Steve Kipepeo: Mwanamume anayefunza wanaume wenzake kuhusu hedhi Kenya

Steve kipepeo huwapatia wanume sodo wakati wa mazungumzo yake kuhusu hedhi ambayo huchukua takriban siku tano kwa mwezi.
Maelezo ya picha, Steve kipepeo huwapatia wanume sodo wakati wa mazungumzo yake kuhusu hedhi ambayo huchukua takriban siku tano kwa mwezi.
Iliyochapishwa

Raia mmoja wa Kenya anawahamasisha wanaume wengine kuzungumzia na kujifunza kuhusu hedhi na hivyobasi kufutilia mbali dhana potofu kwamba ni swala la wanawake pekee.

Steve Kipepeo ambaye anaishi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru katika mji mkuu wa Nairobi , anawazungumzia wanaume katika maeneo wanaokaa kama vile katika vilabu vya burudani na michezo ya pool.

Aliambia kipindi cha bbc cha Lifeclinic na Maisha kwamba alianza kuwafunza wanaume kuhusu hedhi baada ya kugundua jinsi wanawake katika jamii yake wanavyohitaji usaidizi.

''Wengi wa wasichana hapa hawana suluhu nzuri ya kutatua swala la hedhi. Wanalazimika kushiriki ngono na wanaaume ili wawanunulie sodo, ama hata makaratasi ya tishu. Wanawatumia vibaya na hata kukatiza masomo yao''

''Wanalazimika kutumia vipande vya godoro, nguo kukuu ama hata makaratasi ya tishu''.

Bwana Kipepeo alisema katika mazungumzo yake ya kwanza na wanaume kwamba anawapatia sodo ili kuwasaidi kubaini kwamba ni jambo la kawaida kuzishika.

''Wengi wao hawawezi hata kuchukua sodo hizo. Hunitazama kwa tabia fulani''.

''Wanaamini kwamba ni mwiko kuzungumzia kuhusu hedhi . Hawaelewi kwamba ni muhimu kujifunza kile ambacho wasichana hupitia wakati wapo katika hedhi.

Anatumaini kwamba atalifanya jambo la hedhi kuwa la kawaida ili kuweza kuungwa mkono na wanaume.