema kwamba Malkia mara ya mwisho kumuona kijana wake mrithi wa kiti cha Ufalme ni Machi 12, na alikuwa katika afya njema.

Hili linawadia huku watu wengine sita wenye virusi hivi wakiaga dunia huko Scotland, na kufikisha idadi hiyo hadi 47.

Idadi ya watu ambao wameaga dunia na virusi vya Corona Uingereza imefikia 1,228.

Miongoni mwa walioaga dunia Amged El-Hawrani, daktari mwenye umri wa miaka 55, mshauri wa maradhi ya masikio, pua na koo katika hospitali ya Malkia ya Burton.

Wiki iliyopita, daktari na mshauri wa kupandikizwa kwa viungo aliaga dunia baada ya kupatikana na ugonjwa wa virusi vya Corona.

Maelezo zaidi
Police officers from North Yorkshire Police stop motorists in cars to check that their travel is "essential", in line with the British Government"s Covid-19 advice to "Stay at Home", in York, northern England

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maafisa wa Polisi kutoka Kaskazini mwa Yorkshire wakisimamisha magari kukagua kama wanatimiza sheria zilizowekwa

Baadhi ya wafanyakazi 20,000 waliokuwa wahudumu wa afya wamerejea kazini kusaidia kukabiliana na janga la Corona. Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema, na kuongeza kuwa nchi hiyo nchi hiyo itapita mtihani huu kwa kushirikiana pamoja.

Karibia mmoja kati ya madaktari wanne hawapo kazini kwasasa ama kwasababu ya dalili za ugonjwa huu au kwa kujitenga kwakuwa wanafamilia wameonesha dalili za virusi vya corona kulingana na mkuu wa Chuo Kikuu cha Utabibu cha Royal.

Waziri huyo Mkuu ambaye alikuwa wa kwanza kutangaza kwamba anavirusi vya Corona ameendelea kuongoza juhudi za kukabiliana na janga hili na kufanya mikutano kwa njia ya video akiwa amejitenga.

Jumatatu, vyanzo vilithibitisha kuwa Dominic Cummings, mshauri wake mkuu ameonesha dalili za virusi vya Corona na kujitenga.

Wakati huo huo, Bwana Johnson amesema kuwa raia wameonekana kutii sheria zilizowekwa na serikali kama njia ya kupunza usambaaji wa virusi vya Corona na kuongeza kuwa utumiaji wa usafiri wa treni umepungua kwa asilimia 95 huku wa basi ukipingua kwa asilimia 75.

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video, Mambo matano muhimu kuhusu virusi vya corona