Coronavirus: Wanandoa waliodai virusi vya corona ni 'mzaha Tanzania' watiwa mabaroni

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa polisi katika mji mkuu wa kibiashara nchini Tanzania Dar es salaam wanawazuilia wanandoa kwa madai ya kusambaza uongo kuhusu habari za virusi vya corona.
Afisa mkuu wa polisi jijini Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema kwamba mwanamume huyo na mkewe waliikejeli serikali wakati wakiwa katika uchukuzi wa umma wiki iliopita.

Alisema kwamba wawili hao walikuwa wanaupotosha umma.
''Walisema kwamba virusi vya corona ni mzaha na kwamba serikali haina chakula kuwalisha wanafunzi hivyobasi inatumia janga hilo kama nafasi ya kufunga shule , taasisi na vyuo vikuu'', bwana Mambosasa aliambia waandishi.
Kulingana na afisa huyo wa polisi , baada ya kusikia matamshi hayo, abiria waliokuwa katika gari hilo walikasirishwa na kumuagiza dereva wa basi kulipeleka hadi kituo cha polisi kilichokuwa karibu.
Bwana Mambosasa amesema kwamba uchunguzi dhidi ya wawili hao Elias Mwita na Rosemary Mwita umekamilika na kwamba hivi karibuni watawasilishwa mahakamani.
Aliongezea kwamba tangu mlipuko huo wa coronavirus , maafisa tayari walikuwa wamewatia mbaroni watu wengine kwa kusambaza habari za uongo kuhusu mlipuko huo.

Chanzo cha picha, AFP
Kisa cha tatu charipotiwa Zanzibar
Wakati huohuo Kisiwa cha Zanzibar kimethibitisha mgonjwa mwengine wa virusi vya corona na hivyobasi kuongeza idadi ya walioambukizwa virusi hivyo kufikia watatu.
Kulingana na waziri wa afya katika kisiwa hicho Hamad Rashid Mohammed kisa hicho ni cha mwanamke Mtanzania aliyewasili kutoka Uingereza.
Hatua hiyo inajiri baada ya kisiwa hicho kufunga njia zote za kuingia na kutoka kuanzia jana siku ya Ijumaa tarehe 28 mwezi Machi.
Mwanamke huyo sasa nditye Mzanzibari wa kwanza kukutwa na virusi hivyo baada ya visa viwili vya kwanza vilivyohusisha wageni waliowasili katika kisiwa hicho cha kihistoria.
Kulingana na gazeti la The Citizen Tanzania, Wiki iliopita wizara ya Utalii ilipiga marufuku safari zote za ndege za kimataifa zilizotarajiwa kuwasili katika uwanja wa kimataifa wa Sheikh Abeid Karume.
Katika tangazo hilo mamlaka pia iliagiza karantini ya lazima kwa wale waliokuwa wakiwasili katika kisiwa hicho kwa gharama zao wenyewe.
Wiki iliopita Rais Magufuli aliagiza kuchukuliwa hatua wale waliokuwa wakisambaza habari za uongo.
Alisema kwamba ni waziri wa Afya, waziri mkuu ama yeye mwenyewe ndio walioruhusia kutoa habari kuhusu hali ya virusi vya corona nchini humo.
Kufikia sasa Tanzania imeripoti visa 13 vya ugonjwa wa corona, huku raia wanane wakiwa Watanzania na wengine watano wakiwa wageni.
Mmoja ya wagonjwa 13 tayari amepona.













