Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Joyce Elias: Msichana mwenye ulemavu wa ngozi anayekabiliana na changamoto za familia na jamii kufikia malengo yake
- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC, Dodoma
- Iliyochapishwa
Joyce Elias Simon ni binti wa miaka 13 mwenye ulemavu wa ngozi ,ni miongoni mwa mabinti wa kitanzania ambao maisha yao kwa ujumla na safari yao ya elimu ilijawa na misukosuko.
Anatoka katika wilaya ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma ambayo ni miongoni mwa wilaya ambazo zinakabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni na watoto wa kike aidha kukatiza masomo au kutoendelea kabisa baada ya kumaliza darasa la saba.
Vilevile, katika hali isiyo ya kawaida, wilayani humo pia, baadhi ya wazazi wamekuwa na sifa ya kuwataka watoto wao wafeli kwa makusudi mitihani ya darasa la saba kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutaka kuwaozesha wakiwa na umri mdogo.
Joyce ambaye awali alikataliwa na baba yake kwa sababu ya kuwa mlemavu, nae aliingia kwenye mtego huo ingawa tofauti na wasichana wengine, yeye aliweza kujinasua.
"Nilipofika darasa la saba, zilinijia sauti nyingi, ambazo zilikuwa zinaniambia nisifanye vizuri kwenye mtihani wangu wa kumaliza shule ya msingi," anasimulia Joyce na kuongeza, "Ila mimi sikuzisikiliza. Nikaendelea kumuomba Mungu. Nikafanya mtihani vizuri, na kwa bahati nzuri nikachanguliwa shule ya vipaji maalumu."
Hata hivyo, furaha yake iliingia doa pale alipogundua kuwa safari yake ya kufika Mkoani Singida, katika kijiji cha Kinampanda, wilaya ya Iramba ambapo ndipo ilipo shule ya Sekondari ya Tumaini anapotakiwa kwenda haikuwa rahisi.
Safari yake iligubikwa na changamoto tele, kwanza mbali na pingamizi kutoka kwa wazazi wake na wanakijiji kwa ujumla ambao awali hawakutaka asome mbali na eneo analotoka kwa kuhofia kwamba yeye ni mlemavu wa ngozi, lakini pia uwezo mdogo wa familia yake wa kumpeleka shule ulikuwa ni kigingi.
"Nilipochaguliwa, zilijitokeza baadhi ya changamoto, uwezo wa nyumbani ulikuwa mdogo nikawa nashidwa kuja shule. Lakini namshukuru Mungu alionesha njia pasipo na njia. Jumuia ya watanzania waliosoma nchini Australia pamoja na afisa maendeleo ya jamii Sofia Swai, wakanisaidia. Nawashukuru sana," alisema Joyce.
Unaweza pia kusoma:
Akiongea kwa sauti ya chini pindi alipokutana na mwandishi wa makala hii katika Shule ya Tumaini, Joyce anasema matokeo yake ambayo yalikuwa ni mazuri yaliwashtusha wengi kijijini kwao, na kuongeza kusema kuwa, hii ni dalili tosha kwamba, iwapo watoto wa kike hawatashawishiwa na wazazi wao kujifelisha, basi idadi ya ufaulu itaongezeka.
Na ni kwa sababu hiyo, hivi sasa Joyce, amekuwa mwanaharakati chipukizi ambapo anapokuwa likizo, usishangae kumuona katika baadhi ya shule za wasichana akitoa hamasa kwa wengine.
Huku akishikwa mkono na wanaharakati wengine wabobezi, anasema anaona kazi yao imeanza kuzaa matunda.
"Mabinti wenzangu wanavyoniona wanapata hamasa. Baadhi wanasema laiti na wao wangejua. Wapo wengine wameolewa na wengine wana watoto. Wanasema maisha ni magumu, bora mimi niliyegundua mapema kwamba elimu ina umuhimu," anasema Joyce.
Khonorata Joseph Mbiaji, ambae ni mwalimu mkuu wa shule ya Sekondari ya Tumaini anasema, Joyce ni binti anayejituma na ni kati ya wanafunzi wanaofanya vizuri.
"Pamoja na hali yake ya ualbino lakini anasimamia nafasi yake vizuri, pia ni binti mtulivu tofauti na mabinti wengine ambao ni wasumbufu," anasifu mwalimu Mbiaji.
Rhoda Mtune mkazi wa kijiji cha Nzali, katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, anasema katika eneo hilo, ni jambo la kawaida kuona baadhi ya wazazi wakiwaambia watoto washindwe mitihani makusudi kutokana na hali duni. Rhoda anasema wengine hawana uwezo hata wa kununua vitabu.
Unaweza pia kutazama:
Lakini tamaa ya mali pia imeelezwa kuwa chanzo cha baadhi ya wazazi kutaka watoto wao wa kike kufeli.
"Wazazi wanataka watoto waolewe wakiwa na umri mdogo. Ni tamaa ya mali tu," anasema Rosa Musa Mhina.
Kwa upande wake, Esther Paul Gerson, afisa mtendaji wa kijiji cha Mahamha anasema katika miaka mitatu iliyopita, hali imebadilika kutokana na viongozi wa serikali kukemea tabia hiyo.
Katika risala maalumu iliyowasilishwa siku ya wanawake Duniani na Asha Vuai ambae ni mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii katika wilaya ya chamwino, imeelezwa kwamba, licha ya jitihada za serikali na mashirika mbalimbali kuendelea kuelimisha jamii lakini ukatili ya kijinsia bado umeendelea kujitokeza.
Hata hivyo, mimba kwa wanafunzi zinaarifiwa kupungua kutoka 29 kati ya wanafunza 3,604 sawa na 0.8% kwa mwaka 2018 hadi kufikia 7 kati ya wanafunzi 3,647 kwa mwaka 2019 sawa na 0.2%.